MHADHIRI DENIS MPAGAZE: KIGEZO CHA KUTUMWA NA WAZEE KUGOMBEA NAFASI YA UONGOZI NI HOJA DHAIFU

Kuna baadhi ya maandishi ukiyasoma basi kuna kitu lazima kitakugusa, na hii ndio inanisukuma kukichukua alichokiandika mwalimu wangu Mr. Mpagaze aliyenifundisha maswala ya mawasiliano ya umma mwaka wa pili nilipokuwa chuoni St. Augustine (SAUT)

Denis Mpagaze
Mtu unajijua kabisa uwezo wa kuwa kiongozi hauna. Kwa sababu ya tamaa na njaa zako unaamua kuwaadaa wananchi kwamba wazee wa mji wanakutaka ukagombee. Achana na hoja dhaifu! Kwanza kwa kauli hiyo ya kutumwa na wazee inaonesha jinsi unavyotegemea watu wafikiri kwa niaba yako na wakati kiongozi bora ni yule anayeonesha njia. Unaendeleza utamaduni wa kubebwa bebwa (Godfathers). Yaani ni ishara ya kwamba hata ukipata madaraka hutakuwa na uwezo wa kufanya maamuzi, badala yake utawaachia wazee kufanya maamuzi kwa niaba yako na kuipoteza jamii. Nasema hivi kwa sababu wazee watakushauri uwe na hofu ya maisha na kuishia kuwaibia wananchi.Kama huamini ninachokisema, angalia mafisadi wakubwa na wahujumu uchumi nchi hii karibu wote ni wazee!

Tunahitaji kiongozi mwenye uchungu wa maisha ya watu na siyo kiongozi anayeomba kuhurumiwa kwa sababu tu baba yake alikuwa kiongozi. Tunahitaji kiongozi anayejua matatizo ya wananchi wake kwa kina. Kiongozi anayejua nchi hii inaupungufu wa madaktari wangapi. Kiongozi hujui matatizo ya walimu, kiongozi hujui idadi ya albino, kiongozi hujui historia ya nchi yako, kiongozi hujui ukubwa wa eneo unaloliongoza, kiongozi hujui nchi hii imebaki na rasilimali kiasi gani, kiongozi hujui ni kiasi gani cha mabilioni yamefichwa ughaibuni, kiongozi hujui sababu za umaskini wa watanzania, sasa unaomba ridhaa yao ili ukafanye nini? Ukawaibie hata hicho kidogo kilichobaki. Unaposhidwa kuyajua haya yote kwa kina utaishia kushangaza Dunia kama walivyofanya watangulizi wako kwa kusema hawajui sababu za umaskini wa watanzania. Kiongozi dhaifu ataishia kuongozwa na jazba na lugha za kebehi badala ya kuonesha njia. Acha kukurupuka, eti umetumwa na wazee, jipange! Utaishia kuchekesha wagonjwa! Shauri lako!

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA