Watishia kufunga viwanda vya bia na vya pombe kali
Uamuzi huo umekuja baada ya wenye viwanda vya
vinywaji hivyo kubaini kuwa Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2014/15
uliotolewa Julai 11, mwaka huu, unataja kuwa kodi kwa bidhaa hizo
itakuwa asilimia 20.
Akizungumza jana, mwakilishi wa wenye viwanda
nchini, David Mgwassa alisema uamuzi wa kupandisha kodi kinyemela
umewaacha njiapanda wenye viwanda kwa kuwa hawajui walipe kodi ipi kati
ya asilimia 10 au 20 na kwamba, iwapo Serikali haitapunguza, watafunga
baadhi ya viwanda ili kumudu ongezeko hilo jipya la kodi.
“Kila kampuni inafanya utafiti ili kufunga viwanda
vyote na kubaki na kimoja kikubwa kitakachopunguza gharama. Pia
ikumbukwe kuwa kuna viwanda vilijengwa kwa lengo la kuja kubinafsishwa,
hivyo wengi watakosa ajira. Wawekezaji wana wasiwasi kama Tanzania ni
sehemu nzuri kuwekeza tena.
“Kodi ya mwaka 2014 ni ipi? Viwanda vilipanga bei
kulingana na asilimia 10, lakini Muswada wa Sheria ya Fedha unasema kodi
hiyo imeanza rasmi kutoka Julai 1, mwaka huu, tutafilisi viwanda,”
alisema Mgwassa.
Pia alihoji: “Kwa nini Bunge lijadili na kupitisha
kodi asilimia 10 halafu muswada useme asilimia 20. Ni nani anayemtania
mwenzake?”
Alisema iwapo mahitaji ya bidhaa hizo yatapungua
nchini, kampuni zinazomiliki viwanda vya vinywaji zitalazimika kupunguza
uzalishaji.
Alisema viwanda vya bia na vinywaji vikali
vinapambana na ushindani mkali kutoka bidhaa za nje zinazoingia nchini
kinyume cha sheria, jambo linaloweza kuufanya uchumi ukashuka iwapo hali
hiyo haitadhibitiwa.
chanzo: Mwananchi.
chanzo: Mwananchi.
Comments
Post a Comment