Uboreshaji wa Daftari la Wapiga Kura kuanza katikati mwa Mwezi Novemba
Na Magreth Kinabo,Maelezo
Tume ya
Taifa ya Uchaguzi(NEC) imesema kwamba zoezi la majaribio ya Uboreshaji
wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura linatarajia kuanza rasmi katikati
mwa mwezi Novemba mwaka huu.
Aidha NEC
imefafanu kwamba zoezi hilo, litafanyika kwa kutumia mfumo mpya wa
'Biometric Voter Registration'(BVR) katika majimbo matatu ya uchaguzi
ambayo ni Kawe katika Manispaa ya Kinondoni, Kilombero, Halimashauri ya
Mji wa Kilombero na Mlele, Halimashauri ya Mlele, ambapo vituo vya
uandikishaji vimewekwa katika kata zilizomo katika majimbo husika.(Martha Magessa)
Hayo
yalisemwa na Makamu Mwenyekiti wa NEC pia na Jaji Mkuu Mstaafu wa
Zanzibar Mhe. Hamid Mahamoud Hamid,wakati akisoma taarifa kuhusu kuanza
kwa shughuli za Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika
mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo jijini Dares Salaam.
"Tume
tayari imekwishapokea baadhi ya vifaa muhimu vya uandikishaji zikiwemo
fomu za unadikishaji, hivyo kinachosubiriwa ni kupokea BVR kits 250
zinazotarajiwa kupokelewa wakati wowote kuanzia leo. Zoezi la
Uandikishaji litakapoanza, vituo vitafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi
na kufungwa saa 12:00 jioni, vyama vya siasa vinaruhusiwa kuweka
mawakala wao katika kituo ili kushuhudia jinsi uandikishaji utakavyokuwa
unafanyika," alisema Hamid.
Makamu Mwenyekiti huyo alisema baada ya zoezi hilo kukamilika zoezi hilo litaanza katika maeneo mengine.
"
Tunatarajia Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utafanyika
kwa wakati mmoja katika mikoa yote nchini isipokuwa mkoa wa Dares Salaam
na Zanzibar.Uandikishaji katika mikao ya Dares Salaam na Zanzibar
utafanyika baada ya uandikishaji katika mikoa yote utakapokamilika.Muda
wa uandikishaji utakuwa ni siku saba katika kila kituo," alisema.
Aliongeza
kwamba uandikishaji katika mikoa yote umepangwa kufanyika kuanzia
mwanzoni mwa mwezi Januari, mwaka huu hadi katikati ya Februari mwaka
huu, wakati katika mikoa ya Dares Salaam na Zanzibar utafanyika mwishoni
mwa mwezi Februari mwaka huu.
Alisema
uandikishaji katika mikoa yote utafanyika katika awamu nne kwenye kila
halimashauri ili kutoa fursa ya kuhamisha vifaa vya uandikishaji kutoka
eneo moja kwenda eneo lingine.
"Uboreshaji
wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utahusisha wapiga kura wote wapya
na wa zamani. Wapiga kura wa zamani yaani wale ambao walikuwa
wamejiandikisha katika Daftari la Zamani, watatakiwa kwenda katika vituo
vya kujiandikisha vilivyoko karibu na maeneo wanayoishi ili kuchukuliwa
taarifa zao hasa alama za vidole, picha na saini zao kuiongizwa katika
mfumo Biometric Voter Registration na hatimaye watapewa vitambulisho
vipya." Alisisitiza.
Alisema
wapiga kura ambao watakuwa na kadi zao za kupiga kura za zamani
watatakiwa kwenda na kadi zao katika kituo cha kujiandikisha ili
kurahisisha zoezi la kuhamisha taarifa zao za awali katika mfumo mpya wa
BVR.
Aidha
alifafanua kwamba kwa wapiga kura waliopoteza kadi au wale ambao kadi
zao zimeharibika watatakiwa kwenta kituoni ili kujiandikisha na kupewa
kadi mpya.
Hamid
alisema kwa wapiga kura wenye vitambulisho vya taifa Dares Salaam na
Zanzibar watakuja na kadi zao ambazo ni taarifa zao zitasomwa na vifaa
maalum ili kupunguza muda utakaotumika katika zoezi hilo, pia watapewa
kadi mpya ya mpiga kura.
Alisema
kwa wapiga kura wanaoishi na ulemavu na wale ambao hawajui kusoma na
kuandika wanaruhusiwa kwenda kituoni na mtu mmoja katika familia
wanayemuamini ili kusaidia katika uandikishaji.
"Uboreshaji
huu unahusisha pia kuandikisha wapiga kura wote waliotimiza umri wa
miaka 18 au zaidi na wale ambao ifikapo siku ya upigaji kura ya maoni na
uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 watakuwa wametimiza umri wa miaka 18. Pia
wale wote ambao kwa sababu mbalimbali hawakuwahi kujiandikisha katika
Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika mazoezi yote uandikishaji
yaliyopita," alisisitiza.
Hivyo jumla ya watu wenye umri wa miaka 18 na zaidi wapatao milioni 23.09 wanatarajiwa kujiandikisha.
Hamid
aliongeza kwamba mpiga kura atakayejiandikisha katika daftari hilo la
sasa pekee na kupewa kadi ndiye atakayeruhusiwa kupiga kura.
"Wakati
wa uandikishaji, kipaumbele kitatolewa kwa watu wanaoishi na ulemavu,
wazee, wagonjwa wakinamama wajawazito na wenye watoto wachanga. Hivyo
hawatalazimika kusimama kwenye mstari.
Naye
Mkurugenzi wa Uchaguzi kutoka NEC, Julias Malaba alisema tayari kiasi
cha fedha cha Sh. bilioni 15 zimeshatolewa kwa ajili ya zoezi hilo.Huku
Makamu Mwenyekiti wa NEC akisema bajeti halisi litafafanuliwa baadae.
Kwa
upande wake, Sisti Cariah ambaye ni Mkuu wa Daftari la Kudumu la Wapiga
Kura na Naibu Katibu NEC, alisema daftari hilo litakamilika Aprili
14,mwaka huu na litawekwa wazi kwa muda wa siku tano katika maeneo
husika ili kumwezesha kila mtu aliyejiandikisha aende kukagua na
kujiridhisha kwa taarifa zake zimeandikwa kwa usahihi.
Tume hiyo
inatoa wito kwa wananchi wote wenye sifa za kujiandikisha kujitokeza
kwa wingi katika vituo vyote vya uandikishaji kwa ajili ya kujiandikisha
katika daftari hilo.
Akizungumzia kuhusu mfumo wa BVR alisema unasaidia kupunguza ujiandikisha mara mbili na kuwa na taarifa sahihi.
Comments
Post a Comment