UPIGAJI KURA TUZO ZA KILI MWISHO APRILI 6
Zoezi la upigaji kura kwa
ajili ya kuwapata washindi wa tuzo za muziki Tanzania kwa mwaka 2012 linatarajia
kufikia kikomo wiki hii huku wito ukitolewa kwa wadau wa Sanaa kuendelea kuwachagua
wasanii wao.
Akizungumza kwenye Jukwaa
la Sanaa wiki hii makao makuu ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Afisa
kutoka Kampuni ya ukaguzi na uhakiki wa mahesabu ya Innovex ambayo ndiyo yenye
jukumu la kuratibu zoezi zima la upigaji kura Edna Masalu alisema kuwa, mchakato
wake unaendelea vema na unatazamia kufika kikomo wiki hii.
“Zoezi la upigaji kura
lililodumu kwa zaidi ya mwezi mmoja na nusu litafikia mwisho wiki hii Aprili 6,
wadau wa muziki wanahamasishwa kuendelea kuwachagua wasanii wenye kazi wanazoona
ni bora katika kipindi hiki ili kuwawezesha kushinda” alisema Edna.
Kuhusu umakini kwenye zoezi
la kupiga kura, Edna alisema kuwa, Kampuni ya Innovex imebuni njia mbalimbali
za upigaji kura ili kuwawezesha wadau wa Sanaa wa kada mbalimbali kuweza kupata
fursa ya kupiga kura na kuwa sehemu ya tuzo hizo zenye umaarufu katika ukanda
wa Afrika Mashariki na Kati.
Alizitaja njia hizo ambazo
zinatumika kupiga kura kuwa ni pamoja na ujumbe mfupi wa simu ya mkononi
kupitia namba maalum, magazeti, vipeperushi na mitandao ya kompyuta ambapo
alisisitiza kwamba, kila mtanzania ana haki ya kupiga kura moja tu kwa kila
eneo (category) inayoshindaniwa.
“Hakuna njia yoyote ya
upendeleo, kura zinapigwa na kuhesabiwa kwa uwazi kupitia mtandao. Toka Academy
imeanza hadi sasa zoezi la upigaji kura kwa watanzania mfumo ni wa wazi na
hakuna mwanya wa upendeleo” alisisitiza.
Awali, akiongea kuhusu tuzo
hizo, Mratibu kutoka BASATA Angelo Luhala alisema kuwa, wasanii na wadau wa
Sanaa wanapaswa kuthamini tunzo hizo kama kitu chao kwani ni kitu kilichobuniwa
na watanzania kwa ajili ya kukuza muziki nchini.
“Malengo ya tuzo hizi ni
kukuza muziki nchini na kuwapa ari wasanii wabuni kazi zenye ubora. Ni wazi
msanii anayepata fursa ya kuwa kwenye moja ya kipengele kinachoshindaniwa ni
heshima kubwa” Alisisitiza Luhala.
Comments
Post a Comment