BASATA YAWATAKA WASANII KUONGEZA THAMANI KATIKA KAZI ZAO
Mtendaji
Mkuu wa asasi ya Musoma Handcrafts Haroun Sabili akitoa elimu kwa
Wasanii na Wajasiriamali wa Sanaa za mikono kwenye programu ya Jukwaa
la Sanaa wiki hii.
Mkurugenzi
wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Habari wa BASATA Godfrey Lebejo
akisisitiza jambo wakati akihitimisha programu ya Jukwaa la Sanaa wiki
hii. Aliwataka wasanii kuongeza thamani katika kazi wanazozalisha.
Akina
mama Wasanii wa Sanaa za mikono wakiangalia moja ya kazi iliyobuniwa na
kuongezewa uthamani. Kazi hiyo ilikuwa imetengenezwa na malighafi
kutoka masalia ya viumbe wa baharini.
Sehemu
ya Wasanii na Wadau wa Sanaa za Mikono waliohudhuria kwenye programu ya
Jukwaa la Sanaa wiki wakifuatilia darasa kwa makini.
Na Mwandishi Wetu
Huku
kukiwa na juhudi za kutambuliwa na kuthaminiwa kazi za wasanii ndani na
nje ya nchi, Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limewataka wasanii
kuongeza thamani kwenye kazi zao ili kuzipa ubora zaidi.
Wito
huo umetolewa mapema wiki hii na Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti,
Mafunzo na Habari wa BASATA Godfrey Lebejo wakati akihitimisha programu
maalum iliyohusu Ubunifu, Utengenezaji na Uongezaji thamani katika Kazi
za Sanaa kupitia Jukwaa la Sanaa.
Alisema
kuwa, ubora katika Sanaa unapatikana pia kwa Wasanii kuangalia wenzao
wanafanya nini na wao kupata ubunifu mpya kwa kuongeza vionjo, uthamani
na ubunifu binafsi katika kuifanya kazi ya Sanaa kwanza kupendwa na
baadaye kupewa thamani kubwa sokoni.
“Ni
wazi Wasanii wetu wanapaswa kuzingatia uongezaji uthamani kwenye kazi
wanazozifanya. Kubuni kazi ni suala moja lakini kuongeza uthamani
katika kazi yako ili ivutie wengi na kuuzika kwa thamani kubwa ni suala
lingine la kuzingatia” alisistiza Lebejo.
Aliongeza
kuwa, kwa sasa kuna taarifa za Wakenya kununua kazi za Wasanii wetu kwa
bei ya chini na baadaye kuziongezea ubunifu, thamani na kuziuza nje kwa
bei kubwa. Katika hili anasema, inatokana na wasanii wetu
kutokuzingatia falsafa hiyo ya ubunifu na uongezaji thamani wa kazi zao.
“Tuna
bahati ya kuwa na malighafi nyingi sana, baadhi zimeoneshwa hapa lakini
suala hapa ni sisi kutumia ipasavyo malighafi hizo katika kubuni kazi
zenye ubora na kuhakikisha tunazipa thamani stahiki tunapozisafirisha
nje” alizidi kusisitiza.
Awali
akiendesha darasa hilo maalum ambalo wiki hii lilikuwa mahsusi kwa
ajili ya wasanii na wajasiriamali wa Sanaa za mikono (Handcrafts),
Haroun Sabili kutoka asasi ya Musoma Handcraft alisema kuwa, Sanaa hizo
zinahitaji ubunifu na umakini mkubwa kwani kinyume chake ni kutokuvutia
na kupoteza uthamani.
Alitoa
wito kwa Wasanii kujiunga katika vikundi na kuwa rasmi ili kuhakikisha
kwanza,wanajenga mazingira ya kuwezeshwa lakini pia kupata mafunzo
mbalimbali ambayo yatawafanya wazalishe kazi za Sanaa zenye ubora na
thamani kubwa.
“Ni
ngumu sana kuhudumia msanii mmoja-mmoja lakini mkiwa kwenye umoja ni
rahisi sana kupata fursa za uwezeshaji hususan mafunzo katika kuongeza
ubunifu na uthamani wa kazi zenu” alishauri Haroun.
Katika
programu hiyo iliyohudhuriwa na wadau 72, elimu kuhusu ubunifu na
uongezaji thamani kwenye kazi za Sanaa ilitolewa sambamba na malighafi
mbalimbali na jinsi zinavyoweza kutumika kuzalisha kazi za mikono
kuoneshwa.
source www.freebongo.blogspot.com
Comments
Post a Comment