Mkuu wa Mkoa Katavi asimamisha kazi watumishi 12 wa serikali
MKUU wa Mkoa wa Katavi, Dk Ibrahim Msengi
MKUU wa
Mkoa wa Katavi, Dk Ibrahim Msengi amewasimamisha kazi maofisa waandamizi
11 wa Manispaa ya Mpanda akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wake, Suleiman
Lukanga kwa ukiukwaji wa sheria za manunuzi kwa kufanya ubadhirifu fedha
zaidi ya Sh milioni 92.8.
Dk Msengi
alieleza kuwa Lukanga na maofisa 11 wa Manispaa ya Mpanda wanatuhumiwa
kununua gari la kubeba taka ambapo kiasi cha Sh milioni 92.8 zilitolewa
kwa manunuzi hewa kwa kampuni hewa.
Wengine
waliosimamishwa kazi ni Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Vincent
Kayombo ambaye pia ni Ofisa Elimu (Msingi) wa Manispaa ya Mpanda, Ofisa
Manunuzi aliyetajwa kwa jina moja la Kakulima, Ofisa Mipango, Ferdinard
Filimbi, Mweka Hazina, Bosco Kapinga, Mhasibu Kibi Hamis Msaka na
wajumbe wanne wa Bodi ya Zabuni.
Dk Msengi
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Mkoa huo,
ameamuru wakati uchunguzi kuhusu tuhuma hizo ukiendelea, watuhumiwa wote
12 wasitoke nje ya Mji wa Mpanda na wahakikishe wanalipa kiasi hicho
cha fedha kwa kuwa ni fedha za umma.
“Maofisa
hawa wa Manispaa na Mkurugenzi wao wanatuhumiwa kufanya malipo hewa,
ikiwa ni nusu ya fedha zilizotengwa kununua gari hilo hakika wamefanya
kwa makusudi ..... “Sasa naomba watupishe ili tufanye uchunguzi kwa
kuhusisha vyombo mbalimbali vya dola na wote wawe nje ya ofisi kuanzia
sasa, lakini wasitoke nje ya Mji wa Mpanda.....naagiza pia walipe kiasi
hicho cha fedha,” aliamuru.
Uamuzi
huo umechukuliwa na mkuu huyo wa mkoa kutokana na uchunguzi uliofanywa
na tume tatu tofauti zilizoundwa kuchunguza upotevu wa kiasi hicho cha
fedha ambazo ni kati ya Sh milioni 200 zilizotolewa na Tamisemi kwa
ajili ya kununulia gari la taka katika Manispaa ya Mpanda.
Aidha, Dk
Msengi ametoa onyo kwa mtumishi yeyote aliyezoea kufanya ubadhirifu wa
mali ya umma akisema wakae wakijua kuwa siku zao zimetimia na kwamba
tabia hiyo ovu haiwezi kufumbiwa macho.
Katika
uchunguzi wa upotevu huo wa kiasi hicho cha fedha uliofanywa na kamati
tatu tofauti zilizoundwa na RC huyo zilibaini kuwa Kampuni ya Bluecyon
iliyoko Mbezi, Dar es Salaam ilizawadiwa zabuni ya kununua gari hilo.
Uchunguzi
wa Kamati hizo tatu zilizoongozwa na Katibu Tawala Mkoa, Polisi Mkoa na
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuwa Bluecyon
ilikuwa haijihusishi na biashara ya magari, bali ni kampuni ya
uchapishaji.
Akizungumza
mjini Mpanda, Lukanga alisema, “Nilikuwa kikazi kijijini baada ya
kufika hapa mjini ndipo nimesikia agizo hilo la Mkuu wa Mkoa kwamba
amewasimamisha kazi watumishi 12 wa Manispaa ya Mpanda nikiwemo na mimi
niseme wazi kuwa agizo hilo tumelisikia.
“Hata
kabla ya RC hajatoa taarifa hiyo jana tayari nilikuwa nimeanza
kulishughulikia tangu mwaka jana na tayari baadhi ya watumishi wa
Manispaa wamefikishwa mahakamani. Mgogoro unakuja baada ya mzabuni huyo
kushindwa kuleta gari hilo la kubebea taka....basi nilichukua hatua
ikiwemo kuvunja mkataba na mzabuni huyo na kuhakikisha fedha hizo
zinarudi.
Chanzo:HabariLeo
Comments
Post a Comment