SIMBA YAFANYA KUFULU YA MABAO KWA WATANI WAO WA JADI YANGA

Waziri wa Habazri, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk Fenela Mkangara akimkabidhi kombe nahodha wa timu ya Simba Juma K. Juma baada ya timu ya Simba kuifunga Yanga magoli 5-0 kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar salaam katika mchezo uliokuwa ni wa  kumaliza michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom uliomalizika jioni hii  kwenye uwanja wa Taifa, huku ikiwa tayari ni mabingwa wapya wa ligi hiyo, Simba imefanikiwa kutunza heshima yake baada ya kuifunga Yanga magoli 5 kupitia wachezaji wake Emmanuel Okwi, goli la kwanza.  

Goli la pili la Simba likafungwa na mchezaji Felix Sunzu kwa njia ya penati na dakika chache baadae Emmanuel Okwi akaongeza goli la tatu , Juma Kaseja akaongeza goli la nne kwa penati wakati pia Patrick Mafisango akafunga hesabu kwa kufunga  goli la tano baada ya wachezaji wa Yanga kufanya makosa katika eneo la hatari  

Mchezaji wa timu ya Simba mganda Emmanuel Okwi akishangilia goli mara baada ya kuifungia timu yake goli la kuongoza
Wachezaji wa Simba wakishangilia baada ya kukabidhiwa kombe  leo kwenye uwanja wa Taifa jioni hii.
Waziri wa Habazri, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk Fenela Mkangara akimvisha Medali mtoto wa mchezaji Uhuru Selemani wa Simba.
Waziri wa Habazri, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk Fenela Mkangara akimvisha medali mshabuliaji wa Simba Emmanuel Okwi.
Wachezaji wa timu ya Simba wakishangilia na kocha wao kwa kumbeba juu juu.
Luninga kubwa ya uwanjani ikionyesha magoli yaliyofungwa na Simba

SIMBA ALAMBA, ALAMBA, ALMBA TENA AAMH!

Okwi akishangilia moja ya mabao yake. picha hisani ya Full Shangwe

WEKUNDU wa Msimbazi, Simba SC jioni hii wamekabidhiwa Kombe lao la ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania kwa shangwe nzito, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya kuwabwaga wapinzani wao wa jadi, Yanga mabao 5-0.
Mabao ya Simba yalifungwa na Emmanuel Okwi mawili, Juma Kaseja, Felix Sunzu na Patrick Mutesa Mafisango.
Hiki ni kipigo cha pili kihistoria Simba wanaifunga Yanga, baada ya zile 6-0 za mwaka 1977.
Ilikuwa ni hoi hoi, nderemo na vifijo kuanzia Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam hadi kona mbalimbali za Jiji, rangi nyekundu na nyeupe zikiwa zimetawala na shangwe za Simba.
Hadi mapumziko, Simba walikuwa tayari mbele kwa bao 1-0, lililofungwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Arnold Okwi dakika ya kwanza tu ya mchezo huo.
Okwi alimtungua kipa Mghana, Yaw Berko baada ya kutumia mwanya wa kuzubaa kwa mabeki wa Yanga mwanzoni mwa mchezo huo.
Katika kipindi hicho, Okwi alikuwa akimpita kwa urahisi beki mkongwe wa Yanga, Nsajigwa Shadrack Joel Mwandemele ambaye aliishia kumkwatua mara kwa mara, jambo ambalo lilimponza kwenda chumba cha kupumzikia akiwa ana kadi moja ya njano aliyopewa dakika ya 39.
Pamoja na kufungwa bao hilo, Yanga waliendelea kucheza kwa utulivu, wakigongeana pasi vizuri na kutengeneza nafasi kadhaa, ingawa kikwazo kilikuwa Tanzania One, Juma kaseja.
Nafasi pekee nzuri katika kipindi hicho na ambayo Yanga wataijutia waliipata dakika ya 35, baada ya Mwanasoka Bora wa Uganda, Hamisi Kiiza kuwatoka vizuri mabeki wa Simba, lakini akiwa amebaki yeye na kipa, hesabu zake ziliendana na Kaseja.
Kiiza aliupelekea mpira upande wa kushoto wa kipa huyo bora Tanzania, ambaye naye akachupa upande huo huo na kuokoa.
Kipindi cha pili, Yanga walianza kwa mabadiliko, wakimtoa kipa Yaw Berko na kumuingiza Said Mohamed Kasarama, wakati Simba walimpumzisha Mwinyi Kazimoto na nafasi yake kuchukuliwa na Jonas Mkude.
Simba waliingia tena kwa kasi na kufanikiwa mabao matatu ya haraka haraka, mawili yakipitia kwa Nsajigwa.
Bao la pili la Simba lilitokana na penalti, baada ya Nsajigwa Shadrack kumkwatua Okwi kwenye eneo la hatari na Felix Sunzu akaenda kufunga kwa penalti.
Okwi alifunga bao la tatu dakika ya 52, baada ya kumtoka Nsajigwa Fusso na kumchambua kipa Said Mohamed Kasarama.
Baada ya bao hilo, kocha Fred Felix Minziro alipumzishwa Nsajigwa na kumuingiza Godfrey Taita Magina.  
Dakika ya 66 Uhuru Suleiman aliangushwa na Taita kwenye eneo la hatari na Juma Kaseja akaenda kufunga bao la nne kwa penalti.
Patrick Mafisango alifunga bao la tano kwa penalti pia dakika ya 73.
Simba SC: Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Amir Maftah, Shomary Kapombe, Kelvin Yondan, Patrick Mafisango/Obadia Mungusa, Uhuru Suleiman, Mwinyi Kazimoto/Jonas Mkude, Felix Sunzu/Edward Christopher, Haruna Moshi ‘Boban’ na Emmanuel Okwi.
Yanga: Yaw Berko/Said Mohamed, Nsajigwa Shadrack/Godfrey Taita, Oscar Joshua, Athumani Iddi ‘Chuji’, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Juma Seif ‘Kijiko’, Nurdin Bakari, Haruna Niyonzima, Davies Mwape/Kenneth Asamoah, Rashid Gumbo na Hamisi Kiiza.
 
SOURCE: BIN ZUBEIRY (http/bongostaz.blogspot.com)

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA