HESLB: Hii ndio mbinu mpya kuwabana wanaokwepa kurejesha mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu

Serikali
imetangaza kuwa haitawaruhusu wahitimu wa elimu ya juu wanaodaiwa na
Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kwenda nje ya nchi kwa masomo
zaidi au kufanya kazi mpaka watakapomaliza kulipa madeni yao.
Akizungumza
bungeni hivi karibuni, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi,
Jenista Mhagama alisema hatua hiyo inalenga kuongeza kiwango cha
ukusanyaji wa mikopo ambayo imeshawanufaisha wahitimu wengi ingawa ni
wachache wanaorejesha.
"Tumezungumza
na idara ya uhamiaji ili wale wote wanaotaka kwenda kufanya kazi nje ya
nchi wasiruhusiwe mpaka watakapomaliza kulipa mikopo yao ya elimu ya
juu. Lengo ni kuepuka ukwepaji unaojitokeza baada ya kuajiriwa,"
alisema.(Martha Magessa)
Suala la
wahitimu wa Kitanzania kutafuta kazi nje ya nchi limekuwa likizungumzwa
na wadau wengi kama njia mbadala ya kupata ajira, kutokana na kuwapo kwa
ushindani mkubwa wa soko la ndani la ajira.
Wahitimu
Hata
hivyo, baadhi ya wadau hawaoni manufaa endelevu ya mpango huo, wakisema
chombo kinachohusika na mikopo hakijajipanga vilivyo kukusanya madeni na
ndiyo maana kimeshindwa kuwafikia hata wadaiwa waliomo nchini.
Leonard
Mhongole ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha Ardhi mwaka 2010. Anasema mkakati
huo hauwezi kuleta tija kwa kuwa ni watu wachache sana wanaofikiria
kwenda nje ya nchi.
"Mamlaka
husika zinaangalia sana waajiriwa wa serikalini lakini kwa wale
tunaofanya kazi sekta binafsi au waliojiajiri hatufikiwi. Kama watu wote
watabanwa kama inavyotakiwa nadhani fedha za kutosha zitarudi
serikalini," anasema na kuongeza:
"Mimi
binafsi nilitakiwa niwe nimeanza kulipa mkopo wangu lakini kwa kuwa
hakuna anayenitaka kufanya hivyo siwezi kuwatafuta
wahusika...inawezekana wametoa msamaha kwa baadhi ya watu."
Kwa
upande wake, mwanafunzi wa shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam, Joseph Isindikiro, anasema utekelezaji wa mkakati huo ni
ukiukwaji wa haki ya msingi ya mtu kupata elimu.
"Mpango
huo hautawezekana kwa sababu serikali yenyewe imekiri kuwa kuna tatizo
la ajira na kupendekeza wahitimu kuomba kazi nje ya nchi. Sasa itakuwaje
wao wenyewe wazuie ilhali wanajua mhusika hana uwezo huo na ajira hiyo
ndiyo tegemeo lake?" anahoji.
Anaongeza
kusema kuwa kufanya hivyo ni sawa na kumtia mtu hatiani kutokana na
haki yake ya kupata elimu kama inavyobainishwa katika Katiba.
CHANZO:MWANANCHI
Comments
Post a Comment