HII NDO HALI HALISI YA "SAJUKI" KAMA ILIVYORIPOTIWA NA GAZETI LA IJUMAA
OOH SAJUKI! Siku mbili kabla ya kwenda katika Hospitali ya Apollo nchini India kwa matibabu, afya ya stadi wa filamu za Kibongo, Sadick Juma Kilowoko ‘Sajuki’ ni ya kusikitisha kupitiliza.
Kadiri siku zinavyosonga, hali ya Sajuki inazidi kuwatoa watu machozi baada ya kuzidiwa na kushindwa kunyanyuka kitandani. Laiti kama utamuona na ukashindwa kububujikwa na machozi basi utakuwa huna utu.
ASHINDWA KUPOKEA MCHANGO
Tukio bichi kabisa lililowatoa machozi wasanii wenzake ni lile la Jumanne wiki hii nyumbani kwake Tabata Barakuda, Dar es Salaam ambapo msanii na prodyuza huyo wa filamu alishindwa kuamka kitandani kupokea dola elfu kumi (takribani Sh. milioni 15) alizozitoa mwigizaji mwenzake, Jacqueline Wolper kwa ajili ya matibabu huku akisindikizwa na mastaa wengine wa Bongo Movie.
The Udaku Master, Ijumaa lilimshuhudia Sajuki akiugulia maumivu huku akilalamika kujisikia vibaya, hivyo kuwaomba wasanii wenzake kwa heshima waingie chumbani kwake ili apokee fedha hizo.
WASANII VILIO
Kitendo hicho ndicho kilichowafanya baadhi ya wasanii wenzake kushindwa kujizuia na kujikuta wakiangua vilio huku Sajuki akiwatuliza na kuwaomba wasilie wala wasihuzunike kwani kila kitu ni mapenzi ya Mungu.
“Msihuzunike ndugu zangu, naamini kila kitu ni mapenzi ya Mungu na si vinginevyo, jipeni moyo,” alisema Sajuki kwa tabu akiwa amelala kitandani akiwa amezungukwa na mastaa hao.
WOLPER
Kwa upande wake Wolper aliyekuwa akimwaga machozi mithili ya bomba la mvua, alisema kuwa siyo kwamba ana fedha nyingi, ila ni namna alivyoguswa na mateso ya Sajuki.
“Siyo kwamba sina shida bali ni moyo wa kusaidia kuokoa uhai wa mwenzetu. Tulizoea kuwa naye location (sehemu ya kurekodia filamu) na kwenye tasnia yetu, anaumwa na hajiwezi, niliumia sana,” alisema Wolper aliyekuwa akifutwa machozi na wenzake.
WASTARA
Naye mke wa Sajuki, Wastara Juma, huku akilia muda wote, alitoa shukurani zake za dhati kwa Wolper na kueleza jinsi alivyoguswa na kuona umuhimu wa kumsaidia mumewe.
MASTAA
Baadhi ya mastaa wa Bongo Movie walioambatana na Wolper kuwasilisha mchango huo ni pamoja na Jacob Steven ‘JB’, Muhsein Awadhi ‘Dk. Cheni’, Chiki Mchoma ‘Chiki’, Hartmann Mbilinyi, Sabrina Rupia ‘Cathy’ na wengine.
TUMEFIKAJE HAPA?
Oktoba, 2011, magazeti ya Global Publishers yalikuwa ya kwanza kuripoti habari ya Sajuki kuwa hoi kitandani akipatiwa matibabu katika Hospitali ya TMJ, Dar.
Katika mahojiano yake, Sajuki aliyaambia magazeti ya Global: “Madaktari walibaini nina uvimbe pembeni ya ini. Ni tatizo ambalo limekuwa likinisumbua kwa muda mrefu.
“Kwa siku za hivi karibuni nimekuwa siwezi kuamka kitandani kwani napata maumivu makali kupita maelezo, hivyo nasubiri kufanyiwa upasuaji katika Hospitali ya TMJ.”
HISTORIA UGONJWA WA SAJUKI
Taarifa za awali kabla ya Sajuki kuthibitisha ilielezwa kuwa alianza kwa kupata uvimbe sehemu tofauti katika mkono wake mmoja lakini baadaye tatizo hilo lilihamia ndani na kuanza kupata maumivu makali pembeni ya ini.
UNDANI WA UGONJWA
Kwa mujibu wa daktari aliyezungumza na Ijumaa (jina linahifadhiwa kwa sababu maalum), uvimbe pembeni ya ini ni dalili za ugonjwa alioutaja kitaalamu kama Hepatoma.
HEPATOMA NI NINI?
Daktari huyo alieleza kuwa Hepatoma ni moja ya kansa za ini ambayo huanzia kwenye sehemu ya juu kulia ya ini.
CHANZO
Ilifahamika kuwa chanzo cha Hepatoma ni magonjwa yanayoshambulia ini kwa pamoja, kitaalamu huitwa Hepatitis. Mbali na magonjwa hayo shambulizi, pia watu wanaotumia pombe, madawa ya kulevya wapo hatarini zaidi kupatwa na ugonjwa huo.
DALILI
Dalili za Hepatoma ni pamoja na maumivu makali sehemu ya juu ya kulia ya ini, kupoteza hamu ya kula, kukosa usingizi, kukondeana na kukosa furaha, yaani mtu wa ‘stresi’ muda mwingi.
MATIBABU
Mara nyingi njia ya upasuaji huwa chaguo la kwanza ili kuundoa uvimbe, dozi maalumu ya kutibu uvimbe huo na dawa za kutuliza maumivu.
KILA LA HERI SAJUKI
Tunawatakia Sajuki na Wastara safari njema ya matibabu nchini India watakapoondoka Jumapili ijayo.
Tunaamini watarejea na matumaini tele kwani tunawasubiri kuwaona runingani wakituburudisha tunapokuwa sebuleni kwetu.
Mbali na dua za Watanzania kwa namna kila mtu anavyoguswa, tunaomba tuendelee kumchangia fedha kupitia simu ya mkononi kwa kutuma kwenye Tigo Pesa namba 0713 666 113 au kwenye akaunti namba 050000003047 katika Benki ya Akiba Commercial yenye jina la Wastara Juma Issa-Mhariri.
SOURCE: GAZETI LA IJUMAA
Comments
Post a Comment