IGP Mwema afanya mabadiliko katika safu ya Jeshi la Polisi Tanzania
Mkuu
wa Jeshi la Polisi nchini, (IGP), Saidi Mwema amefanya mabadiliko
katika jeshi hilo kwa kuwahamisha makamanda wa polisi wa mikoa kadhaa,
kuwateua makamanda mapya na wakuu wa vitengo ndani ya jeshi hilo.
Msemaji Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Advera Senso alisema jana kuwa mabadiliko hayo ni ya kawaida katika kuimarisha utendaji ndani ya jeshi hilo, pia kutekeleza maboresho (reforms) yanayoendelea kufanywa.
ASP Senso alisema miongoni mwa maboresho hayo ni kuundwa kwa vikosi vitatu maalum vitatu vipya vya polisi ambavyo ni Mazingira (Enviromental Police Unit), Utalii (Tourism Police Unit) na Migodi ya Madini (Mining Police Unit).
Alisema katika mabadiliko hayo, aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC) wa Arusha, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP), Thobias Andengenye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Utawala na Rasilimali, Polisi Makao Makuu na nafasi yake inachukuliwa na aliyekuwa RPC Manyara, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Liberatus Sabas.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, SACP Adolfina Chialo amehamishiwa Makao Makuu ya Upelelezi (CID – HQ) na nafasi yake inachukuliwa na aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ilala, ACP Fautine Shilogile.
Mabadiliko mengine yamewagusa RPC Kilimanjaro, SACP Absalom Mwakyoma ambaye amehamishiwa mkoani Mara akibadilishana na RPC Mara, ACP Robert Boaz ambaye amehamishiwa mkoa wa Kilimanjaro.
Senso alisema RPC Ruvuma, SACP Michael Kamuhanda amehamishiwa mkoani Iringa kuchukua nafasi ya ACP Evarist Mangala ambaye amehamishiwa mkoa wa Shinyanga, wakati aliyekuwa kamanda wa Shinyanga, ACP Diwani Athumani amehamishiwa mkoani Mbeya kuendelea na wadhifa wake huo.
Aliyekuwa RPC Mbeya, ACP Advocate Nyombi amehamishiwa Ofisi ya Upelelezi Makao Makuu katika kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini huku aliyekuwa Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), Kanda Maalum ya Dar es Salaam, ACP Ferdinand Mtui akiteuliwa kuwa mkuu wa kikosi hicho nchini, kuchukua nafasi ya SACP Anaclet Malindisa ambaye anastaafu.
Makamanda wa Polisi wapya wa mikoa walioteuliwa na mikoa yao kwenye mabano ni aliyekuwa Ofisa Mnadhimu mkoani Arusha, ACP Akili Mpwapwa (RPC Manyara), aliyekuwa Ofisa wa Opareshini Mwanza, ACP Philipo Kalangi (RPC Kagera) aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (RCO) Arusha, ACP Leonard Paul (RPC Geita) na aliyekuwa Ofisa Mnadhimu mkoa wa Dodoma, ACP Furgence Ngonyani (RPC Njombe).
Wengine ni Ofisa wa Oparesheni Kanda Maalum ya Dar es Salaam, ACP Marieta Minangi (RPC Ilala), ACP George Mwakajinga aliyekuwa Ofisa Mnadhimu Lindi anakuwa RPC Lindi, ACP Linus Sinzimwa kutoka CID Makao Makuu anakuwa RPC Singida na ACP Salum Msangi pia kutoka CID Makao Makuu anakuwa RPC Simiyu.
Senso alisema Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Kimataifa Makao Makuu ACP Dhahir Kidavashari anakuwa RPC Katavi, RCO Mwanza, ACP Deusdedith Nsimike anakuwa RPC Ruvuma, ACP Saada Juma Haji ambaye ni Ofisa Mnadhimu Ilala anakuwa Kamanda wa Kikosi cha Reli Dar es Salaamn na Mkuu wa Usalama Barabarani mkoa wa Arusha, ACP Amir Konja anahamia Dar es Salaam kuendelea na kazi hiyo.
Walioteuliwa kuwa wakuu wa vikosi vipya ni ACP George Mayunga kutoka CID Makao Makuu anayekuwa mkuu wa Kikosi cha Ulinzi wa Mazingira, kikosi cha Ulinzi wa Watalii kitaongozwa na ACP Benedict Kitarika kutoka Kitengo cha Sheria na Utafiti Makao Makuu na ACP Deusdedith Katto kutoka Oparesheni Makao Makuu ataongoza Kikosi cha Ulinzi wa Migodi ya Madini.
Senso alisema mabadiliko hayo pia yamevigusa vyuo vya polisi ambapo aliyekuwa Mkuu wa Chuo cha Dar es Salaam, SACP Elice Mapunda ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mafunzo Polisi Makao Makuu na nafasi yake kuchukukiwa na Mkuu wa Chuo cha Kidatu, ACP Ally Lugengo.
Mkuu wa Mafunzo katika Chuo cha Polisi Moshi, ACP Nasser Mwakambonja amehamishiwa Kidatu ambako anakwenda kuwa Mkuu wa Chuo hicho wakati aliyekuwa Mkuu wa Mafunzo SACP Abdulrahman Kaniki ameteuliwa kuwa Mkuu wa Kitengo cha Sheria na Utafiti cha Jeshi hilo.
Senso alisema maofisa wanaotarajiwa kustaafu utumishi wao ni Mkuu wa Mafunzo wa Kitengo cha Sheria na Utafiti, SACP Donald Kaswende na baadhi ya makamanda wa polisi wa mikoa.
Makamanda hao na mikoa yao kwenye mabano ni SACP Henry Salewi (Kagera), ACP Sifueli Shirima (Lindi) SACP Celina Kaluba (Singida) na Mkuu wa Usalama Barabarani Kada Maalum ya Dar es Salaam, ACP Vitus Nikata.
Chanzo cha taarifa: Jeshi la Polisi via blogu ya Lukwangule Ent.
Comments
Post a Comment