Walimu Wakuu kufukuzwa kazi - Naibu W. Elimu




Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Mhandisi Stella Manyanya (wa pili kulia) akikata utepe na Makamu wa Rais wa Kampuni ya Total, Jean-Christian Bergeron (wa tatu kulia) wakati wa hafla ya kukabidhi madawati 1000 yaliyotolewa kama msaada na Total kwa ajili ya Shule 10 za mikoa ya Dar es Salaam na Pwani. Makabidhiano hayo yalifanyika wilayani Bagamoyo jana. Kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Prof. Naomi Katunzi (kulia) na Kushoto anayeshuhudia ni mwanafunzi wa shule ya msingi Nianjema ya Bagamoyo, Ramadhani Issa. (Picha na Francis Dande)

SERIKALI imesema itawafukuza kazi walimu wakuu wa shule zote za msingi ambazo wanafunzi wake watashindwa kusoma, kuandika na kuhesabu kabla ya kuingia darasa la tatu.
Tamko hilo la serikali lilitolewa mjini Bagamoyo Mkoa wa Pwani na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, mhandisi Stella Manyanya wakati akipokea msaada wa madawati 1,000 kutoka kwa kampuni ya mafuta ya Total yatakayosambazwa katika shule 10 za mikoaya Dar es Salaam na Pwani.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, naibu waziri huyo alisema ili kuwa na elimu bora katika hatua za awali lazima wanafunzi kuanzia ngazi ya chekechea wajue kuhesabu, kusoma na kuandika kwa viwango vyao huku akisisitiza kwamba kabla ya mwanafunzi kuingia darasa la tatu lazima kusoma, kuandika, kuhesabu na kuelewa anachokifanya.

“Ni fedhaha unamkuta mwanafunzi wa darasa la tatu hajui kusoma kwa nini? Lazima kuna uzembe mahali sasa hili ni agizo na utekelezaji wake unaanza… tutapita huko kwenye mashule kukagua hili, tukibaini wapo wanafunzi hawajui hizi KKK hatuna sababu ya kuendelea na huyo mwalimu
mkuu. “…Tutamwambia atupishe akafanye shughuli nyingine, lazima walimu wawajibike,” alisema Injinia Manyanya baada ya kuwapa karatasi wasome na kuhesabu baadhi ya watoto wa shule za msingi waliokuwepo kwenye hafla hiyo na kusema elimu bora ni pamoja na kujua kusoma, kuandika, kuhesabu na kuelewa.

Naibu Waziri huyo pia aliipongeza Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), kwa kuhamasisha wadau mbalimbali kuchangia katika elimu hasa suala la madawati, ujenzi wa mabweni huku akisema taifa lina upungufu wa madawati 1,349,090 ambayo gharama yake ni sh bilioni 182.1 hivyo aliwaomba wadau wa elimu kuchangia.
Akizungumza kabla ya kukabidhi madawati hayo, Makamu wa rais wa Kampuni ya Mafuta ya Total, Jean-Christian Bergeron alisema gharama ya madawati hayo ni sh milioni 78 huku akibainisha kwamba kwa miaka mitatu kampuni yake imechangia madawati 3,000 yenye tahamani ya sh milioni 234 ambapo wanafunzi 9,000 wamenufaika nayo.


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Mhandisi Stella Manyanya (kushoto) akiwa amekaa katika madawati yaliyotolewa kama msaada na Kampuni ya Total. Katikati ni Makamu wa Rais wa Kampuni ya Total, Jean-Christian Bergeron, madawati 1000 yaliyotolewa na kampuni hiyo yakiwa na thamani ya shs. milioni 78 kwa ajili ya Shule 10 za mikoa ya Dar es Salaam na Pwani. Wa pili kushoto ni mwanafunzi wa shule ya msingi Nianjema ya Bagamoyo, Ramadhani Issa.

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA