MAONI YA MWALIMU MABALA KUHUSU LUGHA NA MFUMO WA ELIMU



Ni dhahiri kwamba mabadiliko ya lugha peke yake hayatafufua mfumo wa elimu. Iwapo mtu ana kisukari, shinikizo la damu na UKIMWI, kupunguza sukari peke yake haitatosha.

Pili kwangu mimi ni dhahiri kwamba watu wanashindwa kutofautisha kati ya umuhimu wa Kiingereza kama lugha kwa wanafunzi wetu na umuhimu wa Kiingereza kama lugha ya kufundishia. Nadhani hakuna anayebisha juu ya umuhimu wa Watanzania kujua Kiingereza. Lakini wengi tunabisha sana kwamba njia bora ya kufanya watu waelewe Kiingereza ni kukitumia kama lugha ya kufundishia. Mimi nimefundisha shule za sekondari na ninajua kwamba

a) Wako wanafunzi wanaokataa mapema sana Kidato cha Kwanza kwa sababu hawaelewi kitu.

b) Wapo wachache ambao waliweza kupambana vikali na lugha hadi waliweza kuwashinda waliotoka kwenye English Medium Schools. Lakini hawa ni wachache.

c) Mimi kama mwalimu wa masomo mengine kama historia au fizikia nakereka sana kupata shida kufundisha somo langu na kueleweka kwa sababu ya kutumia lugha ambayo wanafunzi hawaielewi.

Kupigania wanafunzi wasome kwa lugha wanaoielewa haina maana kwamba tunafikiri wote watafaulu lakini inatoa nafasi ya akili ya mtu kufanya kazi zaidi. Narudia utafiti tuliofanya TAMASHA (ambayo inafanana na ile waliofanya Uwezo na watu wengine). Katika shule 16 za sekondari katika wilaya nane tofauti tulitoa kipande cha kiingereza cha darasa la pili na kuuliza maswali. Ni 25% tu walioweza kusoma kipande kile na kujibu maswali bila wasiwasi. Katika wilaya moja hakuna aliyeweza kujibu. Si Kidato cha Pili, ni darasa la pili. Sasa tungetoa ya darasa la nne sijui katika hawa 25% wangapi wangeanguka.

Vinginevyo tulitoa kipande cha Kiswahili cha darasa la pili ambalo lilikuwa more complex kuliko kile cha Kiingereza lakini 75% waliweza kujibu bila wasiwasi. Ni dhahiri kwamba 25% walishindwa hatukatai lakini inaonyesha kwamba uwezo wa uelewa ulikuwa mkubwa zaidi mara dufu.

Mimi pia sikatai kwamba kuanzia darasa la nne nilimpeleka mwanangu kwenye English Medium School lakini haikuwa kwa sababu ya lugha. Ilikuwa kwa sababu shule aliyokuwa anasoma kulikuwa na wanafunzi mia katika darasa na niliona alihitaji kuangaliwa zaidi na walimu hivyo ile shule nyingine ilikuwa na wanafunzi 25 kwa darasa ... na vitabu ... na zana za kufundishia n.k. Aidha nadhani kuna kitu kingine ambacho hatujaangalia. Lipo tabaka fulani ambalo linaishi katika English Medium Environment (runinga, vitabu, lugha ya wazazi) ambayo inaifanya iwe rahisi wasome kwa Kiingereza pia). Kwa wale walio wengi ambao hawako katika EME hiyo itabidi wawe na akili ya ziada kufanikiwa hata kama wanasoma katika English Medium School. English medium siyo uchawi wa kuwageuza watu ghafla ingawa nadhani wazazi wengi wamedanganyika hivyo.

Hivyo, tusitumie Kiingereza kama kisingizio cha matatizo ya elimu lakini pia tusiponde ukweli kwamba wanafunzi walio wengi hawawezi kusoma masomo ya sekondari kwa lugha ya kiingereza. Kisha tufundishe kiingereza vizuri kabisa kama somo. Haina maana kukataa kutengeneza kufuli ya gari kwa kisingizio kwamba gari ni mkweche. Tutengeneze gari ndio lakini pia kufuli iii watu waweze kuingia na kufaidi gari.

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA