SERIKALI ISIPOJIPANGA; ITAPANGWA TU

Rais Jakaya Mrisho Kikwete.
ESCROW imepita lakini kupita kwake kumetofautiana sana na skendo za ufisadi zilizowahi kuikumba serikali yetu. Kama ni mageuzi ya fikra, Escrow imewaacha Watanzania wakipiga hatua kuelekea kujikomboa na unyonge.
Umoja na mwitikio wa pamoja wa wananchi niliouona kwenye skendo hii mbichi, sikuwahi kuuona wakati wa kashfa ya Rada, Meremeta, Epa na Richmond. Hii ni ishara kwamba wananchi wamechoka kuibiwa rasilimali zao.
Kuchoka huku kunaambatana na kupoteza imani na serikali iliyopo madarakani, kwa kuwa ufisadi mwingi uliopata kutokea umewahusisha baadhi ya viongozi wa ngazi za juu serikalini. Uongozi wa nchi umekuwa siyo utumishi wa umma tena bali ni mradi wa utajirisho.
Nasikitika kuona makundi ya wezi na mafisadi yameungana,  na serikali yameiweka mfukoni kiasi cha kutengeneza mfumo wa kulindana kwa kuwa mnyororo huo hauwezi kutenganishwa.
Nasema hivyo kwa sababu, Escrow pekee imenipa ushahidi wa hiki ninachokisema. Serikali madhubuti iliyo nje ya mfumo wa kifisadi isingekuwa rahisi watuhumiwa wa skendo hii ya wizi wa mabilioni ya fedha kuendelea kufikiriwa juu ya hatua za kuchukuliwa dhidi yao.
Kuchelewa huku ndiko kunazaa minong’ono kuwa waziri mkuu kahusika, sababu hakuonesha ukali kwenye suala hili. Wanasema mawaziri wamehusika na hoja ni hiyohiyo ambayo kucheka kwao na nyani wakati taifa linavuna mabua.
Kama hilo halitoshi, ikulu ya rais nayo inahushishwa.  UkiangalAkwa makini kasoro ni hiyohiyo ya upole. Watu wanahoji, iweje rais asilizungumzie suala hili mpaka leo?  Linamfurahisha nini wakati limewakera wananchi anaowaongoza na wangependa kuona hatua kali zinachukuliwa dhidi ya  wahusika?
Kwa dalili hizi, ni wazi serikali imeshindwa kujipanga na inachosubiri ni kupangwa na wenye nchi.
Anayesema naongopa arejee wakati wa vikao vya bunge. Wakati wa mjadala wa Escrow naamini watu wengi watakubaliana nami kuwa wananchi wana hasira na rasilimali zao kuibiwa na wahuni.
Jijini Dar es Salaam foleni za magari zilipungua wakati wa mijadala ya Escrow ambapo maelfu ya wakazi wa jiji hilo waliegesha vyombo vyao vya usafiri na kukimbilia kwenye runinga kuangalia mambo yanavyokwenda bungeni.
Nashukuru hawakutokea watu wa kuiwasha moto petroli ya hasira za wananchi vinginevyo hali isingekuwa hivi. Sura zenye hasira za wananchi ziliashiria kumsubiri mwendawazimu apige kiberiti na nchi itikisike kwa maandamano na ghasia.
Wakati mimi naona hatari hii bado ipo kuna baadhi ya viongozi hawaoni ninachokiogopa huenda ni kwa sababu wamezoea kusema kwamba ‘Huu ni upepo utapita mambo yatatulia na wizi utaendelea kama kawaida’.
Narudia kusema kwamba  serikali hii isipojipanga katika kulinda masilahi ya taifa, kusaidia uchumi kukua, wananchi ambao ndiyo wenye taifa hili wanapanga mipango yao, na mipango hiyo itapangika bila shaka!
Maana huwezi kuwa na hospitali ya taifa isiyokuwa na dawa na vifaa, watu wanakufa halafu ukawa na viongozi wanaobeba viroba vya fedha za wizi kwenda kuzifanyia anasa wao na familia zao!
Haiwezekani taifa likawa katika wakati mgumu kifedha kiasi cha watumishi kutolipwa mishahara yao, kukawa na huduma duni za jamii, elimu ikazorota na wakati huohuo ukawa na viongozi wanagawana mabilioni eti yawasaidie kuoana! Inasikitisha sana!!!
Serikali isipojipanga itapangwa na umma! Hata Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alisema: Watanzania wanataka mabadiliko, wasipoyapata ndani ya CCM, watayatafuta nje ya CCM! Nadhani muda wa wosia huo kutimia umewadia.



Rai yangu, kwa kuwa mageuzi huambatana na gharama wakati mwingine za umwagaji damu, naishauri serikali hii ifikirie mara mbili uongozaji wake na hasa kwenye suala la ufisadi na umaskini wa watu. Nachochea tu!
Chanzo:global publishers

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA