WALIMU WAJIONDOA CWT NA KUUNDA CHAKAMWATA


CHAMA kipya cha Kutetea Haki na Maslahi ya Walimu Tanzania (CHAKAMWATA) kimesajiliwa rasmi na kupata cheti cha usajili wa kudumu kutoka Wizara ya Kazi na Ajira.

Akizungumza na FikraPevu, Katibu Mkuu wa Chakamwata, Mwalimu Meshack Kapange, anasema chama hicho kipya kinaundwa na walimu nchini waliojiondoa kutoka mikononi mwa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT). Kapange amesema mchakato wake wa kukisajili chama hicho ulianza miaka minne iliyopita, hadi hivi juzi kilipopewa usajili wa kuendelea na shuhuli zake kisheria.

“Ni furaha iliyoje kupata usajili huu wa chama chetu cha kutetea haki na maslahi ya walimu? Huu ni ukombozi kwa walimu wanaokatwa asilimia mbili za mishahara yao bila kurejeshewa wanapostaafu,” anasema Katibu Mkuu huyo.

Kuundwa kwa chama kipya hicho kumetajwa na wachambuzi wa mambo kwamba kunaweza kuipasua CWT na pia kutahitimisha ukiritimba wa muda mrefu mrefu wa chama hicho. Aidha, chama hicho kitatoa fursa sasa kwa walimu nchini kuwa na hiyari ya kujiunga na chama ambacho wataona kina maslahi kwao badala ya ilivyo sasa ambapo walimu walikuwa hawana chaguo zaidi ya kujiunga na CWT.

Kwa mujibu wa Mwalimu Kapange, Makao Makuu ya sasa ya chama hicho yatakuwa Jijini Mbeya. Anasema walimu watakaohitaji kujiunga na chama hicho kipya, watafanya hivyo kwa hiari yao kama sheria za kazi zinavyoelekeza tofauti na CWT ambayo kila mwalimu anayepata ajira serikalini alikuwa analazimishwa kujiunga na kuanza kukatwa fedha zake kutoka kwenye mshahara wake bila ridhaa yake na kinyume cha sheria za ajira.

“Kila mwanachama atachangia asilimia moja tu ya mshahara wake kwa kila mwezi badala ya asilimia mbili kama ilivyo kwa CWT. Wakati mwanachama anapostaafu, atapewa ‘bonus’ kama asante kwa kuchangia Chama,” anasema Mwalimu Kapange.

Mbali na hilo, Kapange anasema Chakamwata kitafanya jitihada za kuwajengea wanachama wake uwezo wa kutambua wajibu wao, haki zao na jinsi ya kuzidai, badala ya kutambua wajibu pekee kama ilivyo ndani ya CWT, kwa maelezo kwamba hakuna wajibu kwa mtumishi yeyote wa umma usiokwenda sambamba na haki yake.

“Tulipokuwa tukiomba usajili kwa mara ya kwanza Mei, 2012, tulikuwa wanachama 400 ingawa masharti ya kisheria ya kuanzisha vyama kama hivi yanataka wanachama 20 tu. Nashukuru kwamba hadi tunapata usajili huu, wanachama wetu wanafikia 9,743, wengi wao wakitokea mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe, Rukwa, Ruvuma, Arusha, Mara, Morogoro, Singida na Kagera,” amesema.

Chama kipya hicho, kabla hakijasajiliwa, kilikuwa kikijulikana kwa jina la Umoja wa Maofisa Elimu Tanzania (UMET). Hata hivyo, uongozi wa muda wa chama hicho ulikaa tena na kukipa chama hicho jina la Chakamwata. Chama hicho kimepewa usajili kwa namba 031, huku cheti chake kikiwa kimesainiwa na Msajili wa Vyama Huru vya Wafanyakazi na Waajiri nchini, Doroth Uiso.

FikraPevu inaendelea kumtafuta Rais wa CWT, Gratian Mukoba, pamoja na maoni ya walimu mbalimbali nchini, ili pamoja na mambo mengine, waweze kuelezea ujio wa chama kipya hicho cha walimu nchini na athari zake katika mstakabali wa mshikamano na utengamano wa walimu nchini katika siku za usoni.

  • via FikraPevu

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA