Kalou Na Drogba Wainyonga Taifa Stars ( Mwananchi)

TANZANIA imeanza vibaya kampeni zake za kucheza Fainali za Kombe la Dunia Brazil 2014 baada ya kufungwa mabao 2-0 na Ivory Coast.

Katika mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Felix Houphouet Boigny, Stars ilijitahidi kucheza kandanda la kawaida kwa pasi za kawaida tofauti na ilivyotarajiwa.

Ikiwa ni mtihani wa pili kwa kocha wake, Kim Poulsen baada ya mchezo wa kwanza wa kirafiki na Malawi kutoka 0-0, Stars ilipoteana dakika ya tisa tu na kufungwa bao kirahisi lililowekwa kimiani na Solomon Kalou.

Kalou aliwapiga chenga mabeki watatu wa Stars baada ya kuunasa mpira mguuni kwa Kelvin Yondan aliyezubaa kuuondosha akiwa ndani ya eneo la hatari.

Baada ya bao hilo, Stars ilijipanga upya na kuelekeza mashambulizi langoni kwa wapinzani wao na dakika ya 14, Aggrey Moris alipiga mpira wa adhabu uliogonga mwamba lakini hata hivyo, wachezaji wa Ivory Coast walikuwa makini kuondosha.

Katika dakika ya 22, Didier Drogba naye aligongesha mwamba kwa mpira wa adhabu iliyosababishwa na Morris baada ya kumkwatua Kalou akiwa nje kidogo ya eneo la hatari. Morris alionyeshwa kadi ya njano kwa faulo hiyo.

Dakika mbili baadaye, ushirikiano wa Mbwana Samatta na Morris aliyepanda kusaidia mashambulizi nusura uzae bao lakini hawakuwa makini.

Beki huyo anayechezea Azam alipiga kombora lililotokana na mpira wa adhabu baada ya Mwinyi Kazimoto kukwatuliwa ndani ya eneo la hatari na Tiote lakini hata hivyo likatoka nje.

Stars iliendelea kuliandama lango la wapinzani wao na katika dakika ya 36, ilipata kona tatu mfululizo zilipigwa na Amir Maftah lakini hata hivyo zilikuwa tasa. Dakika ya 40 hadi kumalizika kipindi cha kwanza, Stars ilicheza pasi za hapa na pale na kuwachanganya Ivory Coast.

Kipindi cha pili kilianza taratibu na hata hivyo Stars iliyokuwa na uchu nusura ipate bao dakika ya 62 lakini kichwa cha Samatta hakikulenga lango, kabla ya Gervinho kujibu dakika mbili baadaye baada ya kumtoka Maftah.

Kocha wa Ivory Coast, Sabri Lamouchi alifanya mabadiliko kwa kuwatoa Gervinho na Tiote na nafasi zao kuchukuliwa na Kader Keita na Konnan Didier.

Stars ilipata pigo dakika ya 63 baada ya beki wake wa kati, Morris kulimwa kadi nyekundu kwa kumkwatua Kalou ikiwa ni kadi ya pili ya njano. Kuona hivyo, Kim Poulsen alimtoa Salum Aboubakar na nafasi yake kuchukuliwa na John Boko.

Dakika ya 70, Didier Drogba aliipatia Ivory Coast bao la pili kwa mpira wa kichwa baada ya kuunganisha krosi ya Keita. Kuona hivyo, Poulsen alimtoa Boko na kumuingiza Erasto Nyoni kwa ajili ya kuimarisha safu ya ulinzi.

Lolo Alexander alimchezea rafu mbaya Kazimoto na hakuweza kurudi uwanjani katika dakika ya 89. Stars ilishindwa kufanya mabadiliko kutokana na kumaliza wachezaji wake wote wa akiba

Katika mchezo huo Stars iliwakilishwa na: Kaseja, Kapombe, Maftah, Yondan, Agrey Morris, Shaaban Nditi, Salum Aboubakar/John Boko, Frank Domayo, Mbwana Samatta, Ngassa na Mwinyi Kazimoto.

Ivory Coast: Bary Boubacar, Emmanuel Eboue, Tiene Siaka, Kolo Toure, Lolo Igor, Gosso Gosso Jean, Yao Kouassi, Cheikh Tiote, Didier Drogba na Solomon Kalou.

Chanzo: Mwananchi

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA