HUDUMA YA USAFIRI KWENDA KIGOMA KUANZA TENA DAR ES SALAAM KUANZIA JUMANNE IJAYO!


Uongozi wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) unafuraha kuwatangazia  kuwa huduma za safari za abiria kwenda  Kigoma zitaanzia tena Dar es Salaam  hapo Jumanne  Mei 22, 2012  badala  ya  Dodoma.
 
Itakumbukwa kuanzia Januari 24, 2012 huduma za usafiri wa abiria ilibidi zihamishiwe Dodoma baada ya eneo kati  ya Stesheni za Godegode na Gulwe  za reli ya kati ( mkoani Dodoma)  kukumbwa  na mafuriko makubwa. Hata hivyo mamlaka iliyokuwa inafanya ukarabati sehemu hiyo imeithibitishia  TRL kuwa eneo hilo sasa liko imara kwa safari za treni za abiria.

Kwa mujibu taarifa rasmi za TRL  kuanzia Jumanne ijayo usafiri  wa abiria utakuwa mara mbili kwa wiki na utakuwa katika siku za Jumanne na Ijumaa kutoka Dar es Salaam  kwenda Kigoma  ambapo treni zitaondoka saa 11 jioni. Aidha kutoka Kigoma kuja Dar safari zitakuwa kwa siku za Alhamis na Jumapili  treni itaondoka Stesheni ya Kigoma saa 12 jioni.

Taarifa imefafanua kuwa hakuna mabadiliko kwa safari ya treni ya abiria iliyopangwa kuondoka siku ya Jumapili  Mei 20, 2012 kutoka Dodoma kwenda Kigoma saa 1 usiku, isipokuwa wakati wa kurejea itasafiri moja kwa moja hadi Dar es Salaam ili kukidhi matakwa ya ratiba mpya inayoanza  Jumanne Mei 22 na Ijumaa Mei 25, 2012.

Halikadhalika Uongozi unawahimiza wananchi wanaotaka kusafiri kuanzia Dar es Salaam kwenda Kigoma wafike katika Stesheni zilizo karibu nao kwa kupata maelezo ya safari  husika na kukata tiketi wanazohitaji.

Imetolewa na Ofisi ya Uhusiano kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji  Mhandisi K.A.M Kisamfu
Imesainiwa na:

MIDLADJY MAEZ
MENEJA UHUSIANO- TRL
MEI 16, 2012

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA