UKIJIFOSI KUMPENDA KISA MALI, PESA ZAKE, IMEKULA KWAKO


Kwa nini mapenzi yameharibu baadhi ya maisha ya watu? Huwa najiuliza maswali mengi yenye kwa nini, yakihusisha mapenzi. Kwa ujumla kama nilivyo na maswali mengi, majibu pia yamekuwa mengi.
Kwa vyovyote itakavyokuwa mapenzi ni sehemu ya maisha yetu na kwa hakika maisha yetu hayawezi kukamilika bila kuwepo mapenzi. Ninapozungumza juu ya mapenzi namaanisha yale yanayotoka moyoni mwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine.

Mapenzi hayo, hukamilika baada ya wawili hao kuwa na hisia sawa za mapenzi. Amini kama upo katika uhusiano na mpenzi ambaye hakupendi, yaani wewe peke yako ndiyo unayempenda, wewe ni mtumwa wa mapenzi!
Kama ndivyo, kwa nini uwe mtumwa? Unadhani hakuna mwingine ambaye anaweza kukupenda kwa mapenzi ya dhati na penzi hilo likawa kwa pande zote mbili tofauti na ilivyo sasa? Inawezekana, huna sababu ya kulazimisha penzi kwa mtu ambaye hakupendi!
Mapenzi ni nguzo ya maisha yetu, kama ukifanikiwa kumpata mpenzi ambaye atakupenda na wewe ukampenda ni wazi kuwa maisha yako yatakuwa yenye furaha na hakika utafurahia maisha yako na huyo ‘mtu’ wako!
 Mapenzi yapo hivyo na kama ukijaribu kuyabadilisha utaumia mwenyewe! Wakati mwingine unaweza ukapendwa na mpenzi ambaye hujampenda, unadhani kuna ulazima wa wewe kulazimisha kumpenda? 
Moyo wako umeshazungumza na wewe, umekuweka wazi kuwa hauna mapenzi ya dhati kwa mtu huyo, kwa nini ujilazimishe?
Tatizo hili mara nyingi huwa kwa wanawake zaidi!
Anatokea mwanaume anampenda sana, anapomtongoza anajikuta hampendi, anachokifanya ni kumwambia atamjibu baadaye! Lengo la kumwambia hivyo ni kwa ajili ya kujipanga na kufikiria! Mapenzi hayafikiriwi!
Kama mtu unampenda, unapomuona tu siku ya kwanza, moyo wako hutetemeka juu yake na utatamani uambiwe kitu fulani na huyo aliyeuteka moyo wako ghafla.

Hii inamaana kuwa atakapokuambia kuwa anakupenda, huwezi kusubiri zaidi, hutakuwa na kitu cha kusubiri, ni nafasi uliyokuwa ukiisubiria kwa hamu sana, na lazima utamkaribisha!
Hata hivyo, baadhi ya wasichana wakitongozwa na mwanaume ambaye anaona wazi kuwa hampendi, lakini akawa na mali au uwezo mkubwa kifedha, huamua kumkubali kwa lengo la kupata vitu vya mwanaume huyo. 
Hufanya hivyo akijidanganya kuwa atajifunza kupenda akiwa ndani ya uhusiano na mwanaume huyo.
Katika mazingira haya yapo matatizo yanayoweza kuibuka lakini kubwa ni lile la kutokutosheka na mpenzi wako uliyenaye. Anaweza akakupa kila kitu lakini ukakosa penzi la dhati ambalo ndiyo msingi wa maisha.
Hatari zaidi ni pale utakapojikuta unaingia katika uhusiano na mwanaume mwingine kwa ajili ya kusaka penzi la dhati! Unajua kitakachotokea? Kama hutaleta magonjwa ndani basi siku moja utafumaniwa, siku lazima utafukuzwa nyumbani kwa mwanaume huyo, kama ana hasira anaweza kukuua.

Ushauri wangu, usijaribu kuingia katika mkumbo huu, mkumbo wa kujifunza kupenda, ni jambo gumu ambalo huweza kuharibu maisha yako kabisa. Jambo ambalo linaweza kukusababisha ukajuta kuzaliwa.
Kuwa makini, maamuzi yahusuyo mapenzi ni lazima yafanywe kwa umakini wa hali ya juu sana. Unapofanya uamuzi juu ya mapenzi, unakuwa unapanga mustakabali wa maisha yako.

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA