WALIOCHAGULIWA KUFANYA USAILI WA POLISI HADHARANI



Na Thomas Dominick
Musoma

JESHI la Polisi Mkoa wa Mara limetoa majina ya vijana ambao wamechaguliwa kwa ajili ya kufanya usaili wa kujiunga na jeshi hilo ambapo kanda ya ziwa utafanyika Julai 2 hadi 4 mwaka huu katika ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza.

Akizungumza na waaandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Absalom Mwakyoma alisema kuwa majina hayo yatabandikwa kwenye mbao za matangazo zilizopo katika ofisi za Mkoa na wilaya zote.

“Mwaka huu tumeamua kuchukua vijana watakaojiunga na jeshi letu kutoka mashuleni ambao wamemaliza kidato cha nne mwaka jana na cha sita mwaka huu hivyo tunawaamba vijana wote waende wasome na wajue kama jina lake lipo katika orodha yetu,”

“Hii tumerahisisha ili kupunguza msongamano wa vijana kufika katika ofisi zetu na kuulizia ajira hizo na kama unatumia mtandao tafuta katika mtandao wetu wa www.policeforce.go.tz na utaona jina lako na vituo vya usaili,”alisema.

Alisema kuwa vijana ambao wataona majina yao waende katika kituo cha usaili katika kanda mbalimbali kama zitavyoonesha katika matangazo yao wakiwa na vyeti halisi vya elimu yake na cheti cha kuzaliwa.

“Tunasisitiza kwa watahiniwa kufika katika vituo hivyo na vyeti vyao pia tunawakumbusha kuwa hati ya kiapo ya mahakamani haitakubaliwa na awe na barua ya wadhamini wawili wanaomfahamu vizuri zinazoelezea mahusiano baina yao na muombaji na namba za simu na anuani halisi ambazo zinatumika,”alisema Kamanda Mwakyoma.

Alisema kuwa kila kijana ambaye ataona jina lake atajigharamia gharama zote za usafiri, chakula na malazi muda wote wa usaili pamoja na kalamu za wino kwa ajili ya kuandikia.

Kamanda Mwakyoma alisema kuwa mtahiniwa anaruhusiwa kufanya usaili katika kanda yoyote kulingana na tarehe husika kuepusha usumbufu wa kusafiri safari ya mbali.

Jeshi hilo la Polisi limeamua kutumia mfumo huo ambao ulikuwa unatumika miaka ya nyuma walikuwa wanatoa moja kwa moja mashuleni ili kuepusha upendeleo na malalamiko kwa wanyonge.

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA