Daktari aeleza kilichomwua mwigizaji Steven Kanumba

Florence Majani na Suzzy Butondo

MSANII nyota wa filamu nchini, Steven Kanumba amefariki dunia kutokana na tatizo la mtikisiko wa ubongo linalojulikana kitalaamu kama Brain Concussion, taarifa za kitabibu zimeeleza.
Taarifa hizo za ndani, zilizopatikana jana baada ya jopo la madaktari bingwa watano wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kuufanyia uchunguzi mwili wa marehemu huyo, zimeeleza kuwa tatizo hilo linaweza kumfanya mtu apoteze maisha mara moja au baada ya siku kadhaa. Mmoja wa madaktari hao ambaye aliomba jina lake lisitajwe gazetini alisema waligundua tatizo hilo baada ya kumfanyia uchunguzi huo kwa zaidi ya saa mbili.

“Tulianza kuufanyia uchunguzi mwili wa marehemu kuanzia saa 4:00 asubuhi hadi saa 6:45 mchana na tukagundua kuwa marehemu alifariki kutokana na mtikisiko wa ubongo kwa kitaalamu, Brain Concussion,” alisema daktari huyo. Alisema Kanumba alipata mtikisiko wa ubongo ambao husababisha kufeli kwa mfumo wa upumuaji (cardio-respiratory failure) “Kilichomuua hasa ni mtikisiko wa ubongo, ambao endapo unatokea katika sehemu ya nyuma ya ubongo (cerebrum), huua kwa haraka” alisema daktari huyo na kuongeza kuwa mtikisiko wa ubongo  wa nyuma, husababisha matatizo ya mfumo wa upumuaji na hilo limeonekana katika mwili wake.


“Baada ya ubongo wake kutikiswa kwa nguvu, mfumo wa upumuaji ulifeli na ndiyo maana tumekuta kucha za Kanumba zikiwa na rangi ya bluu, huku mapafu yake yakiwa yamevilia damu na kubadilika kuwa kama maini, hizo ndizo dalili za kufeli kwa mfumo wa upumuaji.”


“Mtu aliyepata mtikisiko wa ubongo huweza kutokwa na mapovu mdomoni na hukoroma kabla ya kukata roho na ndivyo ilivyokuwa kwa Kanumba kabla hajafariki.”


Daktari mwingine aliyeshiriki katika uchunguzi huo ambaye pia aliomba jina lake lisitajwe alisema ubongo wa mwigizaji huyo ulikuwa umevimba na kushuka karibu na uti wa mgongo na hivyo kuathiri mfumo wa upumuaji.

Alisema sehemu ya maini na majimaji ya machoni ya marehemu, vimepelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ili kubaini endapo kuna sumu au kitu kingine katika mwili huo.

Baba mzazi azungumza Baba mzazi wa mwigizaji huyo, Charles Musekwa Kanumba alisema kwamba alipata taarifa za kifo cha mwanawe Jumamosi saa 10:00 alfajiri baada ya kupigiwa simu na dada wa marehemu, Sara Kanumba.  “Sara aliniuliza: ‘Una taarifa yoyote kuhusu mwanao Kanumba?’ Nikamjibu kuwa sina taarifa yoyote, ndipo aliponieleza habari za kifo hicho. Aliniambia Kanumba hatupo naye tena amefariki kwa kuanguka, amekorofishana na mpenzi wake.”  alisema taarifa hizo zilimsababisha aishiwe nguvu kwa kuwa kilikuwa kifo cha ghafla… “Basi kuanzia hapo, nilianza kupigiwa simu za kupewa pole, ndipo nilipoamini kumbe mwanangu amefariki.”

 Akizungumzia kuchelewa kufika msibani, alisema kumetokana na tatizo la mawasiliano. Awali, alikuwa amepanga mtoto wake Kanumba akazikiwe Mwanza kwa babu yake ndiyo maana hakufika mapema msibani.   “Nilikuwa nimepanga apitishwe hapa kwangu Shinyanga aagwe, halafu tumpeleke Mwanza kwa babu yake kumzika huko lakini alipokuja mama yake alinishauri kuwa huko kutakuwa na nafasi ndogo kwa sababu watu ni wengi pia alikuwa na marafiki wengi, wengine wa kutoka nje ya nchi kwa hiyo alinishawishi na tukakubaliana kumzika Dar es Salaam,” alisema.

Pia alikanusha uvumi kuwa hajafika msibani kwa kuwa walikuwa na ugomvi na marehemu akisema walishamaliza tofauti zao. Alisema anatarajia kufika leo usiku tayari kushiriki mazishi hayo.

Wabunge  kilio Jana, baadhi ya wabunge waliofika nyumbani kwa marehemu Kanumba waliangua vilio wakati walipotoa salamu zao za rambirambi.
Mbunge wa Viti Maalumu, Martha Mlata hakuzungumza na badala yake aliimba kipande cha wimbo uliozungumzia kifo na maneno ya wimbo huo yalionekana kuwagusa wafiwa na kusababisha vilio kuanza upya huku baadhi wakipoteza fahamu.
Mbunge mwingine, Neema Mwinyimgaya aliongeza majonzi masibani hapo alipounganisha msiba huo na wa mama yake… “Mama yangu amefariki miezi mitatu iliyopita, huko uliko mama, nakuomba umpokee kijana mwenzetu,” alisema mbunge huyo na kushindwa kuendelea.

Wabunge wengine waliohudhuria msiba huo ni Ismail Aden Rage (Tabora Mjini), Aboud Juma (Kibaha Vijijini), Mussa Azan Zungu (Ilala), Abbas Mtemvu (Temeke), Peter Serukamba (Kigoma Mjini) na Ritha Kabati (Viti Maalumu).
 Kova na mchango wa Kanumba Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema anakumbuka mchango wa Kanumba katika kuzuia uhalifu jijini.

“Tulishirikiana naye pamoja na wasanii wengine kuandaa bonanza maalumu ambalo lilidhamiria kukabiliana na uhalifu hapa jijini na kwa kweli mchakato ule ulifanikiwa kwani uhalifu ulipungua kwa kiasi kikubwa” alisema Kova.
“Kifo chake kimekuwa cha ghafla mno na nafikiri kujiweka tayari (kiimani) ni jambo ambalo kila mmoja anatakiwa kuwa makini nalo katika maisha yake,” alisema Kova.

Ratiba ya mazishi
2:30 - Msafara kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili kupitia Barabara ya Umoja wa Mataifa na Ali Hassan Mwinyi hadi Viwanja vya Leaders Club.
3:30 - Misa ya kumuombea na salamu mbalimbali.
6:00 – Kuaga
9:00 - Kuelekea Makaburi ya Kinondoni kupitia Barabara ya Tunisia

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA