Polisi 700, JWTZ 248 waumbuliwa Vitambulisho vya Taifa
MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), imebaini kuwa Jeshi la Polisi lina askari 700 wenye majina yanayofanana na waajiriwa wengine serikalini huku Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) likiwa na askari 248.
Mkurugenzi Mkuu wa Nida, Dickson Maimu (pichani) alisema jana Dar es Salaam kwamba watumishi hao wamebainika kutumia cheti kimoja cha elimu na mtu mwingine jambo ambalo lilikuwa changamoto kubwa wakati ilipoanza uandikishaji kwa watumishi wa Serikali.
Maimu alikuwa akitoa kwa waandishi wa habari, taarifa ya utekelezaji wa mradi wa vitambulisho vya Taifa na kubainisha kuwa hiyo ni dalili kwamba watumishi wake watakabiliwa na changamoto kubwa katika kuhakikisha kwamba kila Mtanzania anapata kitambulisho cha uhakika.
“Kwa hivi sasa maeneo tuliyopitia tumegundua kuna utumiwaji wa vyeti mara mbili vyenye jina moja na mkitaka niwatajie. JWTZ tumekuta watu 248 na Polisi watu 700 ambao vyeti vyao vinatumiwa na watu wawili tofauti,” alisema Maimu.
Kuhusu hali ya mradi, Maimu alisema wameamua kisitisha kwa muda uzinduzi wa vitambulisho hadi Juni Mosi, mwaka huu siku ambayo vitambulisho hivyo vitaanza kutolewa kwa wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam.
“Mamlaka ya vitambulisho vya taifa imekamilisha hatua zote na tuko tayari kuzindua mradi wetu na kutoa vitambulisho. Hata hivyo, zimejitokeza changamoto na mahitaji ya msingi kutoka kwa wadau wetu muhimu ambavyo hatuna budi kuvifanyia kazi kwanza ili kitambulisho kiwe kimekidhi mahitaji yote,” alisema.
Maimu alisema mahitaji makubwa yaliyojitokeza ni mfumo wa vitambulisho kutambua na kuingiza anuani za makazi na postikodi, kufanya usajili wa pamoja na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) na kuwezesha rasimu ya ukusanyaji maoni ya Katiba Mpya chini ya tume iliyoundwa.
Maimu alisema taarifa hizo zitasaidia kupatikana kwa urahisi taarifa kamili za wakazi katika eneo husika, chini ya Serikali za Mitaa.
“Tayari tumeshafanya mazungumzo na mkandarasi (Iris) kuweza kuingiza katika mfumo mahitaji haya makubwa ya wadau wetu,” alisema Maimu.
Alisema maandalizi ya awamu ya kwanza yamekamilika na Nida iko tayari kutoa vitambulisho kwa awamu ya kwanza, baada ya mkandarasi kukamilisha kuingiza mabadiliko makubwa mawili ya mfumo wa daftari la kielektroniki.
“Mabadiliko hayo ni anwani za makazi na simbo za posta(postal code), pia kufanya usajili wa pamoja na Nec,” alisema Maimu.
Alisema Serikali imeamua kuwa uandikishwaji wa vitambulisho unapaswa uende sambamba na ule wa wapiga kura ili kupunguza gharama na usumbufu unaoweza kujitokeza kwa kuwaita watu walewale kujiandikisha mara nyingi ndani ya kipindi kifupi.
“Baada ya kutambua umuhimu wa kupunguza gharama za uendeshaji pamoja na kupunguza adha kwa wananchi, Nida imefanya majadiliano na Nec na kukubaliana kuwa zoezi la usajili lifanyike kwa kushirikiana kwa pamoja katika nyanja za vifaa, watumishi na wakandarasi,” alisema Maimu.
Alisema kutokana na hali ilivyo, kazi hiyo itafanyika kwa mwaka mmoja na nusu badala ya miaka minne kama ratiba ya awali ilivyokuwa ikionyesha.
“Imekuwa lazima sasa kutumia vitambulisho kwa ajili ya uchaguzi na Katiba Mpya ambayo ‘referendum’ (kura za maoni ) itakuwa mwaka 2014,” alisema na kuongeza kuwa Maimu alisema mchakato wa usajili utatanguliwa na ujazaji wa madaftari ya wakazi.
“Madaftari haya ni muhimu katika kutunza kumbukumbu za wananchi wanaoishi katika eneo husika na pia kusaidia upatikanaji wa haraka wa taarifa za wananchi pindi zinapohitajika.”
Comments
Post a Comment