FARU WA JK AWANG'OA VIGOGO MALIASILI

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki ameanza kutekeleza kwa vitendo kauli yake ya kuisafisha Idara ya Wanyamapori baada ya kuwasimamisha kazi wakurugenzi wanne na askari 28 wa Hifadhi ya Taifa Serengeti, Mara ili kupisha uchunguzi wa tukio la kuuawa kwa faru wawili na kung’olewa pembe.

Faru hao ni miongoni mwa watano ambao Rais Jakaya Kikwete aliwapokea wakitokea Afrika Kusini, Mei 21, 2010 lakini Desemba 21, mwaka huo faru dume aitwaye george aliuawa na pembe zake zilinaswa Mwanza. Faru wengine wanne walipewa majina ya cleo, ethna, lunnar na dume pekee aliyebaki, benj.

Wakati akipokea faru hao waliogharimu Sh7.5 bilioni kuanzia ununuzi hadi kuwasafirisha hadi nchini, Rais Kikwete alisema: “Afrika Kusini imeongeza uwezo kwa Tanzania kwa kuleta faru hao weusi na ongezeko hilo ni la manufaa kwa taifa. Hivyo, tutaimarisha huduma zao na ulinzi utakuwa wa kipekee zaidi yangu mimi.”

Lakini tofauti na ulinzi huo alioahidi Rais, kumekuwa na taarifa za kuawa kwa faru wengine wawili hivi karibuni na mamlaka husika zikaficha tukio hilo hadi liliporipotiwa na vyombo vya habari. Takwimu zinaonyesha tangu mwishoni mwa 2009 hadi Desemba 2010, faru 15 wamekwishauawa.

Balozi Kagasheki alisema jana kwamba amechukua hatua hiyo kutokana na wakurugenzi hao kukaa kimya baada ya tukio hilo na askari hao wakidaiwa kukiuka mkataba wao wa ajira ambao unawataka watoe ulinzi kwa wanyamapori.

“Mkataba wao upo wazi kuwa wanapaswa kuwalinda wanyamapori hao na lolote linalowapata liwapate na wao pia, lakini wanyama wameuawa mwezi mzima umepita na wiki mbili baadaye gazeti linaandika ndipo Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa), wanachukua hatua,” alisema.

Waziri Kagasheki pia alisema wahusika hao wameundiwa tume huru ambayo itafanya kazi ndani ya siku 60 na watakaobainika kuhusika kwa namna moja au nyingine, watachukuliwa hatua zaidi za kisheria na wale ambao watathibitika kuwa hawahusiki taratibu nyingine zitafuatwa.

Aliwataja wakurugenzi ambao wamesimamisha kazi kuwa ni Kaimu Mkurugenzi wa Uhifadhi, Justine Hando, Mkurugenzi wa Intelejensia katika Wizara hiyo, Emmly Kisamo, Mkurugenzi wa Hifadhi ya Serengeti, Mtango Mtahiko na Mkurugenzi Mratibu wa Mradi wa faru, Mafuru Nyamalumbati.

Alisema anachukua hatua hizo ambazo ni tofauti na utaratibu wa kawaida kutokana na kukithiri kwa vitendo vya ovyo ambavyo vinaichafua wizara yake.

“Kwanza niliwauliza baada ya kupatikana kwa habari za kuuawa kwa faru hao walichukua hatua gani? Jibu likawa tumewapa siku 14 wajieleze,” alisema Kagasheki na kuongeza kuwa watendaji hao wakamwambia kuwa maelezo hayo yasiporidhisha hatua itakayofuata ni kuundwa tume.

Kagasheki alifafanua kwamba alipohoji muda wa utendaji wa tume hiyo, aliambiwa ni siku 60 jambo ambalo alilikataa na kuchukua uamuzi wa kuwasimamisha ili kupisha uchunguzi huo na kudai kuwa watendaji hao kama wangeachwa wangeweza kuwa na athari zaidi kwa hifadhi na wanyamapori.

Alisema wizara yake haiwezi kufanya kazi kwa woga na kusema yupo vitani akiahidi kupambana kuondoa uozo unaodaiwa kuigubika.

Alisema anajua kuwa kuna mtandao wa ujangili ndani na nje ya nchi ambao una fedha nyingi lakini akasema hatarudi nyuma… “Faru ni moja kati ya viumbe hai ambavyo vipo hatarini kutoweka hivyo kilichotokea hakivumiliki.”

Alisema kuwa mara baada ya kuandikwa kwa habari hizo, walikwenda hadi eneo la tukio na kukuta miili ya wanyama hao wakiwa wameondolewa pembe zao na jirani kukiwa na maganda ya risasi… “Tumewakuta mama na mwanaye wameuawa na pembe zao kuondolewa. Inasikitisha sana.”

Mei 21 akizungumza Dar es Salaam katika uzinduzi wa Bodi ya Ushauri ya Wizara ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Balozi Kagasheki alionya kwamba angeifumua Idara hiyo ya Wanyamapori huku akipiga marufuku usafirishaji wanyama hai nje ya nchi.

Alisema kama idara hiyo itasimamiwa vizuri kukusanya mapato, inaweza kusaidia kupunguza matatizo ya wananchi.


Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA