MFUMO WA KUKOKOTOA ADA ZA VYUO VIKUU KUKAMILIKA MWEZI APRILI


Serikali inaandaa Mfumo (software) wa kukokotolea ada zinazotumika katika Vyuo Vikuu vyote nchini kutokana na tofauti za kiasi cha ada kinachotozwa na Vyuo Vikuu nchini, Mfumo huu unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Aprili, 2015.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mhe. Anne Kilango wakati akijibu swali la msingi la Mhe. Amina Makilagi, Mbunge wa Viti Maalum aliyetaka kujua iwapo mchanganuo wa ada za vyuo vya umma unaendana na hali halisi za Watanzania wa kipato cha chini.

“Serikali ilifanya utafiti wa kina kwa kushirikisha wadau mbalimbali ili kuweza kupanga Ada Elekezi kwa program zote zinazofundishwa katika Vyuo Vikuu Vyote na kwasasa Serikali inaandaa Mfumo wa kukokotolea ada zitakazotumika katika Vyuo Vikuu Vyote” alisema Mhe. Kilango

Ada katika Vyuo Vikuu vya Umma, ikiwa ni pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es salaam na Chuo Kikuu cha Dodoma zinatofautiana kati ya chuo na program ambayo mwanafunzi anasomea

Mhe. Kilango alitoa mifano ya tofauti za ada katika Vyuo vya Umma, katika program za Uhandisi, Chuo Kikuu cha Dar es salaam kinatoza shilingi 1,3000,000 wakati Chuo Kikuu cha Dodoma kinatoza shilingi 1,500,000 kwa program hiyo kwa mwaka.

Aidha katika program za Sayansi na Ualimu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinatoza shilingi 1,300,000 wakati Chuo Kikuu cha Dodoma kinatoza shilingi 1,200,000. Katika Programu za Ualimu wa Sanaa, Chuo Kikuu cha Dar es salaam kinatoza shilingi 1,000,000 wakati Chuo Kikuu cha Dodoma kinatoza shilingi 800,000.

Kwasasa Tanzania ina jumla ya Vyo Vikuu 53 na Taasisi 21 zinazotoa Shahada. Sera ya Elimu ya Juu ya Mwaka 1999 Kifungu 6.4.3 kilikuwa kinaruhusu Taasisi za Elimu ya Juu kupanga na kusimamia vyanzo vya mapato ikiwa ni pamoja na kutoza ada za masomo.

  • Taarifa ya Johary Kachwamba, via Blogu ya Serikali, DODOMA 

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA