HATI YA SHAMBA LA MWEKEZAJI YAFUTWA, RAIS KIKWETE AAGIZA LIGAWANYWE KWA WANANCHI



Rais Jakaya Kikwete amefuta hati ya shamba la Kampuni ya Galapo Ufyomi Estate lenye ukubwa wa Heka 1,220 lililoko Kata ya Galapo, wilayani Babati mkoani Manyara na kuagiza ligawanywe kwa wananchi.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alisema hayo juzi wilayani Babati, alipokuwa akizungumza na wananchi na viongozi waliokuwa wakimwelezea kero mbalimbali za migogoro ya ardhi.

Lukuvi alisema Rais Kikwete amefuta hati za shamba hilo na kuagiza ligawiwe kwa wananchi wa vijiji vya Gidejabung, Gedamara na Ayamango, ambao walikuwa na uhaba wa ardhi.

“Baada ya Rais kufuta hati ya shamba hilo, sasa viongozi wa mkoa na wilaya hakikisheni mtu ambaye anahodhi eneo kubwa bila kuliendeleza, anang’anywa na kupatiwa wananchi, mtakaposhindwa tuleteeni juu,” 
alisema Lukuvi.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Mhandisi Omari Chambo alisema Serikali imetoa kusudio la kufutwa kwa miliki za mashamba matatu ya Kampuni ya Hamir Estate yaliyoko Bonde la Kiru. Alisema mashamba hayo ndiyo yaliyosababisha kuwapo kwa vurugu.

“Mashamba hayo ni ya Endanahai Estate (Kiru Valey), lenye ukubwa wa heka 2,930, Kiru Plantation lenye ukubwa wa heka 1,536 na shamba la Unit 18 lenye ukubwa wa heka 2,390. Mashamba haya yatagawiwa kwa wananchi,” 
alisema Chambo.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Joel Bendera alimuahidi Waziri Lukuvi kuwa ifikapo Mei, migogoro yote ya ardhi itakuwa imetatuliwa.

“Hatuwezi kuwa na migogoro isiyo na kichwa halafu tunasubiri Rais aje aitatue wakati wenyewe tunaweza kuimaliza,”
 alisema Bendera.

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA