Mwl. Mndeme: Rais Magufuli amelianzisha, na sisi tulitibue
Leo
(9/12/2015) siku ya kukumbuka Uhuru wa nchi yetu toka kwa mkoloni wa
kingereza, niliamka mapema nikikimbizana ra ratiba na nikiwaza mambo
kadhaa. Nilisikitika sana baadaye kugundua kwamba nimewapeleka watoto
wangu shule bila kuwaambia kwamba leo ni siku ya uhuru wa nchi yetu.
Nimewafundisha
watoto wangu mambo mengi kuhusu nchi yetu na nimezoea kuwaeleza kwa
undani kuhusu historia yake, viongozi wake, rasilimali zake, vivutio
vyake, na uzuri wake. Nimewafundisha kuiombea Tanzania na viongozi wake
kila siku kwa sababu mafanikio ya Tanzania ni mafanikio yao ya leo na
siku za mbeleni; na kwamba kwa amani na furaha ya Tanzania nao watakua
na amani na furaha. Jioni tulipoketi nao kwa ajili ya chakula
nililaazimika kuwaeleza nilichosahau asabuhi. Baada ya kunisikiliza,
binti yangu wa miaka 7 aliniuliza ninamaanisha nini kusema “siku ya
Uhuru”. Nilichukua muda kidogo kutafuta lugha nyepesi kuwaelezea dhana
ya ukoloni na jinsi wazee wetu walivyopambana kutafuta kuwa huru
wakiongozwa na akina Mwalimu Nyerere na wenzake.
Maswali
ya watoto wangu yamekua yakizunguka kichwani mwangu na nimejiuliza ni
watoto wangapi wakitanzania wa shule za msingi na sekondari wanaelewa
maana ya siku ya Uhuru. Watoto na vijana wetu wanaelewa Uhuru huu ni wa
aina gani au ni wa kitu gani? Je, wanaelewa nani walituletea uhuru na
kwa nini walifanya hivyo? Je, watoto na vijana wetu wanajua nini
kilifanyika hadi tukapata uhuru? Je, wanajua majina mangapi ya babu na
bibi zao waliotutafutia uhuru? Zaidi ya yote, Uhuru una maana gani kwao
leo hii?
Nimejiuliza
maswali haya baada ya kujitathimini mimi mwenyewe kuhusu mantiki ya
siku ya Uhuru kwa zaidi ya miaka 28 tangu nilipoanza kupata uwezo wa
kuelewa mambo ya kitaifa, kama sherehe za siku ya Uhuru. Ndani ya miaka
yote hiyo, sikumbuki kujisikia kwamba mimi ni sehemu ya sherehe hizo.
Huenda ni kosa langu kujiona hivyo lakini huenda inatokana na ukweli
kwamba dhana ya sherehe za Uhuru haikuingizwa kwenye fahamu na hisia
zangu kwa namna ya kunifanya nijione ni sehemu ya historia hiyo.
Maadhimisho ya siku hii hayajawahi kuwa rafiki sana kwangu. Kwangu siku
ya uhuru imekua ni siku ya Rais kwenda “kujisikia vizuri”
kama mkuu wa nchi pale uwanja wa taifa kwa kukagua gwaride la majeshi
yetu ya ulinzi na usalama na kupigiwa mizinga 21; ni siku ya Rais
kusindikizwa na msafara mkubwa wa “magari ya kifahari” na pikipiki za kijeshi; ni siku ya kuona halaiki ya watoto wakionesha uwezo wao “mbele ya Rais na wageni wake wa kimataifa”; ni siku ya kuona watu wengi waliovalia sare wakipamba muonekano wa uwanja wa taifa na “kumpungia Rais kwa tabasamu”; ni siku ya kutazama ngoma na Sanaa huku wasanii “wakijitahidi kufanya Rais afurahi”;
ni siku ya kuonesha silaha za kivita na kushuhudia viongozi wote
wastaafu wakikutanika mahali pamoja. Nimezoea kuiona siku hii ikiisha
kwa kusikia Rais amefanya hafla ya kitaifa pale Ikulu ya Magogoni kukiwa
kumealikwa “waateule wenye connection” kufurahia dhima hii pamoja na mabalozi.
Nimekua
nikipitia hali hii pamoja na ukweli kwamba nimesoma shule za msingi
kule kijijini ambapo tulikaa chini kwenye vumbi tukijifunza mwandiko na
vibao vya chaki. Kule tulipokua hatuna madarasa wala madawati na
kutulazimu kujifunzia nje na kukalia matofali iwapo yalipatikana. Enzi
zile ambapo hatukua na shule ziitwazo “English Medium” na tulifundishwa Sayansi kimu, na somo la Siasa.
Pamoja na hali hii, tulifanya kazi za mikono za shamba kwa muda mrefu
kuliko muda wa darasani; tulikimbia mchakamchaka kila siku asubuhi wengi
tukiwa hatuna viatu; tulitembea gwaride kila siku asubuhi tukiimba nyimbo za uhuru na uzalendo huku nikiwa mpiga ngoma au filimbi; tuliimba nyinyo za kumsifu Mwalimu Nyerere na kuhamasishwa ahadi za mwana TANU na kazi za ujamaa na kujitegemea.
Kama mimi niliyeyapitia haya nimekua nikijisikia mauzauza kuhusu siku ya Uhuru wetu, je watoto na vijana wa ulimwengu huu wa “fesibuku”, “wasapu”, “twita”, “intaneti” na “instagramu”,
wanaelewa nini kuhusu Uhuru? Kwao una maana gani? Uhuru wa Tanzania ni
nini kwao na ni Uhuru upi? Ni wangapi wa vijana na watoto wetu wanajua
dhana na mantiki ya uhuru wetu kwa upana, kina, kimo na marefu
yanayotakiwa? Wanajua nini kuhusu fikra zilizowasukuma wazee wetu
kuijenga nchi yetu kwa gharama na uchungu mkubwa?
Rais wetu Dr. John Pombe Magufuli ameamua kilianzisha mwaka huu. Kitendo chake cha kuhamasisha shughuli za usafi nchi nzima siku ya uhuru kilimepelekea kila Mtanzania kuikumbuka na kuitafakari siku ya Uhuru wetu. Ametugusa na kutukumbusha msingi wa utaifa wetu uliojengwa katika misingi ya Uhuru wa mwaka 1961 na watu wote wamesikia. Kwenye mitaa yetu, nyumba zetu, vyombo vyetu vya habari, na kwenye mitandao ya kijamii, mjadala ulikua mmoja tu nao ni SHEREHE ZA KIPEKEE ZA UHURU WA TANZANIA. Kwa mara ya kwanza mwaka huu nimeshuhudia vyombo vikubwa vya mataifa ya Ulaya na kwingineko Afrika wakitumia muda wao kutangaza habari za SIKU YA UHURU WA TANZANIA. Uhuru umeongelewa na watanzania wa mijini na wa vijijini; wanene wa Masaki na wembamba wa Tandale; wasomi wa UDSM na wafanyabishara wa Tunduma; wafupi wabishi wa kule kwetu Lushoto na warefu wajivuni wa kule Bukoba kwa kina Tibairwagamanyuka; wakali wagomvi wa kule Mara na wapenda raha na vijembe wa kule Bagamoyo; wake kwa waume; watoto kwa wazee. Kila Mtanzania kakumbushwa dhana ya uhuru.
Mwl Mndeme |
Kwa
mara ya kwanza, nimejisikia sehemu ya sherehe za Uhuru wan chi yangu.
Kwa mara ya kwanza nimejisikia fahari kuongelea habari za uhuru wan chi
yangu mbele ya watu wa mataifa mengine. Kwa mara ya kwanza nimejivuna
mbele ya watu wa mataifa mengine juu ya maamuzi na maelekezo ya rais wan
chi yangu. Kwa mara ya kwanza nimeiona tarehe tisa kama siku ya umuhim
mkubwa kwangu na familia yangu. Kwa mara ya kwanza nimepata sababu ya
kuutafakari uhuru na utaifa wetu kwa undani na kwa mapana zaidi. Kwa
mara ya kwanza nimeweka pembeni mapenzi yangu ya kutazama mbwembwe za
kiusalama na ulinzi na kufurahia kuona Rais wangu akizoa taka pamoja na
walinzi wake. Nimepata sababu nyingine kubwa ya kufikiri ni nini mchango
wangu kwa taifa langu na ni kwa kiasi gani bado sijawajibika. Rais Dr.
Magufuli katufungulia ukurasa mpya kwa hekima kubwa, busara, na uzalendo
usiojengwa katika mbwembwe na vijembe vya kisiasa.
KWA KITENDO HIKI, DR MAGUFULI KALIANZISHA NA SISI HATUNA BUDI KULITIBUA. Ni wakati mwafaka kwa kila mtanzania kuona sababu ya kukumbuka matendo makuu ya nchi yetu likiwemo la uhuru na utaifa wetu. Ni wakati wa sisi kuwafundisha watoto na vijana wetu kuelewa kwa nini uhuru wetu ulikua ni tendo kubwa na la kihistoria. Kuwakumbusha na kuwafundisha nini wazee wetu walipitia na maisha yao yalikuwaje ikilinganishwa na sasa. Kuwasimulia habari za mashujaa na wajenzi wa kwanza wa uhuru wetu kama akina Mwalimu Nyerere, Bibi Titi Mohamed, Sir George Kahama, Mzee Kingunge Ngombari Mwiru, Oscar Kambona, Chifu Abdallah Fundikira, Abeid Amani Karume, Profesa Abdurhaman Babu, Tito Okelo, Mzee Kawawa, Bi Shariffa binti Mzee, Ali Migeyo, Sheikh Hassan bin Amir, Oseph Kasella Bantu, Ali bin Abbas, Maalim Mohamed Matar, Abdulwahid Sykes, Abdallah Shomari, Nasoro Kalumbanya, Jumbe Tambaza, Patrick Kunambi na wengine wengi mbao walifanya kazi kubwa ingawa majina yao hayakua maarufu.
Kuanzia
majumbani mwetu, vijiweni na mashuleni, vijana na watoto wetu wajue
utaifa wetu umetoka wapi. Wajue kwa nini sisi ni watanzania. Wajue kwa
nini wanalazimika kuijenga nchi yao. Wajue dhana ya UHURU NI KAZI na
inavyoongezewa uzito na ile ya HAPA NI KAZI TU. Wajue kwa nini
wanalazimika kuipenda nchi yao na kwa nini wawe tayari kutumika kwa
ajili ya taifa lao. Tuwakumbushe misingi ya Ahadi za mwanaTANU
zilizojenga uzalendo wetu. Waelewe tuliwezaje kumpiga Nduli Iddi Amini
katika hali ya umaskini na uchanga wa taifa letu. Wajue kwa nini wazee
wetu walinzisha Azimio la Arusha na kwa nini haliko leo na ina maana
gani katika utaifa wetu.Wajue nini kitaufanya uhuru wetu kuwa na maana
na uzito na ni kwa jinsi gani wao wanakua sehemu ya tunu hii kubwa hata
kama hawakuhusika wala kuwepo wakati tunaipata.
Magufuli kalianzisha na sisi lazima tulitibue
ili kurudisha dhana ya utaifa na uzalendo kwa nchi yetu na wananchi
wake. Kurudisha uwajibikaji, kupenda kazi, kujituma, na kujitolea kwa
manufaa ya wengi. Kurudisha roho ya ufahari na kujivunia utanzania wetu
na kila kinachotutambulisha nje na ndani ya mipaka yetu. Tuwasaide
watoto wetu kuelewa uzito na msingi wa maadhimisho ya uhuru wetu ili
wasiwe na mawazo kama ya mtoto wangu aliyepata ujasiri wa kunaimbia
haikua “fair” kuadhimisha siku ya Uhuru wa nchi yetu bila gwaride la
kijeshi. MAGUFULI KALIANZISHA NA SISI TULITIBUE.
Mwalimu MM (mmmwalimu@gmail.com blog: www.mwalimumm.blogspot.com )
Comments
Post a Comment