UZINDUZI WA KITABU CHA KEMIA CHA KISWAHILI WAFANYIKA


 

 Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Bi. Elizabeth Missokia (aliyesimama katikati) akizungumza katika uzinduzi wa kitabu cha Kemia 'Furahiya Kemia' kilichochapishwa kwa Kiswahili.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Mkuki na Nyota Publishers, Walter Bgoya (kulia) akimshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Bi. Elizabeth Missokia mara baada ya kuzindua  kitabu cha Kemia 'Furahiya Kemia' kilichochapishwa kwa Kiswahili.
 Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Bi. Elizabeth Missokia (kushoto) akipokea zawadi ya shukrani kutoka Mkuki na Nyota Publishers.
 Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Bi. Elizabeth Missokia akikabidhi baadhi ya vitabu kwa wanafunzi
 Baadhi ya maofisa kutoka kitengo cha Habari HakiElimu wakifuatilia mazungumzo mbalimbali katika uzinduzi huo.
--


KAMPUNI ya Uchapishaji wa Vitabu na machapisho anuai kwa mara ya kwanza imezindua kitabu cha somo la Kemia kilichochapishwa kwa lugha nyepesi ya kiswahili. Kitabu hicho kilichopewa jina la Furahiya Kemia (Enjoy Chemistry) kilichochapishwa kwa ushirikiano na Taasisi ya HakiElimu kimezinduliwa Mei 9, 2012 na Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Bi. Elizabeth Missokia.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Bi. Missokia alisema kuzinduliwa kwa kitabu hicho kutaleta chachu ya wanafunzi kupenda masomo ya sayansi hasa Kemia ambayo yamekuwa yakiwatatiza wanafunzi wengi kutokana na lugha ya kigeni inayotumiwa.

Alisema ndani ya kitabu hicho wanafunzi wataweza kusoma na kuelewa vizuri somo la Kemia kwa lugha nyepesi ya Kiswahili jambo ambalo linaibua morali ya wanafunzi kuona masomo ya sayansi ni ya kawaida kujifunza kama yalivyo masomo mengine.

Awali akizungumza kabla ya uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mkuki na Nyota Publishers, Walter Bgoya alisema kitabu hicho kimechapishwa kwa lugha mbili yaani Kiswahili na Kiingereza ili kuwarahisishia wanafunzi kujifunza sayansi ya Kemia kwa lugha mama ya Kiswahili.

Aidha alisema kitabu hicho kimepitiwa na kukubaliwa na Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) kwamba kinaweza kutumika kutokana na kuwa na maneno rahisi na sahihi ya Kiswahili ambayo yatawarahisishia wakati wa kujifunza mada anuai za Kemia hasa kidato cha kwanza.

Pamoja na hayo, Bgoya aliishukuru taasisi ya HakiElimu kwa kusaidia kuchapishwa kwa kitabu hicho na kuwataka wadau wengine waungane na juhudi hizo za kuinua lugha ya Kiswahili katika matumizi ya kufundishia hata masomo ya sayansi.

Naye akitoa maoni yake juu ya kitabu cha Furahiya Kemia mmoja wa walimu wa Sayansi, John Bosco alisema kitabu hicho kitakuwa daraja litakalo wawezesha wanafunzi kuvuka na kuyapenda masomo ya sayansi hasa kemia. Alisema kitabu hicho kina mazoezi ya kutosha kiasi cha kumfanya mwanafunzi apende kujifunza kwa dhati.

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA