HALIMA MDEE NA JOSHUA NASSARI NDANI YA MIPANGO YA NDOA

Ni taarifa iliyoandikwa katika gezeti la HabariLeo na imesomwa kweli kweli huko! Picha zinazofuata hapo ni za mkutano wa CHADEMA kuwashukuru Wananchi kwa kuwapa kura zilizotosha kumpa ushindi Joshua Nassari.


Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) amesema sasa yuko tayari kufunga ndoa na Mbunge mteule wa chama hicho wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari.

“Nafurahi kwamba Nassari hatimaye ameshinda ubunge katika uchaguzi mdogo,” alisema Mdee wakati akihutubia maelfu ya wakazi wa Arusha na Meru juzi katika viwanja vya Leganga kusherehekea ushindi wa chama chake katika uchaguzi huo.

Mdee alifafanua, kwamba yeye na chama chake walikuwa wamebanwa na kampeni za kuhakikisha Chadema inatwaa jimbo la Arumeru Mashariki na ndiyo sababu hakujibu mara moja maombi ya Nassari ya kumwoa aliyoyatoa katika moja ya mikutano yake ya kampeni.

“Naondoka kwenda Dar es Salaam kujiandaa kwa Mkutano ujao wa Bunge, kisha nitakwenda Dodoma ambako nitamsubiri Nassari na kwa pamoja tutafanya maandalizi,” alisema Mdee huku akishangiliwa na hadhira hiyo huku wakiimba na kucheza katikati ya mvua iliyokuwa ikinyesha.

Mdee alisema ndoa kati ya wabunge hao wawili wa Chadema ni wazo zuri na itatangazwa sana na kuandika historia.

Alipoona anashambuliwa sana na wapinzani wake juu ya useja wake katika kampeni hizo, Nassari hatimaye alitangaza kumwoa Mdee ambaye pia hajaolewa.

Na katika moja ya mikutano ya hadhara, alisimama naye jukwaani kukampeni.

“Kuna viongozi wengi wa kidini Dodoma, ikiwa ni pamoja na ndani ya Bunge ambao watatushauri jinsi ya kulitimiza hili,” alisema Mdee na kuongeza kwamba baba yake Joshua, Mchungaji Samuel Nassari alipata kusema, ‘mwanamke mzuri ni zawadi kutoka kwa Mungu’.

Chadema ina idadi kubwa ya wabunge vijana ambao hawajaoa, ikiwa ni pamoja na Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Mr Sugu’; wa Ubungo, John Mnyika; wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe na sasa Nassari. 
Picture
Mbunge mteule wa jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari akiwasili kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Leganga, ambako kulifanyika mkutano wa kuwashukuru wapiga kura wa jimbo hilo
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ametaka wananchi kutoa maoni ya Katiba mpya ili walete mabadiliko mwaka 2015.

Aidha, amewasihi kuacha kutopiga kura, kwa kuwa katika uchaguzi wa Arumeru Mashariki waliojitokeza walikuwa wachache.

Aliwasihi vijana kujitokeza Daftari la Kudumu la Wapiga Kura litakapotolewa kwa ajili ya kuboresha taarifa zao na wengine kujiandikisha upya.

Alisema hayo katika mkutano huo na kumsifu Nassari ambaye alidai ni kijana atakayeleta mabadiliko ndani ya jimbo hilo ingawa baadhi ya watu walihoji umri na mambo mengine. Mbowe alisema chama hicho kitatumia njia ya miguu, magari hata helikopta nchi nzima, kufikia wananchi ili watoe maoni yao juu ya mchakato wa Katiba mpya.

Alitoa rai kwa Polisi kuacha kupiga mabomu, kutumia risasi na nguvu zaidi, nyakati za uchaguzi kwani vijana wanaoumia ndio watakaokuwa viongozi wa baadaye.

"Nawashukuru kwa kunipa kijana mjanja, yaani Nassari namkabidhi Lema (Godbless) ili aje naye mjengoni (bungeni) na sisi wabunge wa Chadema tutampokea na wananchi.

“Lakini nawapasha ninyi vijana, kunapotokea suala la uamuzi wenu kwa ajili ya maendeleo, pigeni kura na natoa rai, tumieni marekebisho ya Daftari mjiandikishe na kulinda kadi zenu, ili tulete maendeleo, kwani ushindi wa Chadema ndiyo safari ya CCM mwaka 2015 na kila wanapotupiga mabomu tunashinda," alidai Mbowe.
Picture
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, akiwashirikisha wananchma na wapenzi wa chama hicho, kuitikia msemo wa ‘Peoples Power’, wakati wa mkutano wa kuwashukuru wapiga kura wa jimbo la Arumeru Mashariki kwa kuwapa ushindi
Mbunge wa Arusha Mjini, Lema alishukuru wananchi hao na kusema watuhumiwa wa rushwa wakae chonjo, kwani baada ya Chadema kushinda Arusha Mjini na Arumeru Mashariki maendeleo yatapatikana.

Aliomba wananchi kuondoa itikadi zao za vyama na kumpa ushirikiano Nassari kwa kuwa yeye ndiye mbunge atakayewaletea maendeleo. Katibu Mkuu Dk. Willibrod Slaa, alisema ushindi huo ni wa kishindo, kwani walimtanguliza Mungu na kutoa angalizo kuwa jimbo la Monduli nalo wanakaribia kulichukua.

Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo alisema yeye si mtu wa ahadi hewa, hivyo atashirikiana na Nassari kuchimba visima viwili na kuongeza kuwa mfadhili wa chama hicho, Mustapha Sabodo, amejitolea kuchimba vinne ili kuondoa kero ya maji jimboni humo. 
Picture
Mbunge wa Moshi Mjini, Ndesamburo akiwashukuru Wananchi wa Arumeru kwa ushindi
Picture
Mbunge wa jimbo la Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi Mr II aka Sugu, akitumbiza wakati wa mkutano wa kuwashukuru wapiga kura wa jimbo la Arumeru Mashariki kwa kumchagua Joshua Nassari kuwa Mbunge wao
Picture
Mbunge wa Arusha Mjini (CHADEMA) Godbless Lema na Wananchi
Credits: 
Habari - Lucy Lyatuu, Dar; Veronica Mheta na Marc Nkwame Arumeru via gazeti la HabariLeo
Picha - Joseph Senga via blogu ya Mroki

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA