Waziri Akumbana Na Madudu Maliasili
WAZIRI
mpya wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, ameelezea
kushtushwa kwake na ubadhilifu wa kutisha ulioko katika wizara hiyo,
Idara ya Wanyamapori unaodaiwa kufanywa na baadhi ya watendaji wake.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuzindua Bodi ya
Ushauri ya Wizara ya Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) jijini Dar es
Salaam, jana, waziri huyo alisema idara hiyo inanuka kwa uozo
unaotokana na wizi na ubadhilifu mkubwa ambao umeleta hasara kwa taifa.
Kagasheki alidai idara hiyo inaongoza kwa madudu ya kutisha, na
ametangaza kuchukua hatua za haraka dhidi ya watendaji wanaotuhumiwa
kuhusika na ubadhilifu huo mkubwa haraka iwezekanavyo, akidai fedha
zilizotafunwa na wajanja hao ni nyingi.
“Jamani Idara ya Wanyamapori ina fedha nyingi, lakini zinaliwa na
watu kwa maslahi binafsi, na kama fedha hizo zingekuwa zinapelekwa
serikalini kama inavyohitajika, nchi hii kwa sasa ingefika mbali, mimi
naogopa hata kutaja kiasi cha fedha hapa hadharani,” alisema.
Mbali na ufujaji huo, Balozi Kagasheki amekiri kuwa, usafirishaji
wanyamapori nje ni mkubwa mno licha ya serikali kusitisha biashara hiyo.
Alisema uchunguzi wa haraka umebaini kuwa, biashara ya kusafirisha
wanyama pori inafanywa kati ya wafanyabiashara wa ndani na baadhi ya
watendaji, ambao hawajali na wanaonekana kutumia kila mbinu
kuifanikisha.
Hata hivyo, katika hali iliyotarajiwa, Balozi Kagasheki alionesha
hofu yake ya kukabiliana na wafanyabiashara na baadhi ya maafisa wa
wizara hiyo, kiasi cha kuomba msaada kutoka taasisi nyingine, vikiwemo
vyombo vya habari kusaidia kupambana na ‘genge’ la wabadhilifu hao.
“Katika idara kunahitaji usaidizi maana hapa ni vita, na hata ninyi
waandishi nafikiri mnaweza tukasaidiana kwa kuwa najua mtakuwa
mnawajua sana wafujaji. Kuwaondoa hawa ni kutangaza vita,” alisema.
Comments
Post a Comment