MADIWANI CHADEMA MWANZA WAGOMEA BAJETI YAO

Leo katika halmashuri ya jiji la Mwanza madiwani wa Chadema ambao ndiyo wanaunda Halmashauri ya Jiji la Mwanza, wamegoma kupitisha bajeti yao na kuzua mvutano huku wakiandikisha kupiga kura ya kutokuwa na imani na Meya Josephati Manyerere.

Madiwani 17 kati ya 29 wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kutoka vyama vya Chadema, CCM na CUF wamesaini pendekezo la kutaka kumng'oa Meya wa Jiji hilo, Josephat Manyerere (Chadema) kwa madai ya kushindwa kuongoza Halmashauri hiyo.


Uamuzi huo ulifikiwa baada ya kuvurugika kwa kikao cha kupitisha Mpango wa Bajeti wa Halmashauri ya Jiji kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji baada ya mvutano uliodumu takribani saa tatu.


Madiwani hao wakiongozwa na Diwani wa Igoma, Adamu Chagulani (Chadema) wamesema wameamua kupiga kura ya kutokuwa na imani na Meya huyo kutokana na sababu mbalimbali. Chagulani alisema kuwa Manyerere, ameshindwa kusimamia Halmashauri na vikao kutoitishwa kwa wakati kutokana na kutoa maelekezo kuwa hakuna kikao kufanyika bila yeye kuwapo pia ameshindwa kuunganisha madiwani, hali ambayo imesababisha kuzorota kwa uhusiano baina ya madiwani na watendaji..


Sababu nyingine ni pamoja na kusaini mikataba kabla ya kupitishwa na Baraza la Madiwani, kukataa kusaini mikataba halali ambayo imepitishwa na Halmashauri ya Jiji, kupendelea kata yake katika miradi na kutumia madaraka yake vibaya.


Diwani wa Mkolani, Stanslaus Mabula (CCM) amemtuhumu Meya huyo kwa kutoa makabrasha ya rasimu ya Bajeti ya Jiji kwa watu wasiohusika katika kikao kisicho rasmi hivi karibuni.


Kwa upande wake Meya Manyerere amesema yuko tayari kuondolewa ikithibitika amevunja sheria na kanuni za kudumu za Halmashauri. Kabla ya uamuzi wa kumwondoa Meya, madiwani hao walikuwa katika malumbano na Meya huyo bila kujali itikadi za vyama kutokana na walichodai amekuwa akiwaburuza kwa kuahirisha kinyemela kikao cha Baraza kwa hofu ya kupigiwa kura hiyo.


source:gsengo.blogspot.com 

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA