Mahakama yathibitisha Mahanga ndiye Mbunge halali wa Segerea

Dkt. Milton Makongoro Mahanga
Dkt. Mahanga
Mbunge wa Segerea, Dkt. Milton Makongoro Mahanga (CCM) amekitetea vyema kiti chake cha Ubunge wa Segerea, Dar es Salaam kwa kushinda kesi iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea wa Ubunge wa jimbo hilo Fred Mpendazoe (CHADEMA) iliyokuwa inapinga ushindi uliopatikana katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2010.

Mpendazoe anapaswa kulipa gharama zote za kuendesha kesi hiyo.

Hukumu ya kesi hiyo namba 98 ya mwaka 2010 iliyosomwa leo na Jaji Profesa Ibrahimu Juma ambaye amekuwa akiisikiliza tangu ilipofunguliwa Novemba 10, 2010,  ilikuwa ikipinga ushindi wa Mahanga kwa madai kuwa sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi zilikiukwa katika hatua ya kuhesabu, kujumlisha kura na kutangaza matokeo. Mbali na Dkt. Mahanga ambaye alikuwa mdaiwa wa pili katika kesi hiyo, mdaiwa wa kwanza alikuwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na wa tatu alikuwa ni Msimamizi wa Uchaguzi (RO), katika jimbo hilo.

Kutokana na dosari hizo, Mpendazoe ambaye alikuwa akiwakilishwa na Wakili Peter Kibatala, aliiomba Mahakama itengue matokeo hayo na iamuru uitishwe uchaguzi mwingine mdogo katika jimbo hilo au imtangaze yeye kuwa mshindi akidai kwamba alipata jumla ya kura 56,962 na Mahanga kura 44,904. Hata hivyo,  Jaji Prof. Juma alisema ushahidi wa upande wa mlalamikaji umebainika kuwa na mapungufu na hivyo kutupilia mbali ushahidi huo ambao uliokuwa na hoja kumi kwa kutokukidhi matakwa ya kifungu 108 na hivyo kumpa ushindi Dkt. Mahanga.

Dkt. Mahanga alikuwa akitetewa na Mawakili Jerome Msemwa na Aliko Mwamanenge na AG na RO wamekuwa wakitetewa na Mawakili wa Serikali, David Kakwaya na Seth Mkemwa.

Wakati wa ushahidi wake, upande wa madai uliwaita mahakamani mashahidi 13 akiwemo mlalamikaji mwenyewe Mpendazoe na wadaiwa wote watatu kwa pamoja waliwaita jumla ya mashahidi 16.

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA