WIZARA YA MALI ASILI YAKANUSHA VIKALI KUHUSU "KASHIFA YA UGAWAJI VITALU KWENYE MAENEO YA HIFADHI"

 
Wizara ya Maliasili na Utalii imekanusha habari iliyoandikwa na gazeti moja la kila wiki lililotoka tarehe 15 Mei 2012 kwa kichwa cha habari ‘Kashfa mpya Maliasili’ zinazohusu ugawaji wa vitalu kwenye maeneo ya Jumuiya ya Hifadhi za Wanyamapori (Wildlife Management Areas -WMAs).Wizara haihusiki na ugawaji wa vitalu ambao uliripotiwa na gazeti hilo kwa kuwa maeneo ya WMA yako nje ya Mapori ya Akiba ambayo ndiyo yanasimamiwa na Wizara moja kwa moja. 
 
Gazeti hilo linanukuu tangazo ambalo lilitolewa na Muungano wa Jumuiya Zilizoidhinishwa za Hifadhi za Maeneo ya Wanyamapori Tanzania (Authorized Associations AAs Consortium) kuhusu vitalu. Tangazo hilo ambalo lilitolewa kwa njia ya magazeti liliwataka wadau wapeleke maombi ya vitalu vya uwindaji wa kitalii vilivyoko katika Maeneo ya Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMAs) kwa kipindi cha mwaka 2013 hadi 2018 . 
 
Inasisitizwa kuwa tangazo hilo la vitalu halikutolewa na Wizara wala Wizara haikuhusishwa kwa vyovyote vile katika kuandaa tangazo hilo. Hivyo, habari iliyotolewa na gazeti hilo  la kila wiki baada ya tangazo hilo kuchapishwa kuwa ugawaji wa vitalu vya WMA ni ‘Kashfa mpya Maliasili’ siyo kweli. 
 
Tangazo lililotolewa na Muungano wa Jumuiya Zilizoidhinishwa za Hifadhi za Maeneo ya Wanyamapori Tanzania (Authorized Associations- AAs Consortium) siyo sahihi kwani Kifungu cha 31 (7) cha Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 kilichonukuliwa katika Tangazo hilo hakikuzingatiwa ipasavyo kwa misingi ifuatayo:- 
 
    i.   Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori hakushirikishwa na hakutoa ridhaa yake  kabla ya tangazo hilo kutolewa;

 ii. Halmashauri za Wilaya viliko vitalu hivyo nazo hazikushirikishwa; na

    iii.  Kifungu hicho [31(7)] hakitoi mamlaka kwa Muungano wa Jumuiya Zilizoidhishwa (Authorized Associations-AAs Consortium) kutoa tangazo la vitalu vya uwindaji wa kitalii katika Maeneo ya Jumuiya ya Hifadhi za Wanyamapori (WMAs).

  iv. Kanuni zinazotumika sasa hazitoi utaratibu utakaotumika kupata wawekezaji katika vitalu vya uwindaji wa kitalii vilivyoko katika WMAs. Kanuni za WMAs zinafanyiwa marakebisho na zitakapokamilika zitatoa utaratibu utakaotumika katika kutangaza vitalu vilivyopo kwenye WMAs.
 
Kutokana na sababu hizo Wizara ya Maliasili na Utalii inatahadharisha kuwa tangazo hilo siyo sahihi kwa kuwa halikuzingatia sheria. Kwa hiyo wadau wa uwindaji wa kitalii wanatahadharishwa kutopeleka maombi ya vitalu hivyo. 
 
Wizara imewasiliana na Muungano wa Jumuiya Zilizoidhinishwa za Hifadhi ya Maeneo ya Wanyamapori Tanzania (Authorized Associations - AAs Consortium) kuwataka wasitishe mchakato huo wa kugawa vitalu katika maeneo ya WMA.
Wizara inazitaka Jumuiya za Hifadhi ya Wanyamapori (WMAs) kuwasiliana kila zinapotaka kutekeleza masuala yoyote yanayotawaliwa na sheria maana Wizara ndiyo yenye dhamana ya kusimamia Sera na Sheria za Wanyamapori.

George Matiko
MSEMAJI
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
16 Mei 2012
                                                     Simu 0784 468047

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA