Polisi, makampuni binafsi na vitengo vya ulinzi wazindua "WhatAapp group" maalumu kupeana taarifa



Mkuu wa Operesheni wa Jeshi la Polisi Mkoani Arusha (ACP) Edward Balele akifungua kikao kati ya Jeshi hilo na Taasisi za ulinzi kujadili mustakabali wa usalama ndani ya mkoa huu. Kikao hicho kilifanyika katika ukumbi wa Bwalo la Polisi Jijini hapa (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha

Jeshi la Polisi mkoani hapa limeazimia kushirikiana na makapuni binafsi ya ulinzi na taasisi za ulinzi kutoka UN-ICTR, UNMICT, kitengo cha ulinzi cha B.O.T pamoja na Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu katika kupeana baadhi ya taarifa za uhalifu na wahalifu mara kwa mara kwa njia mtandao wa kijamii wa “WhatsApp”.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa Operesheni wa Jeshi hilo mkoani hapa (ACP) Edward Balele wakati akifungua kikao kilichofanyika katika Bwalo la Polisi mjini hapa alipokuwa anazungumza kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoani hapa mwishoni mwa wiki kati ya Jeshi hilo na wawakilishi wa Makampuni 31 ya Ulinzi, Benki Kuu Kanda ya Kaskazini, Mahakama ya Afrika ya Haki za Kibinadamu,UN-ICTR na UNMICT.

Mkuu huyo wa Operesheni alisema kwamba imefika wakati sasa kwa taasisi hizo kuzidi kuimarisha mahusiano kwa ukaribu huku njia za kisasa za mawasiliano zikitumika katika kupeana taarifa za uhalifu na pia kubadililishana uzoefu katika masuala ya ulinzi na usalama.

Alisema awali taarifa juu ya matukio mbalimbali sio kwamba zilikuwa hazipatikani bali zilikuwa zinawafikia walengwa kwa mtindo wa ujumbe mfupi yaani SMS lakini kwa kutumia mfumo wa kikundi cha “WhatsApp” ambacho kitapewa jina maalum, taasisi hizo zitakuwa zinapata na kutoa taarifa kwa pamoja na kila mhusika atakuwa anachangia mawazo yake huku wanachama wengine wa kikundi hicho wakiwa wanaona ushauri wa kila mchangiaji.

Aidha mbali na uundaji wa kundi hilo litakalotumia mtandao huo wa kijamii mbao umeshika kasi katika mawasiliano pia aliyaomba Makampuni hayo kutoa ushirikiano zaidi hasa kwa kutoa rasilimali vifaa pamoja na askari katika kuelekea mwisho wa mwaka kwa nia ya kufanya doria ya pamoja hivyo kudhibiti vitendo vya uhalifu ndani ya Mkoa wa Arusha.

Kwa upande wake Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Arusha (SSP) Muliro Jumanne Muliro alisema kwamba Jeshi la Polisi na Makampuni hayo kila chombo kikiwa kinawajibika ipasavyo katika nafasi yake mafanikio ya kudhibiti vitendo vya uhalifu yatakuwa makubwa.

Alisema anathamini mchango mkubwa unaotolewa na Makapuni hayo ya Ulinzi kwani matukio mengi ya uvunjaji wa Maghala ya viwanda, Ofisi mbalimbali na Makampuni yamepungua ukilinganisha na miaka ya nyuma kabla Makapuni hayo ya Ulinzi kukubaliwa kisheria.

Mkuu huyo wa Upelelezi alisema kwamba wakati wa uajiri wa askari hao wanatakiwa waangalie mambo mablimbali ikiwemo akili ya kuweza kugundua kitu kinachoashiria uhalifu, kuwa mwaminifu, kuwa mtulivu na kuwa mvumilivu na kusema kwamba huwa anafadhaishwa sana pale anapopata shauri linalomhusisha askari yoyote katika uhalifu hali ambayo inatia doa na aibu kwa taasisi zote za Ulinzi.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Polisi Jamii Mkoa wa Arusha Mrakibu Mwandamizi wa Jeshi la Polisi (SSP) Mary Lugola ambaye alizungumzia juu ya huduma bora kwa Mteja ambapo aliwataka Wawakilishi wa Makampuni hayo kuwaelekeza askari wao kuwa, wawe na lugha nzuri kwa wateja wao jambo ambalo pengine litakuwa linazidi kuwavutia wengine na hatimaye kupata malindo mengi ambayo yatawaongezea kipato, mbali na hilo pia aliwataka kutotumia nguvu kupita kiasi katika ukamataji ili kupunguza madhara makubwa yanayoweza kutokea.

Kwa upande wake Mkuu wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) Mkoa wa Arusha (SSP) Ramadhani Giro yeye aliyataka makampuni hayo kufanya mazoezi ya mara kwa mara na alisema baadhi ya Makampuni ya Ulinzi huwa yanapata mafunzo mbalimbali kama vile matumizi sahihi ya silaha, ukakamavu na mbinu mbalimbali za kuweza kubaini uhalifu na wahalifu toka kwa askari waliopo katika kikosi hicho na kutoa wito kwa askari wa makapuni mengine kujitokeza ili waweze kupata mafunzo hayo na kupunguza madhara yanayoweza kutokea huko mbeleni.

Wakichangia katika kikao hicho baadhi ya wawakilishi wa Makampuni ya Ulinzi, Mwakilishi toka Kampuni ya KK Security ambaye pia ni Meneja Mkuu wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini Bw. Claude Herssens alilisifu Jeshi la Polisi mkoani hapa kwa kuitikia wito kwa haraka pindi wanapoomba msaada na kuongeza kwamba mtandao huo utawasaidia sana na hivyo kuwafanya wajue tukio ambalo wanatakiwa kwenda kutoa msaada nje ya mipaka yao ya kazi na tukio ambalo litakuwa linawahusu Polisi pekee.

Naye Katibu wa Chama Cha waajiriwa wa Makampuni Binafsi Kanda ya Kaskazini (TUPSE) Aisha Masoud alizidi kusisitiza kwamba bado baadhi ya Kampuni hizo zinachangamoto hasa katika suala zima la mishahara ya wafanyakazi wao japokuwa serikali toka mwaka 2013 mwezi Agosti ilishatangaza mishahara mipya lakini baadhi yao hawajatekeleza hilo na kuwataka wafanye hivyo pamoja na kuwaingiza katika mifuko ya Jamii.

Mara kwa mara Jeshi la Polisi Mkoani hapa limekuwa likifanya vikao na Makapuni ya Ulinzi lengo likiwa ni kukumbushana majukumu ya utendaji wa kazi za kila siku hali ambayo inasababisha kuimarika kwa hali ya usalama.

Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ulinzi ya KK kanda ya Kaskazini Claude Herssens akichangia mada katika kikao kilichoandaliwa na Jeshi la Polisi Mkoani hapa na kuziusisha taasisi mbalimbali za ulinzi (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)

Baadhi ya washiriki wa Taasisi za Ulinzi wakiwa wanasikiliza moja ya mada kwa umakini ili baadae waweze kutekeleza kwa vitendo. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha

Katibu wa TUPSE kanda ya Kaskazini Aisha Masoud akielezea umuhimu wa mikataba baina ya waajiri na waajiriwa wa Makampuni ya Ulinzi. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)

Mkuu wa Upelelezi ya Makosa Jinai Mkoa wa Arusha (SSP) Muliro Jumanne Muliro akielezea athari za kuwa na waajiriwa ambao hawana sifa kwenye kazi za ulinzi. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi.

Mkuu wa Kitengo cha Polisi Jamii Mkoa wa Arusha (SSP) Mary Lugola akitoa elimu ya Huduma bora kwa mteja kwa Makampuni ya Ulinzi (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha

chanzo:wavuti

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA