MASTAA NA SIASA NDO KWANZA MAMBO YAMEIVA

ILIKUWA kama kitu cha ajabu baada ya mastaa wa fani mbalimbali nchini hasa wa muziki na filamu, kutangaza nia zao za kujiingiza kwenye masuala ya siasa ambapo mpaka sasa mastaa kama Profesa Jay na Afande Sele wameweka wazi nia zao huku mastaa kama Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ ambaye ni Mbunge wa Mbeya Mjini na Vicky Kamata ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum wakiwa ni baadhi ya mastaa waliotinga bungeni tangu uchaguzi uliopita.
Mbunge wa Mbeya Mjini Joseph Mbilinyi ‘Sugu’.
Bongo siyo nchi pekee ambayo suala hilo limejitokeza, bali hata kwenye nchi mbalimbali za Afrika, Ulaya na Marekani limewahi kutokea ambapo kwa nyakati tofauti mastaa wakubwa wamewahi kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali huku wengine wakishindwa na wengine kushinda nafasi za kuwakilisha wananchi katika nyadhifa mbalimbali. Wafuatao ni baadhi ya mastaa wakubwa wa majuu ambao wamewahi au wanaendelea kushiriki kwenye siasa:-
ARNOLD SCHWARZENNEGGER.
ARNOLD SCHWARZENNEGGER
Huyu ni staa mkubwa wa filamu za ‘action’ nchini Marekani ambaye anajulikana sana kwa umbo lake kubwa. Jamaa alianza kama mtunisha misuli na kuingia kwenye tasnia ya filamu ambapo alifanya vema na muvi zake kama Terminator na Predator. Arnold alianza siasa mwaka 2003 ambapo aligombea ugavana wa Jimbo la Calfornia na kushinda, alishikilia nafasi hiyo hadi mwaka 2011.ANDRIY CHEVSHENKO.
ANDRIY CHEVSHENKO
Ni msakata kabumbu raia wa Ukraine ambaye alipata mafanikio makubwa katika historia ya soka duniani ambapo alichezea klabu kubwa duniani kama AC Milan na Chelsea. Alitangaza kustaafu mwaka 2012 baada ya kucheza soka kwa muda mrefu. Baada ya kustaafu alijiunga na Chama Cha Demokrasia cha Ukraine akigombea nafasi ya ubunge, hata hivyo alishindwa kupata nafasi hiyo kutokana na ushindani mkubwa uliojitokeza.
WYCLEF JEAN
WYCLEF JEAN
Ni staa wa muziki toka Marekani aliyehamia nchini humo akiwa na familia yake kama wakimbizi waliotokea nchini Haiti. Jamaa aliwika na ngoma zake kama 911, Two Wrongs na Hips Don’t Lie aliyoshirikiana na Shakira. Jamaa alijitosa kwenye siasa mwaka 2010 akitangaza kugombea nafasi ya urais katika nchi yake ya kuzaliwa ya Haiti ambapo hata hivyo alitolewa kwenye kinyang’anyiro hicho kutokana na sababu za makazi yaani kuishi Marekani zaidi kuliko Haiti.
YOUSSOU N’DOUR.
YOUSSOU N’DOUR
Huyu ni staa mkubwa zaidi Afrika ambaye anatajwa kushika namba moja kwenye orodha ya wasanii wa muziki matajiri Afrika huku Jarida la Rollingstone likimtaja kama mwanamuziki anayejulikana sana Afrika. 
Mwanamuziki huyu anayejulikana Afrika na duniani kwa kibao chake cha Dirima, alitangaza nia ya kugombea urais mwaka 2012 lakini akatolewa kwenye kinyang’anyiro hicho kutokana na saini za wadhamini wake kuwa na kasoro na pia kutokana na ushawishi wake aliteuliwa kuwa Waziri wa Utalii na Utamaduni ambapo anaendelea na nafasi hiyo hadi hivi sasa.MANNY PACQUIAO.
MANNY PACQUIAO
Jina lake kamili ni Emmanuel Dapridran Pacquiao ni mkali wa ndondi tokea Ufilipino mwenye heshima na mafanikio makubwa duniani kwa ujumla. Pamoja na mafanikio yake alitangaza kujiingiza kwenye siasa mwaka 2007 lakini alishindwa kiti cha baraza la uwakilishi katika Jimbo la Manila na mwaka 2009 aliamua kugombea tena kupitia Jimbo la Sarangani ambapo alishinda kwa kishindo kikubwa bila pingamizi chochote ambapo pamoja na masuala ya ngumi anaendelea kushika nafasi hiyo hadi hivi sasa.

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA