Ofisi Ya Katibu UVCCM Arusha Yafungwa


HALI ya Siasa Mkoa wa arusha hususan kwa Umoja wa Vijana (UVCCM) ni
tete baada ya vijana hao  kuchukua uamuzi wa kufunga ofisi ya umoja
huo pamoja na kubandika mabango usiku wa kumkia leo .

Mabango hayo yalikuwa yakimshinikiza Katibu wa UVCCM Mkoa wa Arusha,
Abdallah Mpokwa kuondoka na kumfuata aliyekuwa Mwenyekiti wa UVCCM
,James Ole Millya ambaye amehamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) na mengine yakimtuhumu Millya kuwa ni fisadi .

Wakizungumza na waandishi wa habari baadhi ya vijana wa umoja huo
mkoani hapa ambao ni Ally Shabani maarufu kwa jina la Majeshi ambaye ni
Katibu wa UVCCM Kata ya Moivo  pamoja na Masoud Rajabu ambaye ni
Katibu wa UVCCM kata ya Lemara walisema wamechukizwa na kauli ya
Mpokwa aliyoitoa janajuu ya kumsafisha Millya kwa madai hana ushahidi
wa hela Sh. milioni 2 iliyotolewa kwa ajili ya  kuanzishwa kwa saccos
hiyo.

Shabani alisema kauli aliyoitoa  juzi Mpokwa kuwa  UVCCM haijawahi
kuwa na mradi wa SACCOS na pia kukanusha suala la Millya kutakiwa
kukabidhi ofisi mara alipoondoka na kujiunga na Chama cha Demokrasia
na Maendeleo(Chadema).

Alisema  kitendo cha Mpokwa kudai kuwa  kisheria Millya  hakuwa na
ofisi ila alikuwana kazi ya kufungua mikutano  hivyo tuhuma hizo
hazimhusu pia  suala la SACCOS halijawahi kuwepo katika kumbukumbu
za ofisi zao na wala hakuna mtu aliyekatiwa risiti wala kuonyesha
mahali popote mtu wa umoja huo kama alipokea.

Alisema kutokana na kujitoa kwake na wengine wanaoendelea kuondoka
katika Umoja huo, Umoja huo haujatetereka na wala hautatetereka na
sasa wanajiandaa na uchaguzi wa ngazi zao zote.

Majeshi alihoji  ni kwanini Mpokwa amtetee Millya kuhusu suala la
fedha na mambo mengine hivyo uamuzi wa vijana kufunga ofisi hiyo ni
sahihi kwani tamko alilolitoa halina mashiko na kama vijana hawamtaki
tena kuongoza umoja huo.

Alisema haiwezekani hela za miradi ya UVCCM ziliwe kama mchwa kwenye
kichuguu hivyo hawamtaki Mpokwa na kusisitiza kuwa amfuate Millya huko
aliko

Mpokwa amekiuka taratibu za UVCCM kwakumuunga mkono Millya hivyo
hawamtaki awaongoze vijana hao  kwani yeye ni mamluki anayetumiwa na
Millya kuhakikisha anaharibu umoja huo .

Naye Rajab aliongeza kuwa wanamhitaji mlezi wa Chama hicho Mkoani
hapa, Steven wassira aje kurekebisha kasoro zilizopo kwa vijana kwani
awali Wassira alifika kutatua makundi yenye mgogoro kwenye vikao na
kupokea taarifa zisizo sahihi hivyo safari hii kama atakuja
awakutanishe vijana wote ili kutatua migogoro mbalimbali ya umoja huo
ikiwemo ulaji wa fedha za miradi mbalimbali ya UVCCM.

Hata hivyo vijana wa umoja huo walionekana wakiwa makundi makundi kila
mmoja akimvizia mwenzie kuona ni nani atavunja ofisi hiyo huku wengine
wakidai mtu akisogea kufungua makufuli hayo waliyoweka  watahakikisha
wanapigana na kusisitiza Mpokwa kuondoka kwani hawamhitaji tena.

Vijana hao walichukua hatua hiyo baada ya Mpokwa kumsafisha Millya kwa
madai kuwa alihama chama kwa matakwa yake na pia hakukuwa na saccos
kama ilivyodaiwa hapo awali .

Na Ashura Mohamed

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA