OBAMA NA MERKEL WAZUNGUMZIA MADAI YA UDUKUZI

Rais wa Marekani Barrack Obama amezungumza kwa njia ya simu na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, hiyo ikiwa mara ya kwanza viongozi hao kuzungumza tangu kuibuka upya kwa madai ya udukuzi unaofanywa na Marekani
Viongozi hao wawili walikuwa bado hawajafanya mazungumzo yoyote tangu kuibuka kwa madai kuwa Marekani iliwatumia maafisa wawili wa kijasusi wa Ujerumani kupokea taarifa za kijasusi kuihusu Ujerumani.

Madai hayo yaliyoighadhabisha Ujerumani kwa mara nyingine tena yalisababisha kufurushwa kwa afisa wa ngazi ya juu wa shirika la kijasusi la Marekani kutoka Berlin wiki iliyopita.
Taarifa kutoka ikulu ya Rais wa Marekani imesema wakati wa mazungumzo hayo ya simu viongozi hao wawili walibadilishana mawazo kuhusu ushirikiano wa taarifa za kijasusi kati ya Ujerumani na Marekani na inasemekana Rais Obama anafuatilia kwa karibu jinsi ya kuimarisha uhusiano huo ili usonge mbele.

Madai ya udukuzi yazorotesha uhusiano
Obama na Merkel wamekuwa na ushirikiano thabiti wa kikazi na kushirikiana katika masuala mengi muhimu zikiwemo sera za kigeni na ubadilishanaji wa taarifa za kijasusi kukabiliana na kitisho cha ugaidi lakini madai ya udukuzi yametia doa kwenye uhusiano huo na kumekuweko ongezeko la shinikizo kisiasa nchini Ujerumani kwa viongozi wake kuchukua msimamo mkali kuhusiana na mwenendo huo wa Marekani kumchunguza mshirika wake mkubwa barani Ulaya.

Mbali na mazungumzo hayo kati ya Obama na Merkel kutuama katika suala hilo la udukuzi na ushirikiano wa kijasusi,viongozi hao pia waliuzungumzia mzozo wa Ukraine na kukubaliana kuwa Urusi sharti ichukue hatua mara moja kuupunguza mzozo huo.

Merkel na Obama wametilia mkazo kuwa Urusi inapaswa kuunga mkono makubaliano ya kusitishwa mapigano mashariki mwa Ukraine, mchakato wa mazungumzo ya kutafuta amani chini ya usimamizi wa shirika la usalama na ushirikiano barani Ulaya OSCE na kuundwa kwa mfumo wa uangalizi wa mipaka utakaosimamiwa pia na OSCE.

Mzozo wa Ukraine wajadiliwa pia
Mazungumzo hayo yanakuja saa chache kabla ya mkutano wa viongozi wa nchi za umoja wa Ulaya unaotarajiwa kufanyika leo mjini Brussels kutafakari kuiwekea Urusi vikwazo zaidi vya kiuchumi kutokana na mzozo huo wa Ukraine.

Marekani imesema itaichukulia Urusi vikwazo kivyake iwapo bado Umoja wa Ulaya unasita kufanya hivyo.
Aidha viongozi hao wa Marekani na Ujerumani wameyajadili mazungumzo yanayoendelea mjini Vienna kuhusu mpango wa kinyuklia wa Iran na kusema bado kuna tofauti juu ya masuala muhimu na kuitaka Iran kuchukua hatua muafaka zitakazoihakikishia jumuiya ya kimataifa kuwa mpango wake wa kinyuklia ni kwa ajili ya amani pekee.

Hayo yanakuja huku kukiwa na dalili kuwa muda wa mwisho uliowekwa wa kufikia makubaliano kamili kati ya Iran na nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani hautaafikiwa na huenda ukaongezwa kutoka Jumapili hii kwa miezi mingine kadhaa.

Mwandishi:Caro Robi/afp/dpa
Mhariri:Daniel Gakuba

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA