ORODHA YA WALIOSAMEHEWA KODI TANZANIA: BENKI YAFUTIWA HADI KODI "TOILET PAPER" TRA YAJISAMEHE KODI YA VIBURUDISHO
- Get link
- X
- Other Apps
12 Feb2015
ORODHA ya walipa kodi wakubwa ambao serikali imewasamehe kodi kwa kipindi cha kati ya Januari 2010 hadi Septemba 2014 imewekwa hadharani, huku matumizi mabaya ya misamaha yakionekana. Baadhi ya makampuni na taasisi hizo yamepewa misamaha hadi ya vitu vya kawaida kama karatasi za kutumia chooni, jambo ambalo linazua maswali kuhusu misamaha hiyo.
Wizara ya Fedha imetoa taarifa hiyo kupitia katika tovuti yake, kutokana na maagizo ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuitaka kufanya hivyo, ingawa juzi Jumatatu mtandao ulikuwa umezuiwa kuonyesha taarifa hizo kwa sababu ambazo hazijajulikana.
Zaidi ya makampuni hayo makubwa kwa kulipa kodi, wizara hiyo ilitakiwa pia kuweka hadharani majina ya watu binafsi na taasisi nyingine ambazo zilifaidika na misamaha hiyo katika kipindi hicho. Katika orodha hiyo ambayo Raia Mwema imefanikiwa kuiona, makampuni ya kuchimba madini, ya kutafuta mafuta, mabenki mbalimbali ikiwamo Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Majeshi na Idara mbalimbali za serikali ndiyo walionekana kuwa wanufaikaji wakubwa wa misamaha hiyo. Namba kodi inayosamehewa kwa mujibu wa taarifa ya TRA, kiasi cha shilingi trilioni 1.4 kilisamehewa kulipwa kodi katika mwaka uliopita wa fedha, jambo ambalo lilionekana kuichukiza kamati ya PAC.
Taarifa ya Wizara ya Fedha (MoF) imetoa mwanga wa machache ambayo Raia Mwema imeweza kuyabaini. Katika ukurasa wa arobaini wa taarifa ya wizara, kuna taarifa za benki ya M (Bank M) ya jijini Dar es Salaam kupewa msamaha wa kodi kwa ajili ya manunuzi ya bidhaa za kutumia chooni. Zaidi ya bidhaa hizo za chooni, benki hiyo pia iliomba msamaha wa vitu kama tarazi (tiles) na tranfoma. BoT iliomba na kupewa msamaha wa kodi wa vitu kama note book, sare za wafanyakazi, ukarabati wa redio, manunuzi ya kadi za mwaliko na huduma za mwaliko.
Taarifa ya Wizara ya Fedha (MoF) imetoa mwanga wa machache ambayo Raia Mwema imeweza kuyabaini. Katika ukurasa wa arobaini wa taarifa ya wizara, kuna taarifa za benki ya M (Bank M) ya jijini Dar es Salaam kupewa msamaha wa kodi kwa ajili ya manunuzi ya bidhaa za kutumia chooni. Zaidi ya bidhaa hizo za chooni, benki hiyo pia iliomba msamaha wa vitu kama tarazi (tiles) na tranfoma. BoT iliomba na kupewa msamaha wa kodi wa vitu kama note book, sare za wafanyakazi, ukarabati wa redio, manunuzi ya kadi za mwaliko na huduma za mwaliko.
TRA yenyewe ilijiombea na kujipa msamaha kwa ajili ya viburudisho na chakula ambacho walikula katika mojawapo ya mikutano yao.
Kulikuwa na misamaha mingi pia katika eneo la vinywaji kwa majeshi ambapo soda, bia na vinywaji vikali peke yake viliweza kusamehewa kodi ya zaidi ya shilingi bilioni mbili katika kipindi hicho.
Kampuni isiyofahamika sana ya Aurum Africa imepewa msamaha wa zaidi ya shilingi milioni 220 kwa ajili ya kuuza dhahabu ghafi (raw gold).
Mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu, pamoja na mambo mengine umeonekana pia kuomba msamaha na kupewa wa samani (furnitures) za ofisini pamoja na ununuzi wa mashati na suruali.
Mwaka 2012, Benki ya FBME ambayo kwa sasa iko chini ya usimamizi wa serikali, ilipewa msamaha wa kodi wa kiasi cha shilingi milioni 76 kwa ajili ya ununuzi wa samani za ofisini.
Ingawa baadhi ya misamaha ina thamani ndogo kifedha, lakini Raia Mwema imeamua kuionyesha si kwa sababu ya thamani yake bali kutokana na matumizi mabaya ya fursa hii ya misamaha. Katika orodha hiyo ambayo juzi haikufunguka kwenye mtandao na bado sababu za kuzuiwa kufunguka hazijawekwa hadharani, makampuni yaliyopewa misamaha mikubwa zaidi ni yale yanayojihusisha na uchimbaji madini na gesi.
StatOil pekee kwa mfano, imepata misamaha tofauti yenye thamani ya shilingi bilioni tatu, bilioni 12, bilioni nne na bilioni tano kwa sababu tofauti kutokana na matumizi yake ya vifaa vya kuchimba baharini, ukodishaji wa helikopta na matumizi mengine.
Taasisi ambazo zimetajwa katika taarifa hiyo ya Wizara ya Fedha ni Swissport, Mfuko wa PPF, Kundi la Kampuni za Bakhresa, Shirika la Taifa la Maendeleo ya Petroli, ABG Exploration, Bomba la Mafuta la Tanzania na Zambia (TAZAMA) na Diamond Trust Bank.
Makampuni mengine yaliyotajwa ni Kundi la Kampuni za Namera, Benki ya NMB, Jeshi la Magereza, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wakala wa Ujenzi wa Barabara (Tanroads), Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Dawasco, Dawasa, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Takukuru na Kiwanda cha Nguo cha NIDA, Jeshi la Polisi, Mantra Tanzania, StatOil, Wakala wa Umeme Vijijini (REA), Mradi wa MCC, Petrobas, BG Tanzania, TANESCO, Aurum Africa Limited, African Banking Corporation, AlphaKrust, APM Gold, Bank M, Barrick, BG Tanzania, Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu na Camel Oil.
Wafaidikaji wengine wa misamaha hiyo ya serikali ni China Geo-Engineering, Commercial Bank of Africa (CBA), Stanbic, Resolute, East Coast Oil and Fats Limited, Ecobank Tanzania, Estim Construction, Etablissement Maurel Et Prom na Ets Maurel et Prom.
Wengine ni Benki ya FBME, Highland Estate, HTT Infraco LTD, I&M Bank Ltd, Kagera Sugar, Mfuko wa LAPF, Leopard Tours, Mtibwa Sugar, Mufindi Papers, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Shirika la Taifa ya Nyumba (NHC), Mfuko wa NSSF, Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Oilcom, Ophir East Africa, Pangea Minerals na Precision Air Services.
- Taarifa ya Raia Mwema: Benki yafutiwa kodi toilet paper
- Get link
- X
- Other Apps
Comments
Post a Comment