MKAPA, MWINYI "WAGUSWA" NA SWISSLEAKS WAZIRI ASEMA "SI KOSA WATANZANIA KUWEKA FEDHA USWISS"
![]() |
91 client accounts opened between 1982 and 2006 and linked to 286 bank accounts.
(source: www.icij.org) |
UTARATIBU wa Watanzania kwenda kuhifadhi fedha katika mabenki ya Uswisi ulikithiri wakati wa utawala wa marais Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa, imefahamika.
Picha za grafu na zilizotolewa na mtandao wa Umoja wa Waandishi wa Habari za Uchunguzi Duniani (CIJ) na ambazo Raia Mwema imefanikiwa kuziona zinaonyesha kwamba wateja wengi kutoka Tanzania walipeleka fedha zao Uswisi katika kipindi cha kati ya mwaka 1988 na 2007.
Mwinyi alianza kuwa Rais wa Tanzania mwaka 1985 na kumaliza muda wake mwaka 1995 na Mkapa alianza mwaka huo na kumaliza awamu yake mwaka 2005.
Mtandao huo, kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali vya duniani, vimeibua taarifa hizo kutoka katika benki maarufu ya HSBC iliyoko Uswisi na habari hizi ni sehemu ya kampeni kali ya kupambana na ufisadi. Mtandao huo tayari umeibuka na taarifa kwamba Watanzania 99 wamehifadhi kiasi cha dola za Marekani milioni 114 katika benki hiyo, huku wakiwa na jumla ya akaunti 286. Hadi kufikia juzi usiku, ni Mtanzania mmoja tu, Sailesh Vithlani, ndiye ambaye anajulikana kuwemo katika orodha hiyo ya watu 99.
Lakini Raia Mwema limeahidiwa na vyanzo vyake kwamba litapatiwa majina ya Watanzania wengine 98 waliobaki. Taarifa hizo za uchunguzi ambazo zimepachikwa jina la “SwissLeaks” zinaonyesha kwamba katika kipindi cha kati ya mwaka 1982 ambapo ndipo taarifa hizi zimeanza kuvujishwa hadi mwaka 2006, wateja 91 kati ya 99 waliokuwa na akaunti Uswisi ndiyo walifungua kiasi hicho. Kwa maana hiyo, wateja wengine wanane walifungua akaunti zao katika kipindi cha kati ya mwaka 2006 na 2007. Mwezi Juni mwaka 2012, Benki Kuu ya Uswisi ilitoa taarifa iliyoeleza kwamba Watanzania wanahifadhi kiasi cha dola milioni 197 (zaidi ya Sh bilioni 313) katika akaunti mbalimbali nchini humo.
Kwa taarifa za sasa za SwissLeaks, ina maana kwamba ukiondoa dola hizi zilizopo HSBC, kuna takribani dola nyingine milioni 83 katika benki nyingine tofauti nchini Uswisi. Hii ni kama walioziweka hawajaziongeza au kuziondoa kwenye akaunti zao tangu Junui 2012. Hata hivyo, mwaka juzi, gazeti hili lilibaini kwamba pamoja na ukweli kwamba Uswisi ndiko kunakosifiwa, Watanzania wamehifadhi fedha nyingi zaidi katika Visiwa vya Jersey vilivyo chini ya Himaya ya Waingereza kuliko za Uswisi.
Gazeti liliwahi kuripoti kwamba fedha za Watanzania pekee zilizoko katika visiwa hivyo zinakadiriwa kufikia kiasi cha pauni za Uingereza milioni 413 (sawa na shilingi za Tanzania trilioni 1.06). Fedha hizo zinatosha kuhudumia bajeti za wizara za Afya, Mifugo na Uvuvi, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Wizara ya Afrika Mashariki kwa mwaka mzima bila ya kuomba fedha kutoka kwa wafadhili na bado ‘chenji’ ikabaki.
Gazeti hili haliwezi kutaja chanzo cha habari hizi kwa vile taarifa hii ilipatikana katika mkutano uliofanyika Uingereza wiki iliyopita chini ya kanuni za Chatham (Chatham Rules) ambazo zinakataza kutaja vyanzo vya habari zilizopatikana kutoka katika mikutano inayotawaliwa na kanuni hizo.
Kwa mujibu wa taarifa za uhakika zilizopatikana, Raia Mwema limeelezwa kwamba zaidi ya Jersey, kuna fedha nyingine nyingi katika visiwa vingine kama Cayman na Isle of Man ingawa pia kuna fedha zilizohifadhiwa jijini London, mji mkuu wa Uingereza.
“Kuna watu binafsi ambao wamehifadhi fedha zao. Kuna fedha za kampuni kadhaa na kuna fedha za inayoitwa mifuko ya hisani. Naweza nikashindwa kuwapa majina haswa ya wenye fedha hizo lakini nadhani inawezekana kuwapa majina ya kampuni na mifuko hiyo ya hisani (trusts),” kilieleza chanzo hicho.
Kisiwa hicho ni miongoni mwa nchi zinazopendwa na watu, kampuni au taasisi zinazokwepa kulipa kodi au zinazopata mapato yake kwa njia ya kifisadi kwa vile zinatoza kodi kidogo na zina sheria zinazolinda usiri wa walioweka mali zao. Mkutano huo ulielezwa kwamba visiwa hivyo vilivyo chini ya Uingereza lakini vinavyojitawala vyenyewe vimehifadhi kiasi cha pauni bilioni 40 kutoka Afrika na katika hizo, pauni milioni 413 zinatoka Tanzania.
Visiwa vya Jersey vilijipatia umaarufu mkubwa nchini Tanzania miaka michache iliyopita baada ya kubainika kwamba aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Tanzania, Andrew Chenge, alikuwa na akaunti katika visiwa hivyo ambayo ndiyo iliyotumika kumwekea fedha (dola milioni moja) zinazodaiwa kutokana na mauzo ya rada ya kampuni ya BAE Systems kwa serikali ya Tanzania.
- Taarifa kwa mujibu wa gazeti la Raia Mwema: Mkapa, Mwinyi ‘waguswa’ na mabilioni ya Uswisi
Mkuya: Siyo kosa Watanzania kuweka fedha Uswisi
![]() |
| 99 clients are associated with Tanzania. 20% have a Tanzanian passport or nationality. (source: www.icij.org) |
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, amesema siyo haramu kwa Watanzania kuweka fedha nje hivyo, Watanzania 99 waliotajwa kuwa na akaunti Uswisi haimaanishi wote wametorosha fedha.
Hata hivyo, amsema serikali inaangalia ripoti ya Swiss Leaks ili kuona uhalali wa akaunti hizo za siri.
“Sisi hatujaona kama ni kosa kwa Watanzania kuwekeza fedha zao kwenye mabenki ya nje na wala isionekane kama ni jambo haramu kabisa.
Kama serikali tungetamani wawekeze kwenye benki nchini ili kukuza sekta ya fedha lakini pia hatuwafungi kutowekeza nje,” alisema.
“Tunachofanya ni kuiangalia hiyo ripoti ili kujua ukweli wa taarifa hizo, lakini taarifa hiyo haimaanishi kwamba ni kosa kubwa kisheria kwa Mtanzania kuweka fedha nje,” alisema.
Mkuya alisisitiza kuwa hakuna shida yoyote kwa Watanzania kuweka fedha kwenye akaunti nje ya nchi.
Waziri Mkuya ameyasema hayo siku moja tu baada ya vyombo vya habari nchini kuripoti taarifa ya kuwapo vigogo 99 wa Tanzania kuficha mabilioni ya shilingi katika benki za Uswisi kutokana na ripoti ya mtandao wa Swiss Leaks chini ya Waandishi wa Habari za Uchunguzi wa Kimataifa (ICIJ).
Taarifa ya Swiss Leaks iliyotolewa juzi Jumapili, inaonyesha kuwa vigogo hao wa Tanzania wana akaunti za siri zenye Dola za Marekani milioni 114 ambazo ni sawa na Sh. bilioni 199.6.
Msingi wa ripoti hiyo umetokana na aliyekuwa mfanyakazi wa benki ya kimataifa HSBC, Hervé Falciani, kuvujisha siri za akaunti za wateja baada ya kuacha kazi; na mwaka 2008, alivujisha siri za akaunti za siri za baadhi ya watumishi wa umma na wanasiasa kwa Serikali ya Ufaransa ambayo mamlaka za kodi nchini humo ilifanya uchunguzi na kuthibitisha.
Ripoti hiyo ya Swiss Leaks, inaeleza kuwa taarifa za kiuchunguzi kutoka benki ya HSBC nchini Uswisi zinaonyesha kuwa akaunti hizo zinahusishwa na baadhi ya wanasiasa, wafanyabiashara wakubwa na watumishi wa umma ambao wamejipatia utajiri wa siri unaotokana na kampuni hewa (offshore companies).
- Taarifa kwa mujibu wa gazeti la NIPASHE: Mkuya: Siyo kosa Watanzania kuweka fedha Uswisi


Comments
Post a Comment