Tetesi: Ongezeko la mshahara kwa kati ya asilimia 20 hadi 33

Gazeti la Mwananchi linaripoti kuwepo kwa taarifa kwamba Serikali imekubali kuongeza mishahara kwa watumishi wa umma kwa kati ya asilimia 20 na 33.3 katika Bajeti ya mwaka wa fedha wa 2012/13.

Hatua hiyo inamaanisha kwamba kima cha chini cha mshahara sasa kitakuwa kati ya Sh. 180,000 hadi Sh. 200,000 kutoka Sh. 150,000 zinazolipwa sasa.

Vyanzo vya habari kutoka Serikalini vimeeleza kwamba nyongeza hiyo ya kati ya Sh.30,000 hadi Sh. 50,000 ni matokeo ya mazungumzo kati ya Serikali na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA).

Mbali ya kutaja kima hicho, vyanzo hivyo vimeeleza kuwa nyongeza hiyo inaweza kuvuka Sh. 50,000 kutegemea uwezo wa Serikali.

Katibu Mkuu wa TUCTA, Nicolaus Mgaya alipoulizwa jana alisema, “Tunaamini linaweza kutekelezeka, lakini hakuna anayejua nyongeza hiyo itakuwa ni kiasi gani, kwa hiyo ukinitajia kiwango nashindwa kuelewa umekitoa wapi...” “Wafanyakazi ni tabaka kubwa, lakini limesahaulika. Hii inatokana na Serikali kushindwa kusikiliza kilio chao cha kuwaongezea mishahara jambo ambalo limechangia kulipwa ujira mdogo na kusababisha wengi wao kukimbilia kwenye sekta binafsi, kutokana na hali hiyo tunaamini kuwa Serikali itasikilia kilio chetu,” alisema Mgaya

Mgaya alisema mbali na kuomba nyongeza mshahara, TUCTA pia imeiomba Serikali kupunguza gharama za tozo za mifuko ya hifadhi ya jamii huku ikienda pamoja na udhibiti wa mfumuko wa bei ambao umekuwa kikwazo kwa wafanyakazi na kuwafanya kuishi katika mazingira magumu kiasi cha kushindwa kujituma ipasavyo na wengine kukimbilia kwenye sekta binafsi.

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA