UNAIJUA AINA YA WATU WANAONYONYA NGUVU ZA WENGINE?
Shukurani kwa Imani Ngwangwalu kwa kutushirikisha makala iliyopachikwa hapo chini. Mawasiliano yake yamepachikwa hapo mwishoni.
Inaweza
kuonekana kama ni kitu cha kushangaza lakini huu ndio ukweli wapo watu
wanaonyonya nguvu za watu. Watu hawa wana uwezo wa kumwandama mtu hadi
anakufa bila kujua. Watu hawa hawajafa,wako hai na tunaishi nao, wengine
wakiwa ni watu wetu wa karibu sana, kama wazazi, wapenzi, watoto,
jirani, marafiki au mabosi wetu. Hufanya vipi kunyonya nguvu zetu?
Hutumia njia za aina mbalimbali, ambazo huzaa matunda kweli.
Mtu
anaweza kuuliza, inawezekana vipi mwingine anyonye nguvu zangu na hizo
nguvu ni zipi? Kwa mfano, mimi ninapo kuwa nakukera kila siku,
ninakugusa kihisia. Ninapokugusa kihisia, unaumia kihisia na kimwili.
Baada ya muda Fulani wa kero zangu, nakuwa nimekupa athari kubwa kimwili
na kiakili bila mwenyewe kujua na kama imeshawahi kukutokea umekerwa na
mtu huwa inapelekea hata unapokutana na mtu huyu anayekukera unakuwa
unajisikia vibaya.
Hebu
pia tuchukue mfano wa bosi na mtumishi wake. Kama bosi ni mtu wa
maringo, dharau, kulaumu bila kujali nini kimefanyika, mkandamizaji na
asiyejali kuhusu madhila ya wengine, ni wazi aliye chini yake ataumia
tu, kwanza, kihisia, halafu kimwili. Ataichukia kazi yake na hatimaye
anaweza kufika mahali akaona maisha haya maana aliyoitarajia.
Ni
vigumu kubaini mtu ambaye ni mnyonya nguvu mapema, lakini kwa
kuelekezwa, mtu anaweza kuwa makini na kuwabaini watu wa aina hiyo
popote walipo au watakapokuwa. Nimeamua nikuelekeze au kukutajia sifa za
watu wanaoweza kuwanyonya wengine na kuwaacha wakiwa maganda matupu,
huku wakiwaacha wakiwa wanyonge hawajui ni kipi cha kufanya.
Hizi ndizo sifa za watu wanaoweza kuwanyonya wengine:-
1. Kuna watu ambao tunanaweza kuwaita, “miye maskini.”
Hawa
ni watu ambao muda wote unapokutana nao, wanalalamika tu. Hakuna siku
ambayo utakutana nao ukute wanazungumzia mambo mazuri au wanafurahia
hali. Kila siku wao ni walalamikaji, wanaoamini kwamba, wanaonewa na
kuteswa. Unaweza kukuta ni watu wa kulalamika au kukosoa tu, lakini bila
kutoa pendekezo au kuonesha ni njia zipi zingepaswa kufuatwa au njia
zipi zingetatua tatizo.
Wao
wanaona kwamba, wanaonewa, wananyimwa nafasi, wanatafutwa na kuchukiwa.
Hawa kwa kawaida hawana uwezo wa kusema lao, kusema wanachofikiria au
walichobuni, hapana. Hata kama wanatakiwa kusema kuhusu jambo fulani
maalumu, ambalo halihusiani na kuonewa na mtu, watajikuta wakiingia
kwenye kulaumu au kukosoa kwanza, ndipo waweze kujibu, kama basi
watakuwa na uwezo wa kujibu.
Hawa
ni wanyonya nguvu za wengine. Hawa ni watu wa kuepukwa sana. Kama mtu
wa aina hii anakujia na kutaka mjadili jambo, ambapo anaanza malalamiko
au kukosoa kwake, huna budi kutafuta sababu ya kukataa kuwa karibu naye.
Ni lazima ufanye hivyo, kwani akikuzoea ni lazima atakunyonya nguvu
zako zote.
2. Kuna watu ambao wao ni wakuzaji wa mambo.
Hawa
ni wanyonya nguvu pia ambao wao kitu au jambo dogo hufanywa kubwa hadi
mtu anaweza kuamini kwamba ni jambo kubwa kweli, ingawa awali alijua ni
jambo dogo. Hawa wako maofisini na majumbani. Mtu anaumwa na mafua,
lakini atalalamika, atagumia na kuaga kabisa na kuacha kabisa wosia,
kwamba anakufa.
Yeye
mwenyewe huyu anayefanya visa hivyo anaamini kwamba, kwa kufanya hivyo,
atapata huruma zaidi, ataona watu wanavyohangaika kuonesha wanavyomjali
na kutaka kupima umuhimu wake. Kwa kawaida kukuza kwao mambo kunaweza
hata kusababisha hata wengine wakaugua zaidi au hata kupoteza maisha
kabisa, kutokana na kuongeza chumvi sana kwenye maneno yao.
3. Kuna wale ambao kwa lugha ya mtaani tunawaita wameza kaseti.
Hawa
ni wale ambao wanataka waongee wao tu, wanataka wao ndiyo wasikilizwe
na mwingine anapotaka hata kusema moja hapewi nafasi. Mtu atazungumza
yeye kuanzia mwanzo hadi mwisho, hata kama ni kwa saa tatu mfululizo.
Mwingine anapotaka kuongea, yeye ameshamkatisha na kuzungumza yeye.
Hataki kuona mtu mwigine akizungumza kama yeye yupo. Hata kama ni mgeni
mahali, akishapewa nafasi ya kuzungumza, huzungumza kweli.
Hajali
kama kuna mtu ambaye anataka aseme hisia zake, hapana. Inafika mahali,
kama unamsikiliza unachoka kabisa. Hatajali, hata kama utamwonesha
kutokujali. Kama ni nyumbani au ofisini, hatajali kukupotezea muda wako
kwa vyovyote vile. Kama ni ushauri aliomba kwako, yeye ndiye atakupa
ushauri kwa sababu, hatakupa nafasi ya kuzungumza katika kumshauri. Hawa
ni wanyonya nguvu ambao tunao kila siku.
4. Kuna wanyonya nguvu ambao kazi yao ni kuwafanya wengine washitakiwe na dhamira.
Kila
wakati linapotoea jambo , juhudi yao kubwa ipo kwenye kutafuta njia ya
kulaumu ili wengine washitakiwe na dhamira. Wakati mwingine jambo liko
wazi kabisa kwamba, hao anaowalaumu hawahusiki, lakini ni lazima
atalaumu tu. Hata kama atafafanuliwa na kuona kwamba, anaowalaumu hawana
tatizo, bado atasema, ‘hata kama hamtaki anahusika kidogo’Wanyonya nguvu hawa wanatafuta kasoro ili walaumu, ili mtu mwingine ajisikie kukosa, ashitakiwe na dhamira.
Anaweza
kuangalia mtu anavyofanya kazi Fulani na kuona ni nzuri sana. Lakini
atajaribu kwa kadiri awezavyo kumkosoa mtu huyo kwa kitu ambacho wala
wakati mwingine hakihusiani moja kwa moja na kazi ile. Anaweza kusema ‘ile kazi ya mwaka jana angefanya hivi tusingekosa tenda’
lengo ni kumfanya mtu ashitakiwe na dhamira. Hataki kusifia hii kazi
nzuri ya sasa, anataka kukosoa ya zamani ambayo iliharibika.Dawa ya hawa
ni kuwapuuzia.
5. Kuna wanyonya nguvu wengine ambao ni wale wasioisha kuwa na matatizo yanayohitaji ushauri.
Asubuhi
atakuja kukuomba ushauri unaohusu jambo Fulani, mchana atakuja na jioni
atakutafuta. Wakati mwingine ushauri anaoomba ni wa kawaida tu. Ni
vizuri kumwonesha kwamba, unajali anachosema, lakini ni vema kila wakati
kumwonesha kwamba, huna jibu, siyo huna nia ya kumsaidia kwenye tatizo
lake. Ajue kwamba, huna jibu kwa sababu hujui. Ukikosa njia au jibu mara
kadhaa, atakata tamaa na kukuacha. Usimwoneshe jeuri au dharau ama
kisirani.
6. Kuna wanyonya nguvu ambao kazi yao ni kuudhi kwa maneno ya kushushua na kushushua.
Badala ya kunyamaza, akikuona na nguo ya aina Fulani, atakwambia, ‘bwana mzee huwezi kuvaa nguo za mtumba kwa hadhi yako vipi’ Ni
wakati ambao kila mkikutana , watatafuta namna ya kukera kihisia zako
na kujaribu kukushushua. Anaweza mtu kusema ‘ mbona afya yako inazidi
kuwa mbaya’ bila hata sababu ya msingi. Ni watu ambao muda wote wanataka
kuumiza hisia za mwingine.
Bila
shaka umeshawahi kukutana na mmoja kati ya wanyonya nguvu hawa.
Jitahidi wakati wote kuwa makini wasije wakafanikiwa kukuweka chini ya
himaya zao. Jitahidi kuwabaini na kujua namna ya kuwaondolea mbali
kwenye maisha yako.
Nakutakia mafanikio mema, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa kujifunza zaidi na kuhamasika.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI NGWANGWALU, 0713 048 0345/dirayamafanikio@gmail.com
Blog: dirayamafanikio.blogspot.com
Comments
Post a Comment