MTATIRO: HILI LA ZANZIBAR HALIUNGWI MKONO “LABDA NA MWENDA WAZIMU TU”
JULIUS MTATIRO katibu mkuu wa chama CUF Tanzania bara
*********************
Habari
za uchomaji wa makanisa Zanzibar katika vurugu za hivi karibuni
haziungwi mkono kwa namna yoyote ile. Yeyote anayefanya vitendo hivi ni
gaidi kwa sababu anafanya vitendo vya kigaidi. Serikali ya zanzibar
ichukue hatua kali sana za kisheria kwa yeyote aliyehusika na vitendo
hivi bila kujali yeye ni nani.
Kuchoma
makanisa ni jambo la hatari sana, sielewi anayefanya hivi yeye ni dini
gani, sijui ni dini ipi inayoruhusu uchomaji wa nyumba za ibada za dini
nyingine, ni dini ya shetani peke yake inaweza kufanya hivyo.
Kuna watu wanasema ati ni “waislamu” ndiyo wanafanya vitendo hivyo, mie nakataa, nasema wanaofanya hivyo siyo waislamu.
Waislamu
walioko Zanzibar naowajua mimi ni wakarimu, ni watulivu na wasikivu na
wanapenda amani. Hata mapambano ya wafuasi wa CUF na CCM yaliisha kwa
wao wenyewe kuridhiana.
Wazanzibari
siyo wakatili kiasi hiki. Kuchoma makanisa hakuwezi kufananishwa na
kuchoma Mahakama, ikulu,polisi n.k. Uchomaji wa makanisa au misikiti ni
uchonganishi mkubwa unaoibua vita mahali pengi duniani. Anayefanya
hivyo ana malengo mabaya sana siyo kwa wananchi wa Zanzibar tu bali kwa
wananchi wa wa Tanzania kwa ujumla.
Hii
ni kwa sababu makanisa yakishachomwa tetesi zinasema wamechoma
waislamu(jambo ambalo siliamini), tetesi hizi zikizidi na pakatokea
athari kubwa kwa makanisa na labda watu(wakristo) wakachomwa na
kufariki ndani ya makanisa hayo, ina maana wakristo watapoteza ndugu
zao.
Kama
Zanzibar pana wakristo wachache ambao hawawezi kulipiza kisasi cha adui
wasiyemjua, lazima ndugu zao wakristo walioko bara watataka kulipiza
kisasi kwa wazanzibari(waislamu) walioko Tanganyika ambao wamejenga na
kuoa na kufanya biashara Bara na ambao hata ZAN ID(Vitambulisho vya
ukaazi vya Zanzibar hawana) – kwamba kwa sheria za uraia za Zanzibar
hata wakirudi kesho hawatambuliki kama wazanzibari.
Nakadiria
kuwa kuna wazanzibari takribani laki tatu au laki nne walioko
Tanganyika. Wengi wao wana maduka na biashara nyingi, wamenunua
mashamba yao huku Tanganyika na kwa kweli maisha yao na vifo vyao na
maziko yao viko huku Tanganyika kila inapotokea.
Sasa
fikiria hawa “magaidi” wanaojivalisha na kusingizia waislamu
watakapoendelea kutuchonganisha na tukajikuta hasira zimepanda kila
upande. Utastukia mali za wakristo na makanisa yanachomwa na hata
wahusika kuuawa huko Zanzibar na utastukia pia wazanzibari walioko
Tanganyika nao wanaanza kuhujumiwa mali zao na kuuawa na “magaidi” wa
bara watakaojivisha joho la “ukristo” au “joho la kuwapigania ndugu zao
waliouawa Zanzibar” kwa maslahi yao.
Mchezo
huu utaendelea mbele, kwa sababu wazanzibari wengi watakaouawa na
kuhujumiwa huku Tanganyika ni waislamu(hii ni kwa sababu asilimia 99 ya
wazanzibari ni waislamu) itapelekea waislamu wenzao ambao ni mamilioni
walioko Tanganyika kutaka kuwatetea waislamu wenzao wenye asili ya
Zanzibar. Hapo ndipo itaibuka vita kamili ya dini ya kikristo na
kiislamu(Naomba haya yatokee wakati sipo duniani, naomba nisishuhudie
ukatili wa Rwanda ndani ya nchi ninayoipenda kama Tanzania).
Vita
ya kidini, lol! Mamilioni watateketea, malaki watachinjwa, akina mama
watabakwa, watoto watanajisiwa…..what a hell? Wendazimu wachache
waliochekewa watavaa majoho ya dini…..CNN watatangaza vita ya kidini
Tanzania, Mashirika ya kimataifa yataingiza misaada na geresha huku
nchi inahujumiwa.
Vikundi
vya waasi kina Kony na mwenzie nao wataingia kutuunga mkono, hatimaye
Tanzania itageuka kuwa jehanamu ya duniani. Nyerere na wenzie watakuwa
wanalia na kupiga vifua vyao kwa huzuni kuu. Kisiwa cha amani kimegeuka
kuwa Dimbwi la maafa na laana ya damu za mauaji.
Mambo
haya huanza kama mchezo tu. Na yameanza, hakuna mtu mwenye haki ya
kudai haki yake na kuhujumu mali za watu wengine na kuchoma makanisa ya
watu wengine. Wanaofanya vitendo hivi ni wahuni wakuu na serikali ya
Zanzibar ichukue hatua kali sana.
Uhuni
wa namna hii ulitokea pale Tandahimba mwezi uliopita ambapo “polisi”
walihusika “live” katika oparesheni ya kikatili ya kuchoma “waziwazi”
maduka zaidi ya 55 ya wafanyabiashara na gari moja na pikipiki moja.
Kabla hawajaanza oparesheni “ushenzi” hiyo “polisi” walitengeneza tukio
kwa “kuichoma” ofisi ya OCD ili wapate nafasi ya kulipiza kisasi kwa
wananchi wasio na hatia(kisasi cha kutengeneza) – Ujinga ulioje, aibu
iliyoje?
Pana makundi yanadai Zanzibari huru, yaachiwe uhuru wao, yasikilizwe.
Wajanja
wasijitokeze wakatumia upenyo huo ili kuyavunja makundi hayo kwa
kuyabambikizia uchomaji makanisa ili kuyahusisha na hila za dini moja
kuhujumu dini nyingine, tuache michezo hii ya kipuuzi. Siamini kama
uamsho na wanaharakati wale ndio wanachoma makanisa, naamini kuna janja
nyuma ya suala hili. Labda pana wajanja wanataka kuua “move” ya mjadala
wa kudai Zanzibari huru.
Majuzi
wazanzibari waliamua kuwa na serikali ya umoja wa kitaifa, wakapiga
kura wakaamua sawia na serikali yao ikawa, hawakutushirikisha kwa
sababu peke yao wanaweza kusimamia na kuendesha mambo yao na tumeona
wanaweza. Mie nasema wazanzibari wakidai Zanzibar huru yao tusiwapige
na kuwakamata na kuwanyanyasa, tukae nao mezani tusikilize hoja zao. Na
kama wengi wao wakitaka Zanzibar huru yao tuwape.
Baba
yangu mzee aliyeko kijijini hatapungukiwa na lolote iwapo Zanzibar
itaendeleza muungano na Tanzania au itajitoa. Zanzibar ikijitoa katika
muungano haitaongeza wala kupunguza kilo ya sukari au kilo ya mchele.
Watanzania wana matatizo makubwa yanayotishia uhai wao kila kukicha
kuliko muungano huku Tanganyika . Muungano ni jambo la kisiasa tu na
kama “mkuu wa kaya anasema usijadiliwe” lazima utavunjika tu, hana
namna ya kuuokoa maana kushindana na umma wa upande mmoja ni kazi bure.
Mie
nawashauri sana pia wana vikundi vya uamsho na na watu wote wanaodai
Zanzibari yao kuwa watumie busara na njia za kawaida sana kudai haki
yao wanayoiamini. Kwa sababu tume ya jaji warioba inakwenda kukusanya
maoni ya katiba waisubiri, ikifika waioneshe na waieleze kuwa hawautaki
muungano.
”Majority
of zanzibaris” wakiwa na msimamo huo maana yake ni kuwa katiba ya
Tanzania “itafeli” kwa sababu lazima ipitishwe na pande zote za
muungano kwa uwiano sawa. Hii ni njia nyepesi sana kuliko njia zingine,
wanaweza kuendelea kutoa elimu juu ya kuupinga muungano kwa njia ya
makongamano na mikutano tu. Hii itawasaidia kutengeneza mtizamo mzuri
na kuondoa uwezekano wa watu wowote wenye nia mbaya kutumia shughuli
zao na kujenga taswira mbaya sana zinazoweza kuweka amani, usalama na
mshikamano wa wananchi hatarini.
Mwisho
ni kwa serikali zote mbili, hii ya Jakaya na ile ya Shein na Maalim
Seif. “Movement” hii ya uamusho na makundi mengine ya kijamii,
kiharakati na kidini upande wa Zanzibar ya kudai kuvunja muungano siyo
jambo la kubeza na kuchezea. Ukiwatizama wale uamsho utaona umati wa
watu wanaokusanya ni mkubwa kuliko mikutano ya hadhara ya vyama vya
siasa. Hii ina maana kuwa panahitajika busara na nia thabiti katika
kumalizana na wananchi hawa.
Serikali
zote mbili zikae nao chini na kutatua suala hili. Ni bora kuuvunja
muungano kwa heri(kwa utaratibu), kuliko kuuvunja kwa nguvu. Muungano
ukivunjika kwa nguvu na ghafla patatokea mpasuko mkubwa sana. Pana
ma-laki ya wazanzibari wako Tanganyika, pana mahusiano makubwa
yameshajengwa. Tunahitaji “mechanism”na akili nyingi kulishughulikia.
“Nguvu
na mabavu havitasaidia kuzima mawazo thabiti ambayo wananchi
wanayaamini, nguvu na majeshi vinaweza kuua mwili tu lakini haviui
dhamira” Hata kama wananchi hawa watapigwa na kukamatwa na kuwekwa
gerezani moto huu hautazimika.
Muungano utizamwe upya, tusikilize matakwa ya wananchi wengi, ikiwa wengi watasema uvunjwe basi na tuuvunje kwa amani.
(Haya ni maoni yangu binafsi, kwa namna yoyote ile yasihusishwe na chama changu wala uongozi wangu ndani ya chama).
Julius Mtatiro +255 717/787/ 536759,
Dar es salaam,
29 Mei 2012.
Dar es salaam,
29 Mei 2012.
Comments
Post a Comment