HOTUBA YA NAIBU KATIBU MKUU CHADEMA,MH.ZITTO KABWE KWA WANA-CHADEMA NA WATANZANIA NCHINI MAREKANI
Tumekutana leo wakati ambao Taifa letu lipo katika mpito wa mambo mengi sana.
Kufuatia
shinikizo kubwa kutoka chama chetu cha CHADEMA na asasi nyingine za
kiraia ikiwemo viongozi wa dini, tupo katika mchakato wa kuandika upya
katiba ya nchi yetu. Lakini pia kuna muamko mkubwa sana wa haki za
kiraia na haki za kisiasa katika Taifa letu hivi sasa. Watanzania,
kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya nchi yetu, wameamka na
kutaka mabadiliko ya kisiasa na hasa kutaka kabisa uongozi mpya wa nchi
kutoka chama kingine tofauti na chama kinachoongoza hivi sasa. Huu
mpito pia, Mpito wa kutoka chama kimoja hodhi kwenda mfumo wa kweli wa
vyama vingi vya siasa. Watanzania wameamka sana kujua rasilimali za
nchi yao na kutaka kutokomeza rushwa na ufisadi na matumizi mabaya ya
utajiri wa nchi. Huu ni mpito wa kutoka viongozi wanaojali maslahi yao
binafsi na kwenda kwa viongozi wawajibikaji na wenye uchungu wa
kuendeleza nchi yetu na watu wake.
Mpito
wowote unapaswa kuongozwa vyema. Unapaswa kushirikisha wananchi wote
bila kujali wapo sehemu gani ya Dunia. Chama chetu kipo mstari wa mbele
kuongoza mpito tulionao Tanzania. Licha ya kuongoza juhudi za kuwa na
Katiba mpya itakayohakikisha HAKI na Wajibu wa Watanzania, lakini pia
tumekuwa tukiendelea kupambana na rushwa na ufisadi. Pia tumekuwa
tukiendelea kuhakikisha utajiri wa nchi yetu unatumika kwa manufaa ya
Watanzania. Hatujatetereka hata kidogo na hatutateterekea kuhakikisha
Watanzania wanakuwa na Taifa lenye demokrasia iliyokomaa, lenye
maendeleo na ustawi wa watu wake (Developmental Democratic State).
Licha
ya kwamba tupo Upinzani, lakini hatua mbalimbali tulizochukua zimeleta
mabadiliko makubwa katika nchi yetu. Kuanzia vuguvugu la Buzwagi mpaka
kuibuliwa kwa maskandali ya EPA na mpaka kutajwa kwa orodha ya Mafisadi
nchini pale MwembeYanga. Hata hivi karibuni juhudi za Bunge kutaka
Uwajibikaji Serikalini zilizoongozwa na CHADEMA zimeleta mabadiliko.
Inawezekana mabadiliko hayo sio kama tutakavyo, sio kamili, lakini ni
hatua ambayo tumepiga. Tutaendelea kama chama cha siasa sio tu kusema
na kupiga kelele kuhusu uoza uanaofanyika Serikalini (maana ndio kazi
yetu kikanuni) lakini pia kutoa masuluhisho ya matatizo ya nchi yetu na
kusukuma kupitia Bunge mabadiliko chanya yanayotakiwa ili kuleta
mabadiliko nchini.
Ni
matumaini yangu kwamba Watanzania wanaoishi nje ya nchi, kokote walipo
watashiriki pamoja nasi katika vuguvugu (movement) hili la kuleta
mabadiliko katika Taifa letu. Hampaswi kukaa na kutazama, bali mnapaswa
kushiriki kikamilifu maana hii ni nchi yetu sote. Ni wajibu wa kila
mmoja wetu kuhakikisha nchi yetu inakuwa na demokrasia na ustawi wa
watu wake.
Hali ya Uchumi wa Nchi
Tumekuwa
moja ya nchi ambazo uchumi wake unakua kwa kasi zaidi duniani. Katika
kipindi cha muongo mmoja uliopita uchumi wa Tanzania umekuwa ukikua kwa
wastani wa asilimia 6. Kazi hii ya ukuaji ukilinganisha na kiwango cha
ukuaji wa idadi ya watu (ambacho ni 2.8%) ingeweza kupunguza umasikini
kwa zaidi ya 50% katika kipindi hicho. Hata hivyo Umasikini Tanzania
umebakia ni mkubwa ambapo zaidi ya Watanzania 37 katika kila Watanzania
100 hawana uhakika wa mlo mmoja kwa siku.
Idadi
ya Watanzania masikini wa kutupwa (wenye kipato cha chini ya tshs 500
kwa siku) imeongezeka kutoka watu milioni 12 mwaka 2007 mpaka watu
milioni 15 mwaka 2011. Ukitaka kujua wingi huu ni wa kiwango gani,
chukua idadi ya watu wa Nchi ya Botwasana, Namibia, Swaziland na
Lesotho haikaribii idadi ya Watanzania wenye mashaka ya mlo mmoja kwa
siku. Idadi ya watu wa Denmark, Netherlands, Norway na Uholanzi kwa
pamoja ndio sawa na idadi ya Watanzania masikini. Kwa nini?
Ni kitendawili. Ni nadra kukuta uchumi unaokua kwa kasi kama wetu ukizalisha masikini zaidi. It’s a paradox of a fast growing economy and increasing poverty.
Kwa miaka kumi ambayo tumeiangalia (2000 – 2010) tumeshuhudia kwa
dhahiri kabisa kushindwa kwa sera za kuondoa umasikini zinazotekelezwa
na Serikali ya CCM.
Masikini
wa Tanzania wapo vijijini zaidi. Uchumi wa vijijini kwa kipindi cha
muongo mmoja umekua kwa wastani wa asilimia moja tu. Flat lining.
Kwa hiyo uchumi unaokua hivi sasa sio uchumi wa Watanzania bali ni
uchumi wa watu wachache kwenye sekta chache kama madini, mawasiliano na
ujenzi. Watanzania walio wengi walioko vijijini wanaendelea kuandamwa
na ufukara bila juhudi mahususi za kuwasaidia. Tumesema na tunarudia
kusema kwamba ni lazima kubadili mwelekeo wa mipango yetu na kujikita
kwenye maendeleo vijijini. Kama chama tunaendelea kusema jambo hili
ndani ya Bunge na pia kuwaelimisha wananchi kwenye mikutano yetu ya
hadhara.
Mfumuko
wa Bei umefikia kiwango cha juu sana cha 19% na hivyo hata mikopo
katika mabenki imekuwa ghali hadi kufikia riba ya 23% na zaidi. Mfumuko
wa bei unaongozwa na bei ya vyakula. Katika hali ya kawaida, kupanda
kwa bei za vyakula kungemnufaisha mkulima lakini hali sio hiyo
Tanzania. Mkulima bado anauza mazao yake kwa bei za vijijini ambazo ni
ndogo na zinaamuliwa na wachuuzi wa mijini. Lakini mkulima huyu
anaponunua bidhaa za matumizi yake kama sukari, mafuta ya taa, nguo nk
ananunua kwa bei za mijini ambazo zimeathiriwa vikali na mfumuko wa
bei.
Hivyo
mfumuko wa Bei unamuathiri zaidi mwananchi masikini kabisa. Serikali
imekuwa mlalamikaji kama wananchi wengine. Mfumuko wa Bei utapungua kwa
kuongeza uzalishaji wa chakula, kuimarisha miundombinu ya vijijini na
kupunguza gharama za Nishati kama hasa Umeme. CHADEMA inaendelea
kuisukuma Serikali kuchukua hatua ili kupunguza makali ya maisha kwa
wananchi. Hatua za muda mfupi zihusishe nafuu ya kodi kwenye bidhaa
zinazotumiwa na wananchi kwa wingi.
Hata
hivyo bado matumizi ya Serikali ni makubwa mno kwenye masuala ambayo
hayana uhusiano na kuendeleza watu. Bado bajeti ya posho mbalimbali,
safari za nje na hata matumizi makubwa ya magari ya serikali ni kubwa
mno kulinganisha na hali yetu ilivyo. Katika matumizi haya pia kuna
ufisadi mkubwa sana. CHADEMA inaendelea kuanisha masuala haya na
kukemea na kuchukua hatua pale inapobidi.
Uwezo wetu wa kukusanya mapato ni changamoto kubwa.
Mapato
mengi yanapotea kama misamaha ya kodi ambayo sasa imefikia tshs 1.3trn
kwa mwaka. Mapato mengine hayakusanywi kwa sababu ya ukwepaji kodi
uliokithiri. Kodi kwenye Sekta ya Madini imekuwa ni mjadala wa muda
mrefu sana. Sheria ya madini ya mwaka 1998 na Sheria za Fedha ya mwaka
1997 ziliweka mfumo wa kinyonyaji kabisa ambao ulikuwa unafaidisha
makampuni ya uchimbaji madini kuliko Taifa. Sheria mpya ya madini ya
mwaka 2010 ambayo ilitokana na kazi kubwa tuliyofanya ndani ya Bunge
pamoja na Mashirika yasiyo ya kiserikali imeweka mfumo bora zaidi.
Hata
hivyo makampuni ya Madini yaliweka mgomo kwenye sheria mpya kwa kukataa
kuanzisha miradi mipya na hata kukataa kuhamia kwenye sharia mpya.
Sheria mpya inataka Serikali kuwa na hisa kwenye kila mgodi, hisa za
kampuni za madini kuorodheshwa katika Soko la hisa la Dar es Salaam na
kulipwa kwa mrahaba mpya wa asilimia 4 kwa kanuni mpya ya kukokotoa
mrahaba (from Netback Value to Gross value) ambayo ingeongeza mapato ya
Serikali maradufu. Kwa miaka Serikali imekuwa inapoteza mapato kwa
kutotekelezwa kwa sharia mpya. Nimesikia kuanzia mwezi huu kampuni ya
Barrick imeanza kulipa mrahaba mpya. Tutataka maelezo ya Serikali
kuhusu kampuni nyingine na pia mrahaba wa miaka ya nyuma. Ni lazima
Serikali ihakikishe nchi inafaidika na rasilimali zake.
Tunaenda
kwenye Uchumi wa Gesi Asilia. Makampuni mawili makubwa duniani
yamegundua Gesi Asilia nchini kwa kiwango kikubwa sana. Hivi sasa
Tanzania ina Utajiri wa Gesi ulitothibitishwa wa 20TCF na makadirio
yanaonyesha kuwa tutafika 85TCF katika kipindi kifupi sana. Bado kuna
meneo yanaendelea kufanyiwa utafutaji kutokanana vitalu vilivyogawiwa.
Hata hivyo hatuna Sera na Sheria ya kusimamia vema sekta hii na hasa
yenye kuhakikisha Uwazi na Uwajibikaji. Hatuna pia Sheria ya kusimamia
mapato yanayotokana na Gesi Asilia (Petroleum Revenue Management Act).
Hatutaki kurudia makosa yaliyofanyika kwenye sekta ya Madini. Tunataka
Gesi Asilia itumike kwa maendeleo ya watu wetu.
Tumependekeza
kwamba Vitalu vipya vya kutafuta mafuta visitolewe kwa sasa
(moratorium) mpaka hapo Sera mpya, Sheria mpya na mfumo bora wa
matumizi ya Fedha zitakazotokana na Mafuta na Gesi ziwepo. Pia shughuli
za utafutaji katika vitalu vya sasa zitaongeza thamani ya vitalu
vijavyo na hivyo nchi kufaidika zaidi.
Tumependekeza
pia kwamba ni lazima kuweka mfumo mzima wa uwazi na uwajibikaji katika
sekta ili kujipanga vyema na kuepuka yaliyowakuta wenzetu wenye utajiri
kama huu ambao uligeuka balaa. Tatu tumependekeza kusomesha Watanzania
kwa ngazi zote. Mafundi mchundo kupitia VETA na Mafundi wa kati kupitia
Vyuo vya Ufundi.
Muhimu
zaidi tunataka kijengwe Chuo Kikuu kikubwa Mtwara chenye Kampasi Lindi
ambacho kitakuwa ni kituo cha kufundisha sio watanzania tu bali
Waafrika wengine kuhusiana na masuala haya. Ujenzi wa Chuo Kikuu Mtwara
unapaswa kuanza mara moja bila kuchelewa.
Kutokana
na uzoefu tuliupata katika sekta ya Madini na kupitisha sharia mbaya
Bungeni, tunaona kwamba suala la Gesi tukabe kila mahala ili
kuhakikisha nchi inafaidika.
Historia
inatuonyesha kwamba Nchi nyingi za Kiafrika zenye utajiri wa Gesi na
Mafuta hazina demokrasia, zimegubikwa na uvundo wa ufisadi na watu wake
ni masikini. Tunataka kuonyesha Dunia kwamba inawezekana kuwa nan chi
ya Kiafrika yenye utajiri mkubwa wa Mafuta na Gesi na ikawa ya
kidemokrasia, isiyo na ufisadi na yenye watu wenye ustawi.
Sio
kazi rahisi lakini tumedhamiria. CHADEMA haitakaa tu kuona utajiri wan
chi unatapanywa hovyo. Tumesema na kusimamia kwenye Madini, tunatoa
mwongozo kwenye Mafuta na Gesi.
Katiba
Ninajua
Watanzania mnaoishi nje mna shauku kubwa ya kujua ushiriki wenu na
hatma yenu kwenye Katiba mpya. Kwa muda mrefu mmekuwa mkishawishi haki
ya kupiga kura, haki ya kuwa na uraia zaidi ya mmoja (Dual Nationality)
na hata namna gani mnashiriki katika kujenga uchumi wa nchi.
Kwanza
nataka niwapongeze kwa kuchukua uamuzi mzito wa kuondoka nyumbani kuja
ughaibuni kutafuta maisha au maarifa au vinginevyo. Nawapongeza zaidi
kwa juhudi mnazofanya kusaidia familia zenu nyumbani, vijiji vyenu na
hata Taifa kwa ujumla. Takwimu zilizotangazwa na Benki Kuu ya Tanzania
zinaonyesha kwamba Watanzania mliopo nje ya Tanzania mlituma nyumbani
fedha (remittances) zaidi ya Dola za kimarekani 350 milioni mwaka 2011.
Hii ni sawa na asilimia 5 ya mapato yote ya Fedha za kigeni zilizoingia
Tanzania mwaka huo na ni zaidi ya Fedha za kigeni zilizoingizwa na
Chai, Kahawa, Pamba na Korosho kwa ujumla wake. Kwa hiyo ‘Diaspora’ ni
sehemu muhimu sana ya Uchumi wa Taifa ni muhimu Dola iwawekee mazingira
mazuri ya kuweza kufanikisha mambo yenu huku ili mshiriki vema
maendeleo ya nchi yetu.
CHADEMA
tunatambua umuhimu wenu hata kama msingekuwa mnatuma fedha nyumbani.
Ninyi ni Watanzania na ni jukumu la Dola ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kuwalinda popote mlipo duniani. Mtakumbuka mwanzo mwa miaka ya
2000 kulikuwa kuna ‘petition’ ya kudai Uraia wan chi mbili kwa
Watanzania. Dkt. Willibrod Slaa alikuwa ni mmoja wa Wabunge waliokuwa
wanauliza maswali Bungeni kuhusu jambo hilo. Wengi tuliweka sahihi
katika ‘petition’ ile ambayo ilianzishwa na Watanzania wanaoishi nje.
CHADEMA inaunga mkono haki ya Watanzania kuwa na uraia wa nchi
nyingine. CHADEMA inataka suala hili lifikie mwisho kwenye mjadala wa
Katiba. Kuna watu wanasema sio uzalendo Mtanzania kuchukua uraia wa
nchi nyingine. Ninasema sio uzalendo pia kuacha raia wako wanateseka
nchi nyingine kwa sababu tu wamechukua uraia wa huko au wanashindwa
kuchukua uraia wa huko. Sheri zetu za Uraia ni gandamizi hasa kwa
wanawake wa Tanzania. Tumepoteza dada zetu wengi sana na watoto wao
kwa sababu wakiolewa na wageni watoto wao hawana haki ya kuwa raia.
Wakinyanyaswa na wageni na kutaka kurudi nyumbani wao na watoto wao
wananyanyaswa pia kwao. Haikubaliki na tutakabili suala hili kwa nguvu
zetu zote. Tunataka Watanzania walioko nje wapate kila aina ya msaada
kutoka Dola yetu ili wafanikiwe.
CHADEMA
inataka pia Watanzania waliopo nje waruhusiwe kupiga kura nyakati za
uchaguzi. Ni suala la ushamba tu kuendelea kujadili jambo hili la uwazi
kabisa. Kuna teknolojia za kisasa kabisa kuhakikisha watu wanapiga kura
kokote walipo. Mwaka 2004 Chama rafiki cha CHADEMA kutokan Msumbiji
RENAMO kiliniteua kuwa wakala wa kura katika kituo cha Ubalozi wa
Tanzania Msumbiji uliopo Dar es Salaam. Raia wa Msumbiji wanaoishi
Tanzania wanapiga kura nje, seuze Tanzania? CHADEMA inawahakikishia
kulisimamia jambo hili.
Katika
mkutano wa Bajeti ujao Bajeti Kivuli itazungumzia namna ya kuimarisha
uwekezaji wa Watanzania wanaoishi nje katika uchumi wa nchi. Siku zote
tunazungumzia mitaji kutoka nje kwa maana ya ‘Foreign Direct
Investments’ peke yake na kwa kweli tunasahau kwamba kuna ‘Diaspora
Direct Investments’. Tumetoa vivutio vingi sana kwa Wawekezaji kutoka
nje. CHADEMA inakwenda kupendekeza kuwepo kwa vivutio vya kikodi na
kirasimu kwa Watanzania wanaoishi nje wanaotaka kuwekeza nyumbani.
Ninawashawishi muangalie namna ya kujikusanya na kuwa na ‘Investments
Funds’ ili kununua ‘equties’ kwenye miradi mbalimbali. Uwekezaji
Tanzania unalipa sana (Return on Investments goes up to 25%) kwenye
baadhi ya maeneo. Huduma katika sekta zinazoinukia kama Mafuta na Gesi
ni eneo ambalo mnapaswa kuliangalia tusiachie wageni tu. Mnakumbuka
wakati wa mwanzo wa Sekta ya Madini hata huduma za kufua nilikuwa
zinatolewa na kampuni kutoka Australia! Mtwara hakuna vyumba vya
kutosha vya mahoteli na hata nyumba za kupanga, angalieni maeneo haya
maana Mtwara is booming. Sisi kama wanasiasa jukumu letu ni kuwawekea
mazingira mazuri.
Ninyi
mnapaswa kuzileta hizo Dola kidogo mpatazo nyumbani na kuwekeza kwenye
maeneo yatakayozalisha ajira na hivyo kuondoa umasikini kwa ndugu zenu.
Ninaamini mtachukua changamoto hii na kuangalia namna ya kuitekeleza.
Wenzetu kutoka Ethiopia na Kenya wanafanya hivi.
Mjadala
wa Katiba pia na hatimaye Katiba mpya itaamua hatma ya Muungano wetu.
Muungano pekee katika Bara la Afrika ambao umedumu na umeonyesha nia
ya Mwafrika kukataa mipaka ya kikoloni. Kuna Watu wanaona Muungano huu
haina manufaa hivyo uvunjwe. Kuna watu wanaona ni bora kuurekebisha ili
uweze kufaidisha Jamhuri mbili zilizoungana. Mchakato wa Katiba mpya
kupitia Tume ya Katiba ambayo CHADEMA tumeshiriki, ni nafasi ya kuandaa
mustakabali wa Tanzania ijayo. Tanzania tunayoitaka kwa miaka mingine
hamsini, mia moja au hata alfu moja.
Watanzania
wawe huru kusema wanataka Muungano au hawautaki, wanataka Muungano wa
namna gani na wanataka Tanzania ya namna gani.
Ni
Haki ya Watanzania wanaoishi nje kutoa maoni yao kuhusu Katiba. CHADEMA
inakusudia kwanza kukusanya maoni ya wanachama wake walioko nje kuhusu
Katiba lakini pia kuitaka Tume ya Jaji Warioba kuja huku kukutana na
Watanzania na kupata maoni yao. Ni Haki yenu kutoa maoni na ninawaomba
mtumie haki yenu vizuri. Mtupe uzoefu wa nchi nyingine ambazo mmeishi
na kuweza kuona ni vipi tutaimarisha Dola imara ya Kidemokrasia yenye
kuleta ustawi wa watu wake.
Msimamo
wa CHADEMA ni Muungano wa Serikali Tatu. Hata hivyo katika mchakato
tulio nao sasa wanachama wa CHADEMA wana uhuru wa kutoa mawazo mapya na
kuboresha sera hii ya CHADEMA kuhusu Muungano. Muwe huru kabisa kutoa
maoni yenu.
Haki na Wajibu
Watanzania
mnaoishi nje mna haki na lazima Dola ilinde haki hizo lakini pia kama
Watanzania mna wajibu kwa nchi yenu. Ni wajibu wenu kushiriki
kikamilifu katika kuimarisha demokrasia nchini. Sisi wenzenu tumejitoa
muhanga katika eneo hili.
Tumejenga taasisi zinazoitwa vyama vya siasa kwa zaidi ya miaka ishirini sasa.
Hatuchoki
lakini tunahitaji ushiriki wenu. Jambo hili sio kwa wanachama wa
CHADEMA peke yake bali pia hata wanachama wa vyama vingine mnaoishi
hapa Marekani.
Hutakuwa
mwanachama bora wa CCM kwa kufanya kazi ya kuwachoma Watanzania wenzako
ambao ni wana mageuzi kwa viongozi kila wanapokuja kwenye ziara nje ya
nchi. Utakuwa mwanachama mzuri wa chama chako iwapo utawaambia viongozi
ukweli wa mambo na namna bora ya kuongoza nchi yetu.
Hamuitendei
haki Tanzania kwa kusemana, kusingiziana, kutetana na hata kugombana.
Wakati mwingine unapoona mijadala ya watu kwenye mitandao ya kijamii
unasinyaa. Unajiuliza sasa kama hawa ndio wapo kwenye mwanga sisi tulio
kwenye giza inakuwaje?
Fanya
kazi. Furahia maisha. Lakini kumbuka kuna nchi yenye barabara za
mashimo, yenye giza muda mwingi wa mwaka kuliko mwanga, yenye
umasikini, yenye viongozi wasiwajibika na wala rushwa. Ni nchi yako.
Usiseme hii ni kazi ya kina Zitto, Slaa, Mbowe, Nassari, Leticia na
Msigwa. Kila mtu ana wajibu wa kufanya kuisogeza mbele nchi yetu.
Timiza wajibu wako kwa namna unavyoona inafaa.
Nkrumah once said ‘organise, don’t agonise’ narudia hivyo kwa Watanzania mliopo Marekani. Organise for your motherland.
Tanzania yenye usawa wa fursa
Nimalizie
kwa stori yangu. Nilizaliwa katika umasikini wa kutisha kama Watanzania
wengi wa vijijini. Nimekwenda shuleni bila viatu na wakati mwingi tumbo
likiwa tupu ama nimekunywa uji wa unga wa Yanga uliotiwa chumvi.
Darasani nilikuwa ninasoma na watoto wa watu wote wenye mamlaka pale
mjini Kigoma. Wote tulikuwa tunafundishwa na Mwalimu huyo huyo na
tunakaa darasa hilo hilo, tunapata elimu hiyo hiyo. Leo mimi ni msomi
mwenye shahada ya Uzamili na Mbunge nawakilisha watu wa kwetu.
Wenzangu
wengi pia wanaendesha maisha yao na wengine wapo hapa Marekani
wakitafuta maisha. Leo mtoto wa masikini Tanzania hapati elimu
anayopata mtoto wa mwenye uwezo. Mtoto wa masikini hakutani na mtoto
wa mwenye uwezo. Wanasoma shule tofauti. Wanafundishwa na walimu
tofauti. Hawachezi pamoja. Wote wakimaliza kidato cha
Sita,
mtoto wa mwenye uwezo ana nafasi kubwa zaidi ya kupata mkopo kwenda
Chuo Kikuu kwa sababu amesoma shule bora zaidi hivyo anapata daraja
kubwa zaidi la kupewa mkopo na Bodi ya Mikopo.
Wakati
nasoma, kikwazo kilikuwa uwezo wako tu kichwani. Hivi sasa kikwazo ni
kipato pia. Tofauti ya kipato nchini ni kubwa lakini sisi wanasiasa
hatuioni. Wakati wenzetu wanajiandaa kufaidika na ‘demographic
dividend’ kwani watoto wao wanapata elimu bora, sisi hata hatujiandai
na ‘demographic Bomb’ litakaloletwa na kundi kubwa la vijana wasio na
elimu wala ujuzi.
Shiriki kurejesha Tanzania yenye kutoa fursa kwa kila raia bila kujali hali yake ya kipato.
Shirika kurejesha Tanzania yenye Usawa kwenye fursa na yenye demokrasia. Jiunge na CHADEMA tuendeleze mapambano.
Nawashukuru kwa kunisikiliza.
Zitto Kabwe, Mb
Naibu Katibu Mkuu CHADEMA
Naibu Katibu Mkuu CHADEMA
source www.freebongo.blogspot.com
Comments
Post a Comment