Jeshi la Polisi lazungumzia taarifa za utekaji nyara watoto

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limekanusha vikali uvumi unaoendelea kuzushwa jijini Dar es Salaam kuhusu utekeaji nyara wa watoto wadogo wanaosoma shule za jiji hilo na kuwataka wananchi kuupuuza.

Akizungmza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema kuwa mpaka sasa jeshi hilo halina taarifa yoyote ya mtoto kutekwa au kufanyiwa madhara yoyote kwa mtindo wa utekaji nyara.


“Jeshi la Polisi limegundua kwamba huu ni uvumi ambao haujulikani chanzo chake hivyo wananchi wanaombwa kuachana nao na kuupuza kwani unaleta hofu katika jamii bila sababu za msingi” alisema Kova.


Alisema kuwa pia uvumi huo umeanza kuleta usumbufu ambapo mnamo Oktoba 3 mwaka huu saa 3:00 asubuhi huko Vingunguti, mtu mmoja aitwaye

Prosper Makame (34) akiwa na mkewe Marystella Munis (30) walipata usumbufu unaotokana na uvumi huo.

Kamishna Kova aliongeza kuwa watu hao ambao ni wafanyabiashara wa vyombo vya nyumbani walifika maeneo ya shule ya msingi Kombo iliyopo Vingunguti kwa ajili ya biashara zao, wakiwa na gari aina ya Noah yenye namba T252 DAY, ghafla walizingirwa na watu wakidaiwa wanateka wanafunzi.


“Pia mnamo Oktoba 13, 2014 majira ya saa 4:00 asubuhi huko katika kituo cha Polisi Tabata uliibuka uvumi kuwa gari namba T548 BUN aina ya Noah rangi nyeusi ambayo ni mali ya askari polisi A/INSP Ester wa kikosi cha usalama barabarani, ilivumishwa kwamba ndani ya gari hiyo kuna vichwa vitano vya watoto wa shule ya msingi Mtambani na kusababisha wazazi wenye watoto wanaosoma shule hiyo kukusanyika kituoni hapo ili kushuhudia na kuona vichwa hivyo” alisema Kamishna Kova na kuongeza: “Na ndipo Mkuu wa kituo hicho cha Polisi aliamuru gari hilo lifunguliwe na kuwathibitishia wananchi kuwa habari hizo ni za uongo na uvumi”


Kutokana na tukio hilo jeshi hilo lilifanya uchunguzi na kumkamata mtu mmoja Gilbert Stanley (32) mhehe mkulima na mkazi wa Tabata alipohojiwa alikiri kueneza habari hizo na kudai yeye aliambiwa na mtu ambaye hakumkumbuka.


Hivyo, Kamishna Kova alisisitiza kuwa uvumi wa kuwepo kwa kikundi cha wahalifu wanaowateka watoto wanafunzi si wa kweli hata kidogo na hivyo wananchi wanatakiwa kuepukana na taarifa hizo kwani zinaweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA