MAKALA: JE UMEANDAA MASWALI YA KUMUULIZA KIONGOZI WAKO KABLA YA UCHANGUZI UNAOKUJA? SOMA MAKALA HII KUTOKA KWA MHADHIRI MSAIDIZI CHUO CHA SAUT.
Mwandishi wa makala hii ni mhadhiri msaidizi na mkuu wa Idara ya mawasiliano na uandishi wa habari Chuo Kikuu Kishiriki cha Mt. Agustino cha Tanzania (SAUT) Songea. Anapatikana kwa denis_mpagaze@yahoo.com, 0753665484 au unaweza kusoma makala zake kupitia ukurasa wake wa facebook Denis Mpagaze
Ubabe, dharau, kejeli na unafiki ni dhambi ambazo zinalitafuna Taifa letu kwa kasi zaidi ya upepo. Nchi yetu imegeuka kuwa kisima cha ubabe, vitisho na dharau. Kitendo cha Mbunge wa Kasulu kuhoji mstakabali wa nchi yetu na kuitwa tumbili ni ubabe, dharau na kejeli. Kitendo cha wananchi wa Kigamboni kuhoji uhalali wa kuongezeka kwa nauli ya kivuko na kuambiwa asiyeweza kulipa apige mbizi ni dharau. Kitendo cha wananchi kuambiwa maji sio mkojo kupatikana kila sehemu ni kebehi. Kitendo cha wananchi kuuliza uhalali wa kigogo kutumia ndege ya serikali na kujibiwa mlitaka atumie punda ni majivuno. Kitendo cha waandishi wa habari kuhoji mstakabali wa nchi yetu na kuishia kung’olewa kucha na meno bila ganzi ni vitisho. Kitendo cha kusimama Bungeni na kukosoa bajeti na baadaye kuunga hoja kwa asilimia zote ni unafiki. Kitendo cha kuwaambia watanzania asiyeweza kulipia umeme atumie kibatari ni dharau. Mwisho wa dhambi hii siku zote hushangaza. Kwa nini nasema hivi?
Robert Kiyosaki kupitia kitabu chake cha Rich Dad Poor Dad anasema kwamba historia ni mwalimu mzuri. Ni historia inayonipa nguvu na ujasiri kusema kwamba matokeo ya ubabe, dharau, unafiki na kejeli siku zote hushangaza. Bas twende pamoja katika kuthibitisha kauli yangu kwa kurejea kumbukumbu katika historia.
Katika kitabu chake kiitwacho, “A Night to Remember”cha mwaka 1976, uk 73 Walter Lord ameonesha dharau na majivuno aliyokuwanayo mbunifu wa meli ya Titatic. Mbunifu huyo alipoulizwa na waandishi wa habari kuhusu usalama wa meli hiyo kubwa kuwahi kutokea, alijibu “meli hiyo ni kubwa kiasi ambacho hata Mungu hawezi kuizamisha”. Matokeo ya kauli hii yaliishangaza dunia. Meli hiyo ilizama na kuacha huzuni kuu. Na hili ni funzo kwa viongozi mliojaa dharau na mizaa mpaka kumkufuru hata Mungu. Acheni!
Mobutu Sese Seko Kuku Ngbendu wa Za Banga baada ya kuwa rais wa kwanza Afrika kupata misaada mingi kutoka USA aliota kiburi na majivuno. Aliitangazia Dunia kwamba yeye ni kuku anayeatamia nchi ya Congo wakati huo ikiitwa Zaire. Huwezi amini kwa dharau zake alijifananisha na Mungu. Kabla ya taarifa ya habari, luninga ya Taifa ilionesha picha yake akishuka kutoka mawinguni na watu wote walikaa kimya kumlaki mtukufu Mobutu Sese Seko Kuku Ngbendu wa Za Banga. Ni kufuru. Alijenga majumba ya kifahari kila kona ya Dunia wakati mamilioni ya wakongo wakiishi maisha ya Kanyaga Twende. Ni ushenzi. Mwisho wake ulishangaza sana. Alifariki akiwa uhamishoni Rabat, Morocco kwa ugonjwa wa kansa akiwa na umri wa miaka 66, na kuzikwa na watu wanne tu. Hili ni funzo kwa viongozi wenye tabia za Mobutu Seseko. Acheni!
Yuko wapi Saddam Hussein, mbabe aliyoitikisha Dunia mpaka kututia hekaheka ya kuchimba mahandaki kila kona ya nchi yetu. Wengi mnakumbuka. Alitishia kulipua visima vya mafuta ambavyo madhara yake yangekuwa kuiangamiza Dunia. Huu ulikuwa ubabe. Je mnaukumbuka mwisho wake? Pamoja na ubabe wake, alikuja kukamatiwa kwenye shimo mithili ya panya aliyemkimbia paka. Inashangaza na pengine inaweza kuwa funzo kwa viongozi wababe ndani ya nchi yetu kama Saddam. Mbabe siku zote hana rafiki.
Yuko wapi Adolf Hitler aliyemfananisha mtu mweusi na nyani pale alipowashinda wazungu katika mbio za Olympic. Hitler alikataa kumpa mkono jamaa yetu kwa husema haiwezekani binadamu kushindanishwa na nyani. Hii ilikuwa ni kufuru na chukizo kwa Mungu. Nampenda sana hayati Luck Dube, kwa maneno yake matamu, “When I see a black man...I see the image of God, when I see a white man...I see the image of God, I see an Indian...I see the image of God, colours and everybody, we are the images God”, Ni hekima za Lucky Dube .Mwisho wa Hitler nadhani kila mtu anaufahamu. Unashangaza! Hata kaburi lake halijulikani liko wapi. Hili nalo ni funzo kwa viongozi wa namna hii.
Yuko wapi Jonas Savimbi, dikteta wa Angola aliyewakata vidole watoto wetu ili wasije kumpindua madarakani ? Leo vijana wengi huko angola hawana vidole. Ni ubabe huu. Ukiambiwa kifo chake utashangaa. Alifia barabarani na maiti yake kuburuzwa mji mzima kama mzoga wa mbwa kabla ya kuzikwa chini ya mti. Inashangaza. Chukua funzo hili kama ni miongoni mwa viongozi wababe na wenye roho mbaya. Kitendo cha kuuza madawa ya kulevya ni kuwakata vidole watanzania. Acheni!
Yuko wapi aliyewatandika walimu wa shule ya msingi viboko huko Bukoba? Kwa mara ya mwisho nilimsikia kachoka mbaya.Siyo mkuu wa wilaya tena. Ni madhara ya kutumika. Leo hii kiongozi unasimama juu ya majukwaa na kuanza kuporomosha matusi, kejeli na maudhi, kisa umekubali kutumika. Nakwambia we endelea tu, matokeo yake yatakushangaza. Nadhani hili ni funzo kwa wale wote wanaotumika kwa maslahi ya wachache! Acheni!
Yuko wapi Benito Monsoln, aliyekuwa akiwaweka roho juu wachezaji wa Mpira huko Italia kila ilipokaribia kombe la Dunia? Aliwaambia kama hawatachukua Kombe la Dunia atawachinja wote. Ni vitisho hivyo. Leo pamoja na vitisho vyake anarutubisha ardhi ya Italia. Narudia tena, mwisho wa ubabe na vitisho unashangaza.
Yuko wapi Idd Amin aliyewalazimisha watu kucheka na walioshindwa kucheka aliwakata midomo na meno kubaki nje mithili ya mtu anayecheka? Leo hayupo tena. Kafa kifo cha aibu uhamishoni . Inashangaza. Bado tu hamjifunzi?
Nawakumbusha viongozi wenye kauli za kibabe, maudhi na kinafiki kwamba matokeo yake yatawashangaza. Wakumbuke kwamba kwa ubabe wao,watanzania tunadhoofika, kwa unafiki wao watanzania tunasalitiwa, kwa majivuno yao watanzania tunaumia, kwa dharau zao watanzania tunaugua. Hata maneno ya Mungu yanasema kupitia Mithali 29:2,b; "bali mwovu atawalapo,watu huugua". Mwaka 2011 jijini Dar Es Salaam aliyekuwa rais wa awamu ya tatu alisema, “kuwa na viongozi wasiokuwa waadilifu kunasababisha kuwa na Serikali za hovyo zisizojali matakwa ya wananchi”. Kutojali wananchi ni ubabe, dharau, kejeli na unafiki.
Najua kinachowasumbua ni ulevi na ulimbukeni wa madaraka kama alivyowahi kusema mtaalam wa uandishi wa riwaya, George Orwell, kuwa, “Power corrupts and absolute power corrupts absolutely”akimaanisha madaraka yakizidi hulevya. Hakika viongozi wetu wamelewa kwa ukubwa wamadaraka na wananchi wamelewa kwa mizigo ya umaskini na kero. Inashangaza!
Bila kujalisha nani kalewa nini na kwa sababu gani, ukweli ni kwamba, Dunia haitakukumbuka kwa ubabe wako, kwa unafiki wako, kwa kejeli zako, kwa dharau zako, kwa majivuno yako, bali itakukumbuka kwa namna matendo yako mema yamevyogusa nyoyo za watu. Leo mpaka wapinzani bila kujali itikadi zao wanamkumbuka Mwl Julius Nyerere, wanamkumbuka Mahatma Ghandi, wanamkumbuka Nelson Mandela.
Watu hawa wanakumbukwa kwa sababu ya matendo yao mema na si kauli za kibabe, kinafiki na kujipendekeza. Ni watu ambao walikuwa tayari kufa kwa ajili ya watu. Alipopigwa teke la mdomoni na askari wa kikaburu kule Afrika kusini, Mahtma Ghandi aliinuka na kujifuta mavumbi na kuuliza, “Afande, hivi kiatu chako kimepona? Pamoja na kuwekwa jela miaka 27 bado Nelson Mandela aliwasamehe adui zake na kuwa tayari kufanya nao kazi. Baada ya kuusotea uhuru wa Tanganyika kwa muda mrefu bado Nyerere alijiona hayuko huru mpaka Afrika yote iwe huru. Alianza harakati. Wote mnakumbuka. Mpende jirani yako kama nafsi yako, hakika utakumbukwa daima.
Kijana mmoja alikuwa akisafiri kwa basi. Wakati wa safari alikuwa anafoka na kutukukana watu hovyo. Wakati anashuka, abiria mmoja akamwambia, “Kijana umeacha kitu”. Kijana akauliza kwa ukali. “Nimeacha nini?” Abiria akamwambia umeacha jina chafu.
Nachotaka kusema ni kwamba, tunaelekea uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu hivi karibuni, nakuomba msomaji wangu bila kumung’unya maneno, muulize mbunge wako, diwani wako, mwenyekiti wako wa mtaa na rais wako ameacha jina gani kabla hajaomba ridhaa tena ya kukutawala. Nyie ulizeni maswali hayo tu na mtaona matokeo yatakavyoshangaza!
Comments
Post a Comment