SIMBA YAPAA ALGERIA NA MATUMAINI KIBAO
Wawakilishi pekee wa Tanzania katika michuano ya Afrika,
Simba SC wameondoka alfajiri ya leo Dar es Salaam kuelekea Algeria kwa ajili ya
mechi ya marudiano, Raundi ya Pili Kombe la Shirikisho la Soka Afrika dhidi ya
wenyeji ES Setif, wakipitia Algeria.
Simba imeondoka ikisema ina matumaini makubwa ya kuitoa ES
Setif katika mchezo huo utakaofanyika Ijumaa wiki hii.
Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema wachezaji
wapo katika ari nzuri na kwamba wimbo wao ni ushindi. Kamwaga aliwataja
viongozi watakaofuatana na timu hiyo kuwa ni Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail
Aden Rage, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo Damian Manembe na
Kamwaga.
Alisema benchi la ufundi watakaokuwepo ni Kocha Mkuu Milovan
Cirkovic, Kocha Msaidizi Amatre Richard, kocha wa makipa James Kisaka, daktari
wa timu Cosmas Kapinga, Nyagawa na mtunza vifaa Kessy Rajab.
Aliwataja wachezaji waliopo kwenye msafara ni Juma Kaseja,
Ally Mustafa, Nassor Masoud, Shomari Kapombe, Amir Maftaha, Juma Nyoso, Kelvin
Yondani, Victor Costa, Obadia Mungusa, Jonas Mkude, Patrick Mafisango, Mwinyi
Kazimoto, Haruna Moshi, Salum Machaku, Uhuru Suleiman, Felix Sunzu, Emmanuel
Okwi, Edward Christopher, Derick Walulya na Gervais Kago.
Naye Kocha Mkuu, Milovan alisema wamejipanga vilivyo na
kwamba wataufanyia kazi udhaifu uliojitokezakwenye mchezo wa kwanza na kuwaomba
mashabiki wasiwe na wasiwasi na kuwa watarejea na ushindi.
Simba ilishinda mchezo wa kwanza wiki moja iliyopita mabao
2-0, hivyo sare ya aina yoyote au isipofungwa zaidi ya bao 1-0 itakuwa imesonga
mbele.
Comments
Post a Comment