CHADEMA YAITEKA MTWARA
Aliekuwa
Mbunge wa Arusha Mjini, Mh Godbless Lema akihutubia maelfu ya wananchi
wa Mtwara katika Viwanja vya Mashujaa jana. CHADEMA wako mikoa ya
kusini mwa Tanzania kwa ziara ya kuimarisha chama hicho katika maeneo
hayo na pia kuutanzaza mapango wao mpya wa kuwashirikisha wananchi
katika shuguli za chama (Movement for Change-M4C) kuanzia jana hadi
Juni 11, 2012
*********
DHANA
ya kuwa mikoa ya kusini ni ngome ya Chama cha Mapinduzi jana ilifutika
vichwani mwa wakazi wa mikoa hiyo, baada ya umati mkubwa kujitokeza,
kuulaki msafara wa viongozi na hatimaye kuhudhuria mkutano mkubwa wa
hadhara uliofanyika katika viwanja vya Mashujaa, mkoani Mtwara.
Msafara
huo wa kitaifa ukiongozwa na Mwenyekiti Freeman Mbowe, ulipata mapokezi
ya vijana wakiwa katika msafara wa pikipiki magari na baiskeli karibu
na daraja la Mikindani na kuelekea katika uwanja wa Mashujaa ambapo
umati mkubwa wa watu ulifurika kupita kiasi.
Akihutubia
katika mkutano huo Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Freeman Mbowe alisema
ameshajiandaa kisaikolojia kufa kwa ajili ya kutetea haki na kwamba
wananchi wasiogope kupigania haki zao.
Alisema
ikitokea akafa akiwa katikati ya mapambano waliobaki wasihuzunike bali
wahakikishe huo ndiyo unakuwa mwanzo wa ukombozi.
“Nikifa
katika mapambano haya uinueni mwili wangu uwekeni pembeni na kisha
endeleeni na mapambano kwa kuwa haya si ya Mbowe peke yake bali ni ya
Watanzania wote,” alisema Mbowe.
Aliwaambia
wakazi wa Mtwara kuwa hawakwenda pale kutafuta jimbo au kata bali
kuleta ukombozi wa kweli kwa kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania
kuhakikisha nchi inakombolewa.
Akizungumzia
kuhusu udini, Mbowe alisema viongozi wa serikali wanaotumia udini,
ukabila na ukanda kuwagawa watu wamekata tamaa ya kuwatumikia.
Alisema
kuwa kwa hali ilivyo itakuwa ni hatari zaidi kwa ustawi wa Tanzania
kama hata tone moja la mafuta yatapatikana huku nchi ikiwa inaongozwa
na serikali ya CCM kwa kile alichodai tayari wamemwaga damu kwa tamaa
ya mali katika rasilimali zilizokwishaanza kupatikana.
Naye
Katibu mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, aliwataka polisi kuacha
kuwanyanyasa raia na kueleza hata yanayotokea Zanzibar kwa sasa ni
udhaifu wa Rais Jakaya Kikwete wa kutaka kuzuia watu wasitoe maoni.
Alisema
hatua ya kuwataka watu wasijadili suala la Muungano wakati unawagusa
haiwezi kukubalika na kwamba polisi wawe na akili ya kuambiwa na kisha
kuchanganya na zao kwa ajili ya maslahi ya Tanzania.
“Kikwete
amesababisha hali hii ya Zanzibar, maana hakukuwa na haja ya kumkamata
mtu aliyekuwa anatoa maoni juu ya mustakabali wa nchi yake,” alisema
Dk. Slaa.
Kuhusu bajeti ya 2012/2013 Dk. Slaa alitaka isimamishwe na mishahara ya wafanyakazi iboreshwe.
Kuhusu
korosho, Dk. Slaa alisema wakazi wa Mtwara wanafanywa maskini huku
korosho zao zikienda kutoa ajira kwa wananchi wa India na wajanja
wachache wa hapa nchini.
“Tanzania
haitakombolewa bila mikoa ya kusini kuwa huru, tunataka mtuunge mkono
katika kila hatua ili tuchukue nchi 2015,” alisema Dk. Slaa.
Mnyika adai Bunge ni Kanyaboya
Mbunge
wa Ubungo John Mnyika akihutubia umati huo alisema Bunge la Tanzania
halina nguvu ya kuiwajibisha serikali na kama litafanya hivyo Rais
anaweza kuwatimua wabunge wote.
Alisema
hali hiyo inachangiwa kwa kiasi kikubwa na Katiba liyopo ambayo alisema
ni lazima Watanzania wajitokeze na kuingiza mambo ya msingi wakati wa
kutoa maoni.
Aliongeza
wakazi wa Mtwara wanashindwa kufaidika na gesi iliyoko mkoani humo
pamoja na kukosa uwezo wa kumiliki ardhi kwa amendeleo yao.
Mawazo abeba silaha
Aliyekuwa
diwani wa CCM kata ya Arusha Alphonce Mawazo aliwaambia wakazi wa
Mtwara kuwa mabadiliko ya kweli huanza kwenye akili na mtu akishafungua
akili kila kitu chake kitaenda kwa ufasaha na kuwa huru.
Huku
akishangiliwa na umati wa watu uwanjani hapo Mawazo alisema wameenda
Mtwara wakiwa na silaha za nguvu ya umma, na kuwataka wasitengane
katika kutafuta mabadiliko ya kweli, na kuachana na waliowasaliti kwa
kuwaingiza katika maisha magumu.
Aliwaeleza
wakazi wa Mtwara kuwa wamefungwa na minyororo ya umaskini na kwamba
minyororo hiyo ni mibaya kwa mustakabali wa maisha yao kuliko hata
minyororo ya chuma waliyokuwa wakifungwa watumwa enzi za ukoloni
Millya: CCM imeshaanza kuaga
Kwa
Upande wake aliyekuwa Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha James Millya
alisema harakati zilizoanzishwa na CCM hivi karibuni kutaka nafasi ya
mgombea urais ihojiwe mahakamani ni baada ya kugundua mwaka 2015
hawatakuwa na nafasi ya kushinda hivyo kimbilio lao ni mahakamani.
“CCM
wanatuaga na mkitaka kuamini hilo sasa wameanza kutaka nafasi ya urais
ihojiwe mahakamni kwa kuwa huko ndiko kimbilio lao lililobaki kwa
sasa,” alisema Millya.
Alisema
CCM inaichukia CHADEMA kwa kuwa inataka uhakika wa maisha hata kwa
mtoto wa maskini ambaye hajui hatma yake ya maisha kwa siku zijazo.
Aliongeza
kuwa ni wakati muafaka sasa kwa Watanzania kuachana na watu
waliowasaliti kwa kushindwa kusimamia wajibu waliokabidhiwa.
Habari na Tanzania Daima, Mei 29. 2012
Comments
Post a Comment