CCM yasema: Mawaziri watuhumiwa washitakiwe! Kama Mkapa alienda kortini...

 
Chama chenye hatamu ya madaraka Tanzania kwa sasa, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimesema hakitakuwa na huruma kwa Mawaziri ambao wamewajibishwa kutokana na wizara zao kutajwa kwenye Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwamba zimehusika na ufisadi, badala yake kitakuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanafikishwa mahakamani.

Kauli hiyo imekuja kipindi ambacho tayari Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), inafanya uchunguzi dhidi ya mawaziri sita ambao wametajwa kwenye ripoti hiyo ya CAG na ambao Rais Jakaya Kikwete aliwang’oa katika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri.

“Kama uchunguzi wa TAKUKURU utathibitisha tuhuma hizo, watapanda kizimbani kwa kuwa hakuna aliye juu ya sheria,” Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema jana.

Akitolea mfano wa Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa kupanda kizimbani juzi kutoa ushahidi kwenye kesi inayomhusu aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu, Nape alisema: “Hii inathibitisha kuwa hakuna aliye juu ya sheria za nchi.”

Nape alikuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa chama hicho, mjini Dodoma ambako pamoja na mambo mengine, alitangaza ratiba ya Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC).

“Katika hilo nasema kuwa hakuna aliye juu ya sheria, jana (juzi) Mzee Mkapa alipanda mahakamani kwa ajili ya kutoa ushahidi, iweje hao wengine waachwe? Nasema kama walihusika na ikathibitika kweli hata kama wengine wamebaki katika baraza, ni lazima watawajibika,’’ alisema.

Mawaziri walioachwa katika baraza hilo jipya ni Mustafa Mkulo (Fedha), Mhandisi Omary Nundu (Uchukuzi), Dkt. Hadji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii), Dkt. Cyril Chami (Viwanda na Biashara), Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii) na William Ngeleja (Nishati na Madini).

Wengine waliokuwa wakitajwa kuguswa katika ripoti ya CAG ni George Mkuchika aliyekuwa Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI na Profesa Jumanne Maghembe aliyuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika. Mawaziri hao sasa wamehamishwa katika wizara hizo. Mkuchika sasa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora) na Profesa Maghembe ni Waziri wa Maji.

Nape alikiri kupata taarifa za mawaziri hao wa zamani kuchunguzwa na TAKUKURU, lakini akasema katika mtego huo si wote ambao wanaweza kunaswa.

Kuhusu wabunge wa CCM waliotia saini barua kutaka kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu ikiwa ni shinikizo la kutaka mawaziri hao wajiuzulu au wawajibishwe, Nape alisema chama chake hakifikirii na hakitathubutu kuwajadili.

Akizungumzia ratiba ya kikao hicho, alisema Kamati ya Maadili ya CCM itakutana Jumamosi ijayo chini ya Uenyekiti wa Rais Kikwete na baadaye siku hiyohiyo, Kamati Kuu itakutana.


via  gazeti la Mwananchi

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA