Watuhumiwa wa CAG ‘kuanikwa’ wakati wowote

MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hosea amesema taasisi yake itatoa orodha ya vigogo wanaochunguzwa baada ya kutuhumiwa katika ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).


Akizungumza kwa simu na gazeti hili jana, Dk Hosea alisema kuna hatua za kiuchunguzi wameanza kuchukua baada ya kutolewa kwa ripoti ya CAG ambayo imeainisha ulaji mkubwa uliofanywa katika mashirika ya umma, Serikali Kuu na Serikali za Mitaa.

“Lakini kwa leo (jana) siwezi kukutajia, kwa sababu niko katika eneo ambalo haliruhusu nikutajie, ila tumedhamiria kuwataja kwa wanahabari, kwa sababu mnaulizia sana suala hilo,” alisema Dk Hosea.


Hata hivyo, hakuwa tayari kutaja siku ambayo atawataja vigogo hao, badala yake akasema ni siku yoyote watakayokuwa tayari kuanzia leo.


Mkurugenzi huyo alisema licha ya CAG kutoa taarifa hiyo, lakini Takukuru ambayo kazi yake ni kuchunguza, imekuwa ikichunguza baadhi ya watu ambao wametajwa kwenye ripoti hiyo.


Katika ripoti ya CAG ambayo ilisababisha wabunge kuisulubu Serikali na kushinikiza baadhi ya mawaziri wawajibishwe, kuna taasisi na wizara ambazo zinaonesha kuwa na ufujaji mkubwa wa fedha za umma.


Moja ya maeneo ambayo yamefanya vibaya zaidi ni baadhi ya halmashauri za wilaya ambako malipo mengi yamefanywa bila ushahidi wa stakabadhi.


Pia kuna watumishi hewa ambao wamelipwa mishahara hewa. Katika Serikali Kuu, CAG amenyoosha kidole kwa watendaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ambayo ilituhumiwa kutumia Sh bilioni 1.1 katika maonesho ya Nanenane. Waziri wake Dk. Hadji Mponda na Naibu wake Dk. Lucy Nkya, wameondolewa kwenye nyadhifa zao kisiasa.


Wizara ya Fedha pia ilitajwa na CAG kuuza mali za Serikali bila kushirikisha Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC). Waziri wake Mustafa Mkulo naye aliwajibishwa kisiasa kwa kuvuliwa wadhifa wake baada ya kushutumiwa na wabunge wengi, kuwa anahusika na uuzaji wa mali hizo za Serikali.


Aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami aliondolewa kwa tuhuma za kumlinda Mtendaji Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Charles Ekerege, anayetuhumiwa kutumia Sh bilioni 38 kulipa kampuni hewa za ukaguzi wa magari nje ya nchi.


William Ngeleja ambaye alikuwa Waziri wa Nishati na Madini ameondolewa kutokana na wizara hiyo kugubikwa na kashfa ya rushwa katika ununuzi wa mafuta ya kuzalishia umeme wa dharura katika mitambo ya Agreko na IPTL.


Ezekiel Maige ambaye pia aliondolewa, alituhumiwa kugawa vitalu vya uwindaji kwa kampuni zaidi ya 10 bila utaratibu. Suala hilo lilipigiwa kelele na Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira.


Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu na Naibu wake Athuman Mfutakamba, walijikuta wanaogelea katika kashfa kutokana na kila mmoja kudaiwa kukumbatia kampuni yake kati ya zilizokuwa zinawania ujenzi wa gati namba 13 na 14 za Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).


Mawaziri ambao walipona licha ya kuguswa na ripoti ya CAG ni George Mkuchika aliyekuwa anaongoza Tamisemi, ambako kuna madudu mengi na tayari Waziri Mkuu ameshaagiza wakurugenzi wa halmashauri za wilaya za Geita na Sengerema kushitakiwa.

Waziri mwingine ni Profesa Jumanne Maghembe ambaye Wizara yake Kilimo, Chakula na Ushirika inatuhumiwa kuagiza mbolea isiyo na ubora ambayo iliathiri mazao ya wakulima.

Wizara hiyo pia ilituhumiwa kuwakumbatia watendaji wa Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) ambao wanadaiwa kutafuta Sh bilioni 2.4 zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya kuwalipa wakulima wa pamba.


Chanzo: Habarileo

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA