Wapiganaji wa IS kuondoka kusini mwa Damascus
Na RFI
Nchini
Syria, makubaliano yaliowashangaza wengi yamefikiwa juu ya kuondoka
Jumamosi hii kwa watu 4000 katika maeneo matatu kusini mwa mji wa
Damascus.
Watu hao
ni pamoja na wapiganaji wa kundi la Islamic State (IS), wapiganaji wa
kundi la Al-Nusra Front na raia wa kawaida, vyanzo vilio karibu na
mazungumzo vimebaini Ijumaa Desemba 25.
Hii ni
mara ya kwanza kwa mkataba kama huu unaolishirikisha kundi la Islamic
State. Mkataba huu unaruhusu watu 4000, ambao ni raia pamoja na
wapiganaji hasa wa kundi la Islamic State na wale wa kundi la Al-Nusra
Front, kuondoka katika kambi ya wakimbizi wa Palestina ya Yarmuk, kusini
mwa mji wa Damascus, na maeneo jirani ya miji ya Qadam na Hajar al
Aswad.
Kwa
mujibu wa chanzo cha serikali ya Syria, utekelezaji wa makubaliano hayo
unapaswa kuanza Jumamosi hii Desemba 26. Watu hawa 4000 watahamishiwa
katika mji wa Raqqa, "mji mkuu" wa kundi la Islamic state, kaskazini mwa
Syria, au katika mji wa Marea, katika jimbo la Aleppo, kwenye mpaka na
Uturuki, unaoshikiliwa na makundi ya waasi wa Kiislam na kundi la
Al-Nusra Front.
Kwa
mujibu wa chanzo cha serikali ya Syria, kikosi cha askari kiliingia
katika mji wa Qadam Alhamisi Desemba 24 ili kuchukua magari na vifaa vya
kijeshi. Mabasi kumi na nane yamewasili katika eneo hilo na yako tayari
kuwasafirisha. "Kila mpiganaji ataruhusiwa kuondoka pamoja na familia
yake, sanduku moja na silaha yake binafsi", mwakilishi wa serikali
katika eneo hilo amesema.
Siku za
nyuma majaribio manne kama hayo yalishindikana, chanzo hicho cha
serikali kimebaini. Kuondoka huko ni matokeo ya mazungumzo yalioanzishwa
miezi miwili iliyopita kati ya serikali na wawakilishi wa wakazi wa
maeneo matatu kusini mwa mji mkuu wanaosumbuliwa na kuzorota kwa kiasi
kikubwa kwa hali ya maisha. Inaarifiwa kuwa hali hiyo imesababishwa na
kuzingirwa kwa maeneo hayo na jeshi la serikali tangu mwaka 2013,
shirika la Haki za Binadamu nchini Syria (OSDH) limebainisha.
Kambi ya
Yarmouk inawahifadhi karibu raia 7000 wa Palestina na Syria, dhidi ya
watu zaidi ya 160,000 kabla ya kuanza kwa machafuko mwaka 2011. Mwezi
Aprili, Makundi ya Islamic State na Al-Nusra Front yalikua yaliiteka
kambi hiyo kwa 60% kabla ya kurudi nyuma kwa 40% ya eneo hilo.
Comments
Post a Comment