KATIBU WA CCM AUAWA KWA KUKATWA SHINGO

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi kata ya Mwalugulu wilayani Kahama mkoani Shinyanga Daudi Lusalula anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya 55-56 ameuawa kikatili kwa kwa kuchinjwa shingo na watu wasiofahamika katika eneo la Malenge kata ya Mwaluguru wilayani humo wakati akitokea kwenye mkutano wa Chama cha Mapinduzi uliofanyika wilayani Kahama.

Tukio hilo limetokea jana saa mbili usiku wakati katibu huyo wa CCM kata ambaye pia ni Katibu wa Elimu, Malezi na Mazingira wa Baraza la Wazazi wa CCM wilaya ya Kahama akitokea Kata ya Kagongwa kwenda nyumbani kwake Sungamile baada ya kutoka kwenye mkutano wa chama chake uliokuwa unafanyika mjini Kahama.

Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kahama Mabala Mlolwa ameiambia Malunde1 blog kuwa katibu huyo amechinjwa shingoni na watu wasiofahamika wakati akitoka eneo la Kagongwa akielekea nyumbani kwake.

“Siku ya tukio tulikuwa na mkutano na makatibu kata na madiwani wote wa CCM wilaya ya Kahama,tukijadili mikakati mbalimbali ikiwemo suala la uchaguzi wa serikali za mitaa,tulimaliza kikao saa nane mchana,majira ya saa mbili usiku tukapata taarifa katibu wetu ameuawa kwa kuchinjwa,”
ameongeza Mlolwa.

"Tunaomboleza msiba wa mwenzetu,amechinjwa shingo kama mfugo,inauma sana,tumepoteza mtu muhimu katika chama,wakati wa kikao chetu, mbali na veo vyake hivyo viwili pia wakati wa mkutano wetu alitangazwa kukaimu nafasi ya mwenyekiti wa wazazi wilaya ya Kahama,tunashukuru jeshi la polisi liko eneo la tukio kuchunguza juu ya kifo hiki,"
aliiambia Malunde1 blog.

Katibu wa siasa na uenezi mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Mlimandago alisema CCM inalaani kitendo hicho CCM na kwamba wamepata pigo kubwa kwani alikuwa na mchango mkubwa katika kujenga chama.

Hata hivyo Mlimandago alisema siyo vyema kuhusisha kifo hicho na moja kwa moja na mambo ya kisiasa bali vyombo vya dola viachwe vifanye kazi yake ili kubaini chanzo cha tukio hilo.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga Justus Kamugisha alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa bado wanafanya uchunguzi juu ya tukio hilo na kwamba taarifa kamili watatoa baada ya uchunguzi kukamilika.

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA