Muhimbili yapata CT Scan mpya
Dar es Salaam. Serikali imeanza
kufunga mashine mpya ya vipimo ya CT Scan kwenye Hospitali ya Taifa
Muhimbili (MNH), ikiwa ni mkakati wa kukabiliana na tatizo la upungufu
wa vifaa tiba.
Kifaa hicho kimekuja wakati MNH ikihaha
kutengeneza mashine nyingine kubwa ya uchunguzi ya MRI kwa agizo la Rais
John Magufuli baada ya kukaa muda mrefu bila ya kufanya kazi na
kusababisha wagonjwa kulazimika kuchukuliwa vipimo kwenye hospitali
binafsi.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema jana kuwa
ameamua kumtafuta mbia mwenye mashine hiyo ili kuendana na jitihada za
kupunguza tatizo la wagonjwa kusubiri huduma ya uchunguzi kwa muda mrefu
wakati mashine hizo zinapoharibika.
Ummy, ambaye jana
asubuhi alifanya ziara yake ya kwanza hospitalini hapo, alisema baada ya
kutaarifiwa kwamba mashine hizo zimeharibika siku zilizopita, alifanya
mpango wa kuhakikisha inapatikana mbinu mbadala ili kupambana na tatizo
hilo.
“Tunachojaribu kufanya hivi sasa si kununua
mashine mpya. Hivi sasa watu wanatumia teknolojia mpya. Tumejifunza ili
uweze kufanya vizuri zaidi hununui kifaa, unanunua teknolojia ndiyo
matarajio yetu ya mbele.
“Tunamwambia mtu, tunataka
utufungie vifaa kadhaa na anahusika na matenengezo. Tunamwambia kwa
mwaka tutampelekea wagonjwa kadhaa,” alisema Mwalimu.
“Tumepata
mbia ambaye ana mashine ya CT Scan, kwa hiyo hivi sasa inafungwa na
tunategemea hadi kesho mchana (leo) huduma zitakuwa zimerejea. Muhimbili
inaendelea kutengeneza mashine ambayo imeharibika na kufikia Jumatatu
tutakuwa na mashine mbili za CT Scan,” alisema Mwalimu.
Alipoulizwa
kuhusu hatima ya mashine ya zamani na namna mkakati wa kuzidilisha ili
kuendana na kasi ya tekonolojia, Ummy alisema wataalamu wa Muhimbili
wameeleza kuwa sababu ni kutofanyiwa matengenezo kwa muda mrefu.
Hata
hivyo, alisema mashine hizo ni teknolojia ya zamani na zina vipande
sita wakati wengine wanatumia CT Scan zenye vipande 64 hadi 380.
Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Dk Lawrence Museru alisema hospitali hiyo
italipia gharama za wagonjwa wote wa dharura na wale wa msamaha ambao
watapelekwa hospitali binafsi ili kupatiwa huduma ya vipimo vya MRI na
CT Scan.
“Tutatoa huduma ya vipimo kwa wagonjwa wote wa
dharura watakaofika hospitalini kwa kipindi hiki ambacho mashine
zimeharibika, lakini wananchi watambue kwamba ubovu wa mashine hizi
unasababishwa na uchakavu wa vifaa na kutofanyiwa matengenezo ya mara
kwa mara,” alisema.
chanzo:mwananchi
chanzo:mwananchi
Comments
Post a Comment