WACHEZAJI WAPYA WENYE ITC RUKSA KUTUMIKA
SHIRIKISHO
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limefanya marekebisho ya kanuni za
usajili ambapo sasa mchezaji ambaye usajili wake utakuwa umepita kwenye
mfumo wa mtandao wa Transfer Matching System (TMS) atapewa leseni na
kuitumikia moja kwa moja timu yake mpya.
TFF
itatoa leseni ya usajili wa mchezaji ambaye amethibitishwa kupitia
mtandao wa TMS baada ya kuwepo nyaraka zote; mkataba uliomalizika, barua
ya kuvunja mkataba, barua ya kuachwa (release letter), mkataba mpya na
uthibitisho wa makubaliano kati ya klabu zinazohusika.
Licha ya
mchezaji kupata leseni, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji bado
itakuwa na mamlaka ya kushughulia upungufu, malalamiko ya kiusajili,
pingamizi na uhalali wa kimkataba kati ya pande mbili (mchezaji na
klabu).
Wachezaji
wote wa kigeni waliosajiliwa kwa ajili ya kucheza Ligi Kuu ya Vodacom
(VPL) wanapaswa kulipiwa dola za kimarekani U$ 2,000 kwa kila mmoja
kabla ya kupatiwa leseni na kuanza kuzitumikia klabu zao katika michuano
ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho.
Pia TFF
kupitia kamati ya sheria na hadhi za wachezaji inaweza kumruhusu kwa
kipindi maalum mchezaji mwenye dosari acheze kwa leseni ya muda
(provisional license) hadi dosari hizo kati ya klabu na klabu
zitakapomalizwa. Iwapo dosari hizo hazitakuwa zimemalizwa, mchezaji
anaweza kuzuiwa kucheza na klabu husika kuadhibiwa.
Timu zote
za Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili zinatakiwa
kufuatilia TFF kujua wachezaji ambao hawana pingamizi na leseni za
wachezaji waliopitishwa wanaweza kuanza kutumika kuanzia kesho tarehe
18/12/2015 na kwenye michezo ya kombe la Shirikisho (FA Cup) kama
hawakuwa wamecheza raundi ya kwanza kwenye vilabu vya zamani.
Comments
Post a Comment